Kuna masaa 24 pekee kwenye siku, imekuwa hivyo tangu dunia imeanza na itaenda hivyo miaka yote ambayo dunia itakuwepo.
Kila mtu ana masaa hayo 24, hakuna anayeweza kupata hata sekunde moja ya ziada.
Lakini karibu kila mtu analalamika kwamba muda haumtoshi. Hii ni sababu ambayo wengi wanaitumia kama kikwazo kwao kupiga hatua.
Lakini kama ambavyo tumeona, hakuna anayeweza kupata muda zaidi, hivyo kusema muda hautoshi, hakuwezi kukusaidia kuondoka pale ulipokwama sasa.
Kitu pekee kinachopelekea muda unakuwa hautoshi ni kwa sababu tunajaribu kufanya vitu vingi ndani ya muda mfupi. Kujaribu kuweka vitu vingi kwenye muda mfupi ni sababu kubwa ya kufanya muda usitutoshe.
Na hivyo njia pekee ya kuondokana na uhaba huu wa muda, ni kuacha kufanya mambo mengi kwa muda mfupi ulionao. Weka vipaumbele kwa mambo gani utafanya na yapi utaachana nayo.
Na vipaumbele vyako ni matokeo ya malengo na mipango ambayo mtu unakuwa nayo kwenye maisha. Jua kipi hasa unachotaka kwenye maisha, kisha kabla hujafanya chochote jiulize kama kina mchango wowote kwa wewe kufika kule unakotaka kufika. Kama hakina mchango usifanye.
Kama unajiambia huna muda, basi neno HAPANA linapaswa kuwa rafiki yako wa karibu, unapaswa kupunguza sana mambo mengi unayofanya sasa, ambayo hayachangii wewe kufika kule unakotaka kufika.
Na kila mtu, bila kujali yupo ‘bize’ kiasi gani, kuna muda mwingi sana ambao anaupoteza kwenye mambo yasiyo muhimu kwake kufika kule anakotaka kufika. Ni wajibu wako kujua yale yasiyo muhimu na kuacha kuyafanya.
Kufuatilia habari, mitandao ya kijamii, kubishana, vikao visivyo na tija na hata kufuatilia maisha ya wengine ni mambo ambayo ukichagua kuyafanya umechagua kupoteza muda wako.
Leo fanya usafi kwenye muda wa maisha yako, angalia kila kitu kinachochukua muda wako kisha jiulize kama ni muhimu. Kama siyo muhimu acha mara moja kukifanya, hata kama umezoea kufanya na hata kama kila mtu anafanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,