Mpendwa rafiki yangu,

Aliyekuwa baba wa taifa wa Africa ya kusini Nelson Mandela enzi za uhai wake aliwahi kusema, kutokusamehe ni kama kunywa sumu ya panya wewe mwenyewe na huku ukisubiria panya afe.

Mahusiano yetu yanapokosa msamaha yanakuwa yamepoteza mwelekeo. Tunakuwa kama tumekunywa sumu ya panya huku tukisubiria panya afe. Mahusiano yetu yanahitaji usawa kila mmoja anatakiwa kuwajibika na siyo swala la mtu mmoja kuwajibika.

Mahusiano yaliyopoteza mwelekeo ni yale ambayo wahusika hawataki kusameheana. Tunaruhusu msamaha upite katika mahusiano yetu tunakuwa tunapata dawa ya uponyaji lakini pale tunapokataa kusamehe tunakuwa tunaingiza sumu ndani yetu.

Mahusiano hayawezi kuwa na afya kama wahusika hawana desturi ya kusameheana. Hakuna mahusiano ambayo yako salama asilimia mia moja. Na hakuna mahusiano ambayo hayana changamoto, nina uhakika kuwa kila mahusiano ambayo unayo kupishana kauli ni jambo la kawaida. Wako ambao watakwenda kinyume na sisi ,wako ambao watatukwaza na kututendea vile ambavyo sisi hatupendi.

Msamaha ni kiboko ya kusafisha mahusiano yetu, kama unataka kurudisha mahusiano yako na mhusika wako. Jishushe na kuwa mnyenyekevu nenda kamuombe msamaha hata kama yeye ndiye aliyekukwaza. Ukisubiri yeye aliyekuumiza ndiyo aje kukuomba msamaha hakika mtapoteza mahusiano yetu.

Mahusiano ya kulipizana visasi yaani jino kwa jino yalishapita zamani, hatuwezi kujenga mahusiano bora kama tunataka kuwakomesha wale watesi wetu. Tunapotaka kulipiza kisasi, tunakuwa tunaamua kwa makusudi kuvunja mahusiano yetu kwa lazima.

SOMA; Jinsi Ya Kushinda Katika Ugomvi Wowote Ule

Chuki ni mbaya katika mahusiano yoyote yale. Ukibeba chuki itakuja kuzaa mauti. Kwa mfano,mtu ambaye uko naye katika mahusiano, ukasema amekukosea heshima hivyo ngoja nichukue hatua ya kumpeleka polisi ili nimfundishe adabu. Utaweza kumpelekea polisi kweli, lakini yule mtu atakapotoka kule atakuwa na kinyongo cha kulipa kisasi, hataweza kukubali kukuachia, atatafuta mbinu yoyote ili alipize kisasi. Unapotaka kumwajibisha mwenzako siyo njia sahihi ya kurudisha mahusiani bali ni njia ya kuvunja mahusiano.

Mahusiano yetu yanajengwa kwa upendo. Unaweza kutumia nguvu kweli ya kupambana na mahusiano yako lakini ni ngumu kujenga mahusiano yetu kwa njia ya mabavu.

Aliyekuwa mtawala wa ufaransa na jemedari wa kijeshi Napolean Bonaparte aliwahi kusema, nimewavuta watu wangu kwa mabavu lakini Yesu amewavuta kwa upendo. Kumbe basi, mahusiano yetu hayajengwi kwa mabavu kama alivyokuwa anafanya mtawala wa ufarasa yeye mwenyewe anakiri upendo ndiyo unajenga mahusiano yetu.

Hatua ya kuchukua leo; ukitaka mahusiano yako yapendeze,ruhusu msamaha uwe sehemu ya maisha yenu. Pale mambo yanapokwenda ndivyo sivyo mwalike rafiki yako msamaha.

Hivyo basi, mahusiano mazuri ni yale ambayo wahusika wanayafurahia. Huwezi kuyafurahia mahusiano kama hayana upendo, amani. Jitahidi kujenga faraja kwenye mahusiano yako kila siku na msameheane pale mnapokosana

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana