Rafiki yangu mpendwa,

Sisi binadamu huwa tunajidanganya sana. Huwa tunajiita ni viumbe wa kufikiri, kwamba tunafanya maamuzi yetu baada ya kufikiri kwa kina. Lakini kwa uhalisia sisi ni viumbe wa kihisia, tunasukumwa na hisia katika kufanya maamuzi yetu.

Changamoto kubwa ni kwamba maamuzi yoyote ambayo tunayafanya kwa kusukumwa na hisia, huwa siyo maamuzi mazuri kwetu. Ni maamuzi mabovu ambayo yanatugharimu sana baadaye.

Na wale wenye uelewa wa makosa haya tunayoyafanya kwenye maamuzi, wamekuwa wanayatumia kwa kujinufaisha wao wenyewe. Mfano wafanyabiashara wamekuwa wakikusukuma wewe ununue wanachouza kwa kuibua hisia mbalimbali ndani yako, hata kama huhitaji sana kile wanachouza.

Swali; je umewahi kukutana na mtu anauza kitu ambacho huna uhitaji nacho, lakini baada ya kuongea na wewe ukajikuta umenunua kitu hicho, lakini baada ya kufika nyumbani ukajutia kwa nini umenunua? Je umewahi kumwona mtu kwa nje ukamwamini na kuona ni mtu wa heshima lakini akakutapeli au kukudhulumu na hukuamini angeweza kufanya hivyo? Kama umewahi kukutana na hali hizo, au zinazofanana na hizo, basi jua umekuwa unafanya makosa ya kisaikolojia ambayo yanakupelekea kufanya maamuzi mabovu na yanayokugharimu.

Mwandishi Peter Bevelin kwenye kitabu chake cha SEEKING WISDOM; From Darwin to Munger ametushirikisha makosa 28 ya kisaikolojia tunayoyafanya na kutupelekea kufanya maamuzi mabovu na yanayotugharimu sana.  Makosa haya 28 amejifunza kutoka kwa wanafalsafa, wanasaikolojia, wanasayansi na hata wawekezaji wenye mafanikio makubwa.

misjudgement

Kwenye makala hii ya leo nakwenda kukushirikisha makosa haya kwa kifupi na hatua za kuchukua ili uache kufanya maamuzi mabovu na yanayokugharimu.

 1. Uhusiano usio sahihi.

Huwa tuna tabia ya kuweka uhusiano usio sahihi kwa vitu viwili vinavyotokea kwa pamoja. Kama kuna kitu ambacho tunajisikia vizuri kufanya tunakifanya hicho, na kama kuna kitu tunajisikia vibaya tunakwepa kukifanya.

Wanasiana na wafanyabiashara wanaelewa hili na kulitumia vizuri, wanapotaka ukubaliane na kile wanachotaka ufanye, wanakihusisha na mambo mazuri yanayoibua hisia zako za kutaka kufanya kitu hicho, hata kama hakina manufaa kwako. Mfano eneo la biashara linakuwa na mwonekano mzuri na sana, halafu bei ya vitu inakuwa juu, unapoangalia bei hiyo na mazingira uliyopo, unaona unastahili kuilipa, hata kama ungeweza kupata kwa bei ya chini sehemu nyingine.

Hatua ya kuchukua; acha kuleta uhusiano baina ya vitu, badala yake fikiria na chambua kitu kwa thamani yake na umuhimu wake kwako. Na pale unapotaka kubadili tabia za wengine, tengeneza mazingira ambayo yanawafanya wajisikie vizuri kufanya kitu unachotaka wafanye, au wajisikie vibaya pale wanapofanya kitu ambacho hutaki wafanye.

 1. Zawadi na adhabu.

Huwa tunafanya kile ambacho tunazawadiwa tukifanya na kuepuka kile ambacho tunaadhibiwa tukifanya. Hivi ndivyo tunavyojenga tabia zote, kwa kurudia kile tunachopata zawadi tukifanya na kuepuka kile ambacho tunapewa adhabu tukifanya.

Wale wanaotaka kunufaika kupitia sisi, huwa wanatupa zawadi ndogo ili kutusukuma kufanya kile wanachotaka tufanye. Au kutunyima kitu pale tunapoacha kufanya kile wanachotaka tufanye.

Hatua ya kuchukua; kama kuna watu unataka wabadili tabia zao, tumia vizuri zawadi na adhabu, wape zawadi pale wanapofanya kile unachotaka wafanye na wape adhabu pale wanapofanya kitu cha tofauti. Katika kujenga tabia imara, zawadi ina nguvu kuliko adhabu. Hivyo angalia fursa zaidi za kutoa zawadi pale mtu anapofanya vizuri.

 1. Maslahi binafsi na marupurupu.

Tunasukumwa kufanya vitu ambavyo vina maslahi kwetu, ambavyo vinatupa nafasi ya kupata zaidi. Kama kitu hakiendani na maslahi yetu huwa hatuhangaiki nacho.

Kila mtu anayetaka kukuuzia kitu, ana maslahi nyuma yake, kila anayekushawishi ufanye kitu fulani, kuna maslahi anayopata kwa wewe kufanya. Huwa watu hawaweki maslahi haya mbele, na kutufanya tuamini kwamba wanafanya kwa kuwa wanatupenda sana.

Hatua ya kuchukua; kwa kila ambalo watu wengine wanakutaka ufanye, kwa kila ushauri unaopokea kutoka kwa wengine, jiulize swali hili moja, watu hao wana maslahi gani kwa wewe kufanya wanachotaka ufanye? Angalia kwa kina na utaona kuna maslahi wao wanapata. Ukishayajua maslahi ya wengine unaweza kufanya maamuzi kwa usahihi.

 1. Matumaini yaliyopitiliza.

Kila mtu huwa anakuwa na matumaini kwake, lakini kwa wengi matumaini haya yamepitiliza. Huwa tunaona wengine wakikosea na kushindwa, lakini tunajiona sisi hatuwezi kufanya makosa kama yao, hatuwezi kushindwa kama wao, na hilo linapelekea kuanguka vibaya sana.

Tunapofanikiwa kwenye kitu huwa tunajipa sifa sisi wenyewe, tunaona mafanikio hayo yametokana na juhudi zetu na uwezo wetu mkubwa. Lakini tunaposhindwa, huwa lawama tunazipeleka kwa wengine, kuona wao wamesababisha sisi kushindwa.

Hatua za kuchukua; matumaini ni mazuri, lakini uhalisia ni bora zaidi. Angalia uhalisia, kwa kujua uwezo wako halisi na ukomo wako, na kujua changamoto unazoweza kukutana nazo kwenye chochote unachofanya na jinsi ya kuzivuka.

 1. Kujidanganya na kuukataa ukweli.

Huwa tunajidanganya sisi wenyewe na kuukataa ukweli, huwa tunaona kile ambacho tunataka kuona na kusikia kile ambacho tunataka kusikia. Tukishafanya maamuzi yetu, tunatafuta taarifa zinazokubaliana na maamuzi ambayo tumeshayafanya. Hata tunapoomba ushauri, tunachagua kuwasikiliza wale wanaokubaliana na sisi.

Hatua ya kuchukua; epuka kujidanganya wewe mwenyewe, uangalie uhalisia jinsi ulivyo. Kama kuna kitu unataka kujua, basi kuwa tayari kupokea taarifa na ushauri ambao utakuumiza.

Huwa tuna tabia ya kufanya kitu kwa sababu tumekuwa tunakifanya, tunapenda kuwa na msimamo. Hali hii imekuwa inatupelekea kufanya maamuzi mabovu. Mfano wafanyabiashara wanajua ukishanunua kitu kimoja, basi ni rahisi kwako kununua kitu kingine, kwa sababu unapenda msimamo, hivyo unaponunua kitu, wanakuonesha kitu kingine kizuri unachoweza kununua pia.

Pia msimamo huu umekuwa unatufanya tupate hasara kubwa kwa sababu tu hatutaki kubailika. Mfano mtu umeingia kwenye biashara fulani, ambayo haikulipi, lakini hutaki kuacha nayo kwa sababu unaona umeshaweka muda na fedha nyingi, hivyo unaendelea kupoteza muda na fedha zako.

Hatua ya kuchukua; usifanye kitu kwa sababu tu umeshakubali kufanya au umekuwa unakifanya, bali fanya kitu kwa kutathmini kama ni muhimu na sahihi kwako kufanya. Usiogope kuvunja msimamo wako pale mambo yanapokwenda tofauti na ulivyotegemea.

 1. Hofu ya kupoteza.

Huwa hatupendi kupoteza kitu ambacho tayari tunacho, hata kama hakina manufaa kwetu. Huwa tunapenda kubaki na kila tulichonacho. Hali hii ndiyo inafanya mabadiliko kuwa magumu kwa wengi, kwa sababu hatupendi kuacha kile tulichozoea. Kwa njia hii wengi sana wamepata hasara kwenye biashara na hata uwekezaji.

Hatua ya kuchukua; jua vitu vingi unavyong’ang’ana kuwa navyo ni kwa sababu za kihisia tu na siyo kwa sababu vina umuhimu wowote kwako. Hivyo using’ang’ane kubaki na kitu kwa sababu tu umeshazoea, kuwa tayari kuachana na vitu ambavyo havina tena umuhimu au faida kwako.

 1. Kuacha hali kama ilivyo.

Mabadiliko yoyote kwenye maisha yanatutaka tubadili yale tuliyozoea, ambayo inakuwa ni kazi kwetu, kitu ambacho wengi hawapo tayari kufanya. Hivyo kinachotokea ni wengi kuamua kuacha hali kama ilivyo. Tunapenda kufanya na kuishi maisha yetu kama ambavyo tumezoea kuishi kwa kuwa tunaweza kutabiri matokeo tutakayopata. Hatupendi kufanya mambo mapya kwa sababu hatuna uhakika wa matokeo yake. Hii ndiyo sababu inayopelekea wengi kubaki kwenye ajira zile zile na hata kutumia vitu vya aina ile ile hata kama ni rahisi kubadili.

Hatua ya kuchukua; tambua kwamba kuacha hali kama ilivyo kunaweza kukugharimu sana kuliko kubadilika. Hivyo kuwa tayari kubadilika wakati wote na usiwe na hofu kwamba ukibadilika mambo yatakuwa magumu. Jua nini unataka na jua njia bora ya kupata unachotaka, na kuwa bora zaidi kila siku. Achana na mazoea.

 1. Kukosa uvumilivu.

Huwa tunaweka uzito sasa kuliko baadaye, tunapenda kupata raha sasa kuliko furaha ya baadaye. Kwa njia hii tumekuwa tunafanya maamuzi ambayo yanatunufaisha sasa, lakini baadaye yanakuwa na madhara kwetu. Huwa hatupo tayari kuumia sasa ili tunufaike zaidi baadaye. Mfano ni mtu unaponunua kitu ambacho hukimudu, kwa mkopo, ambao utaulipa kwa gharama kubwa siku zijazo.

Hatua ya kuchukua; katika kila maamuzi unayoyafanya, angalia muda mfupi na muda mrefu. Kama maamuzi yanakupa manufaa kwa muda mfupi, lakini madhara kwa muda mrefu usifanye. Ni bora maamuzi yanayokupa maumivu ya muda mfupi lakini manufaa ya muda mrefu.

 1. Wivu na husuda.

Huwa tunasukumwa na wivu na husuda katika kufanya maamuzi, huwa tunawaangalia wengine na kutamani kuwa kama wao au kupata kile walichonacho. Kwa kusukumwa na wivu, wengi wameishia kufanya mambo ambayo hayana umuhimu kwao, na hata wengine kuleta madhara kwa watu kwa kuwa tu wanawaonea wivu. Huwa hatuwezi kutulia pale tunapoona wengine wanafanikiwa kuliko sisi, hivyo tumekuwa tunakimbilia kuchukua hatua zisizo sahihi na kupoteza.

Hatua ua kuchukua; furahia maisha yako bila ya kujilinganisha na wengine. Weka malengo yako na yafanyie kazi, unapoyatimiza furahia na piga hatua zaidi. Waache wengine wafanya yao, na kushinda au kushindwa kwao hakuna uhusiano wowote na kushinda au kushindwa kwako.

 1. Kulinganisha kwa utofauti.

Mara nyingi huwa tunafanya maamuzi kwa kulinganisha kitu kimoja na kingine, na hii imekuwa inatugharimu sana. Mfano ukienda dukani kununua tai pekee na ukaambiwa tai ni elfu 50 utaona ni ghali sana. Lakini ukienda kununua suti ya laki tano, tai ya elfu 50 itaonekana ni bei ya ndogo, hii ni kwa sababu baada ya kutoa laki tano, elfu 50 inaonekana ni ndogo.

Hatua ya kuchukua; fanya maamuzi kwa kuangalia thamani ya kitu na siyo kwa kulinganisha na kitu kingine.

 1. Kutia nanga.

Huwa tunatumia taarifa ya mwanzo kama msingi wetu wa kufanya maamuzi. Mfano kama mtu anataka kukuuzia kitu cha shilingi elfu 10 kwa bei ya juu, anaanza kukuambia bei ni elfu 20. Hapo utaomba punguzo na akikuambia ulipie elfu 15, utaona ni nafuu kuliko elfu 20.

Hatua ya kuchukua; fanya maamuzi kwa kufikiria kitu kwa uhalisia wake na siyo kwa kutumia taarifa ulizopewa awali. Fikiria kama ungekuwa hujui chochote kwenye kitu hicho, ungefanya maamuzi gani?

 1. Ushahidi na ukaribu.

Huwa tunaamini sana maelezo na hadithi ambazo zimeelezewa kwa namna ambayo zinaibua hisia zetu. Kadiri maelezo yanavyokuwa ya kihisia na yanavyoelezwa mara nyingi, ndivyo tunavyoyaamini kama ukweli. Vyombo vya habari vimechochea sana hili, kwa kuweka kipaumbele kwenye habari hasi kuliko chanya.

Hatua ya kuchukua; jifunze kutofautisha ukweli na uongo, kwa kila hadithi au maelezo unayopewa, epuka kuweka hisia zako na fikiri kwa kina kupata ukweli wake.

 1. Upofu wa kuchagua.

Ni kawaida kwetu kuona kile ambacho tunakijua na kutokuona kile ambacho hatukijui au kukizingatia. Huu ni upofu wa kuchagua, tunapokuwa tunaweka mipango mbalimbali, tunakazana zaidi na yale maeneo tunayoyataka na kuachana na yale tusiyoyataka, hali hii hupelekea kushindwa kutimiza mipango hiyo.

Huwa tunaangalia kile tunachotaka na kuachana na tusichotaka. Mfano huwa tunaangalia mtu mmoja aliyefanikiwa, na kusahau kwamba kuna wengine wengi ambao wameshindwa, hatuwaangalii hao.

Hatua ya kuchukua; epuka upofu wa kuchagua kwa kuangalia upande wa pili wa kitu, kupata taarifa mbadala na kuangalia upande chanya na upande hasi wa kitu.

 1. Kulipa fidia.

Tuna tabia ya kuwalipa watu kile ambacho wametufanyia, iwe ni kizuri au kibaya. Mtu anapotupa kitu fulani, inakuwa kama deni kwako kwamba na wewe inabidi umpe kitu. Wengi wamekuwa wanatumia njia hii kuwanyonya wengine, mtu anakupa kitu kidogo kama zawadi, halafu baadaye anakuwa kwako na ombi kubwa. Kwa kuwa ulishapokea zawadi, unaona ni wajibu wako kumpa kile anachokuomba.

Hatua ya kuchukua; epuka kupokea vitu kama kuna hitaji limejificha nyuma yake. Pia unapowapa watu vitu, angalia usiwajengee deni kwako ambalo litawafanya wajisikie vibaya kama hawawezi kukulipa kwa kukupa kitu pia.

 1. Kukubalika na jamii.

Huwa tunapenda kukubalika na wale wanaotuzunguka, hivyo tunalazimika kufanya kile ambacho watu hao wanakikubali ili watukubali pia. Hivyo tabia zetu na mtindo wetu wa maisha, unaamuliwa zaidi na kipi kinakubalika kwenye jamii na kipi hakikubaliki. Tunaishi siyo kwa mipango yetu, bali kwa kuangalia kipi kitatufanya tukubalike.

Hatua za kuchukua; elewa kwamba kila mtu anafanya kitu ili kukubalika na jamii, mwonekano wa nje unaweza kumwamini mtu kwamba anafanya kitu kwa moyo, kumbe kwa ndani ni mtu tofauti kabisa. Pia njia hii ya kukubalika na jamii ni nzuri katika kujenga tabia nzuri kwenye jamii, kwa kuwaadhibu wale ambao wanakwenda kinyume na taratibu.

 1. Kinga ya kijamii.

Huwa tunafanya kitu kwa sababu kila mtu anafanya. Hata kama siyo kitu sahihi, kama kila mtu anafanya, basi tunakuwa na kinga ya kijamii. Upo usemi kifo cha wengi harusi, tunajisikia amani ndani ya kundi hata kama tunakosea. Wanasema kushindwa ndani ya kundi haiumizi kama kushindwa peke yako.

Kinga hii ya kijamii imekuwa inatumika sana na wafanyabiashara kwenye matangazo, wanakuambia kila mtu anatumia kitu hiki, hivyo unaposikia kila mtu anatumia, unapata uhakika kwamba hata kama utakosea, hukosei peke yako.

Hatua ya kuchukua; acha kufuata kundi na fanya maamuzi kwa kutumia akili yako mwenyewe. Kitu hakiwi sahihi kwa sababu kila mtu anafanya, na mara nyingi kinachofanywa na wengi huwa siyo sahihi. Usiogope kuwa tofauti na wengine, simamia ukweli na fanya kilicho sahihi, bila ya kujali wengine wanafanya nini.

Tuna tabia ya kutii mamlaka na kufanya kile ambacho mamlaka zinasema ufanye, hata kama siyo sahihi. Mamlaka hizi ni kuanzia ambazo ni ndogo mpaka kubwa. Mfano wazazi ni mamlaka kwa watoto, madaktari, walimu, viongozi wa kidini ni mamlaka kwa wengi.

Wengi wanapokuwa hawana uhakika wa nini wafanye, huwa wanatii mamlaka na kufanya kile ambacho mamlaka inasema wafanye, hata kama siyo sahihi. Pia tumekuwa tunawaamini sana wale ambao wanatuambia ni wataalamu waliobobea kwenye eneo fulani, na tunachukua maneno yao kama ukweli usiohitaji kuhojiwa.

Hatua ya kuchukua; tenganisha mamlaka na kile kinachosemwa au kushauriwa, kihoji chenyewe bila ya kukiweka kwenye mamlaka husika ili uweze kuona kama ni kweli au siyo kweli, sahihi au siyo sahihi. Mara nyingi wenye mamlaka wamekuwa wanakosea, pia watu hao huwa wanakuwa na maslahi yao binafsi, hivyo fikiri kabla ya kuamua.

 1. Kupata sababu.

Huwa tunapenda kupata sababu ya kila kitu kinachotokea, hatuwezi kutulia kama hatujapata sababu. Na hata kama hakuna sababu ya kitu kutokea, basi huwa tunatengeneza sababu zetu wenyewe, ili tu tuwe na uhakika wa nini kimesababisha.

Na kwa mambo yaliyotokea nyuma ni rahisi kukusanya sababu zilizopelekea yatokee kuliko kutengeneza sababu ya vitu vitakavyotokea. Sababu nyingi tunazojipa za mambo kutokea siyo sahihi. Tumekuwa tunahusianisha vitu visivyokuwa na uhusiano kwa sababu tu vimetokea kwa pamoja.

Hatua ya kuchukua; acha kujipa sababu zako mwenyewe kwenye vitu vinavyotokea, badala yake angalia uhalisia wake. Usione vitu kama unavyotaka kuviona wewe, bali ona vitu kama vilivyo.

 1. Kuheshimu sababu.

Uhitaji wetu wa kupata sababu ya kila kitu, umepelekea sisi kuamini sababu ambazo siyo sahihi. Mtu anaweza kuwa anataka umpe kitu, ambacho kwa hali ya kawaida usingempa, lakini anapokupa sababu kwa nini anataka umpe, wewe unampa. Siyo kwa kuwa amekupa sababu sahihi, ila tu kwa kuwa ana sababu. Tuna tabia ya kuheshimu sababu hata kama siyo sahihi, na hii imekuwa inatumika na wengine kupata vitu kutoka kwetu.

Hatua ya kuchukua; usikubaliane na kila sababu ambayo watu wanakupa, badala yake angalia uhusiano huo na kile ambacho watu wanataka. Mara nyingi utagundua hakuna uhusiano kabisa. Pia unapotaka watu wafanye kitu, wape sababu.

 1. Amini kwanza, shuku baadaye.

Hili ni kosa ambalo tumekuwa tunafanya kwenye maamuzi yetu mengi, tunaamini kwanza, au kukubaliana na kitu kwanza, kisha baadaye tunajipa sababu kwa nini tumefanya maamuzi sahihi. Mfano mtu ananunua kitu bila ya kufikiri kwa kina, halafu baadaye anaanza kujipa sababu kwa nini kitu alichonunua ni sahihi.

Hili pia lipo kwenye mambo mengine ya kijamii, kama dini, siasa na hata jumuiya mbalimbali, tunakubaliana na upande fulani kwanza, halafu tunaanza kujipa sababu kwa nini upande tuliochagua ni sahihi.

Hatua ya kuchukua; unapotaka kufanya maamuzi muhimu kwenye maisha yako, fikiri kwanza kabla hujafikia maamuzi. Na ukijikuta umeshafanya maamuzi kabla ya kufikiri, jua chochote unachojiambia cha kuhalalisha maamuzi hayo ni kujifurahisha tu.

 1. Ukomo wa kumbukumbu.

Huwa tunaamini sana kwenye kumbukumbu zetu, lakini huwa zinatuangusha. Kumbukumbu zetu siyo nzuri kama tunavyofikiri, kadiri muda unavyokwenda tunasahau kitu kilichotokea. Na hata tunachokuwa tunakumbuka, kinakuwa ni vipande tu vya tukio zima. Vitu ambavyo vimegusa hisia zetu tunavikumbuka kwa muda mrefu kuliko ambavyo havijagusa hisia. Pia vitu ambavyo vina mifano na hadithi tunakumbuka kwa muda mrefu.

Hatua ya kuchukua; usiamini sana kumbukumbu zako, kama kuna kitu ambacho hutaki kukisahau kiweke kwenye maandishi wakati ambapo kimetokea.

 1. Msukumo wa kufanya chochote.

Kazi kubwa kwa mtu ni kukaa eneo moja bila ya kufanya chochote. Huwa hatupendi kukaa bila ya kufanya kitu, hivyo huwa tunapata msukumo wa kufanya chochote. Hali hii imewapelekea wengi kufanya mambo ambayo siyo sahihi na yanayowagharimu, kwa sababu tu hawawezi kukaa bila ya kufanya kitu.

Pia kwa kufanya kitu, tunaamini tunaonekana ni wachapa kazi, hata kama hakuna chochote cha msingi tunafanya.

Hatua ya kuchukua; kabla hujakazana kuchukua hatua, jiulize ni kitu gani unataka kukamilisha na ipi njia sahihi ya kukikamilisha. Usifanye tu ili kuonekana kuna kitu unafanya, fanya kufikia kile unachotaka. Na kama hakuna cha kufanya, ni bora ukae utulie, kuliko kutafuta chochote cha kufanya.

 1. Msukumo wa kusema chochote.

Huwa hatuwezi kukaa kimya, hasa pale ambapo hatuna cha kuongea. Huwa tunaongea ili tu kuonekana na sisi tupo, au tuna haki ya kuongea pia. Msukumo huu wa kuongea chochote umewapelekea watu kuonekana wajinga na wapumbavu na hata kuvuruga mipango mizuri ambayo ilikuwepo.

Hatua ya kuchukua; Plato anasema, mwerevu huongea kwa sababu ana kitu cha kusema, mjinga huongea kwa sababu inabidi aseme kitu. Benjamin Franklin anasema, kama unataka kuishi kwa amani na utulivu, usiseme kila unachojua na usihukumu kila unachoona.

Hisia huwa zina msukumo mkubwa kwetu, tunapokuwa na hisia kali, huwa tunasukumwa kufanya maamuzi na kuchukua hatua. Lakini maamuzi yote unayoyafanya ukiwa na hisia huwa ni maamuzi mabovu, kwa sababu hisia zinapokuwa juu fikra zinakuwa chini. Huwezi kufikiri kwa usahihi unapokuwa umetawaliwa na hisia.

Hatua za kuchukua; unapokuwa kwenye hisia kali, jizuie kufanya maamuzi yoyote. Pia kwenye kila maamuzi unayotaka kufanya, jipe kwanza muda, mfano kama kuna kitu unataka kununua, usikinunue pale pale ambapo umepata wazo la kukinunua, bali jipe muda. Kwa kufanya hici utaepuka kufanya maamuzi kwa hisia.

Pale tunapojiona hatuna udhibiti kwenye maisha yetu, huwa tunapata msongo. Na tunapokuwa na msongo huwa tunafanya maamuzi ambayo siyo sahihi. Unapojikuta njia panda na hujui njia ipi ya kuchukua, unapata msongo, na unapokuwa na msongo, huwezi tena kufikiri njia sahihi, badala yake utaamua kuchukua njia yoyote, au kutokuchukua hatua kabisa.

Hatua ya kuchukua; Epictetus anasema, maisha ya furaha ni pale unapojua kilicho ndani ya uwezo wako na kilicho nje ya uwezo wako. Ukifuata kauli hiyo hutapata msongo kabisa. Kwa chochote kinachotokea, jiulize je kipo ndani ya uwezo wako, kama ndiyo basi chukua hatua na hakuna msongo. Kama jibu ni hapana, hakipo ndani ya uwezo wako basi unapaswa kukikubali kama kilivyo na kuendelea na mengine, msongo hautasaidia.

 1. Maumivu, kemikali na ugonjwa.

Hakuna wakati mbovu kwako kufanya maamuzi kama unapokuwa kwenye maumivu, unapokuwa na kemikali kama ulevi kwenye mwili wako au unapokuwa unaumwa. Unapokuwa kwenye hali hizo huwezi kufikiri kwa usahihi na unaweza kukubaliana na chochote hata kama baadaye kina madhara kwako.

Hatua ya kuchukua; epuka kufanya maamuzi makubwa ya maisha yako ukiwa katika maumivu, ulevi au ugonjwa.

 1. Makosa mengi kwa pamoja.

Hapa tumeona kosa moja moja tunalofanya kwenye maamuzi, lakini mara nyingi makosa haya hayatokei yenyewe, badala yake huwa yanaandamana pamoja. Na kadiri makosa mengi yanapokuwa pamoja, ndivyo tunavyoishia kufanya maamuzi mabovu kwenye maisha yetu.

Mfano kwenye wizi, mtu anaweza kuiba kitu kwa mara ya kwanza, kama hataadhibiwa basi ataendelea kuiba tena na kwa kuwa alishaanza kuiba basi anaendelea na wizi na wengine wanapoona mwenzao anaiba, wanaona ni sahihi na hivyo wanaiba pia. Hii inapelekea wale wanaoiba kuonekana wapo sahihi na wasioiba kuonekana hawapo sahihi.

Hatua ya kuchukua; kwenye kila maamuzi na hatua tunazochukua, tuchunguze kwa kina msukumo wa sisi kufikia maamuzi hayo na kuchukua hatua ambazo tumechukua. Tunapogundua kwamba makosa mengi ya kisaikolojia yamehusika, tunapaswa kufanyia kazi kosa moja moja ili baadaye tuweze kufanya maamuzi bora zaidi.

Rafiki, hayo ndiyo makosa 28 ya kisaikolojia ambayo yamekuwa yanakusababisha ufanye maamuzi mabovu. Kwa kila maamuzi unayochukua kwenye maisha yako, jitafakari katika makosa haya ili usifanye maamuzi mabovu.

Kwenye makala ya tano za juma hili la 14 utajifunza mengi zaidi kutoka kwenye kitabu cha SEEKING WISDOM ambayo yatakuwezesha kufanya maamuzi ya busara na kuepuka makosa ya wazi ambayo umekuwa unayafanya kila siku. Ili kupata uchambuzi wa kina pamoja na kitabu, hakikisha unajiunga na CHANNEL YA TANO ZA JUMA ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM. Kuunganishwa tuma ujumbe kwa kutumia TELEGRAM MESSENGER kwenda namba 0717396253 ujumbe uwe na maneno TANO ZA JUMA na utaunganisha. Huko kila juma utapata chambuzi za kina za vitabu na vitabu vyenyewe. Karibu sana.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge