Mpendwa rafiki yangu,

Kama unaendelea kuvuta pumzi basi huwezi kujitenga na msamaha katika mahusiano yako mbalimbali. Mahusiano yetu bila msamaha yanakuwa ni magumu kweli. Mara nyingi tunakwazana na kujeruhiana kwa mambo mbalimbali lakini kupitia msamaha unarudisha mahusiano yetu.

Kama isingekuwa msamaha basi mahusiano mengi yangekuwa  yameshavunjika. Kwa sababu watu wengi  wanaishi kwa kuvumiliana kwenye mahusiano mengi sasa isingekuwa hakuna msamaha hali ya mahusiano ingekuwa ni mbaya.

Watu wengi wanasema wanasamehe au wamesamehe lakini wengi hawafanyi hivyo. Wengi wanasamehe kwa kutumia msamaha usiyo na fadhila za kimungu. Watu wanasamehe kwa msamaha wa uwongo na msamaha wa uwongo ni msamaha unaongozwa na hisia za kibinadamu hauna fadhila.

Watu wanasamehe kwa mdomo tu fulani nimekusamehe lakini bado anaendelea kubaki na uchungu ulioumbika ndani ya moyo. Hatusamehi kutoka ndani ndiyo maana mateso yanaendelea kuwa makubwa, tunasamehe kwa kutumia msamaha wa uwongo usio kuwa na fadhila.

KWA NINI SIYO TAJIRI

Tunaposamehe kwa msamaha wa uwongo tunakuwa tunabaki na uchungu uliombika ndani ya moyo, kama ni majeraha tunaendelea kubaki nayo ndani. Vinyongo, wivu na chuki vinaendelea kututafuna sisi wenyewe pale tunaposamehe kwa uwongo. Unapomsamehe mtu basi itoke ndani ya moyo ndiyo utaweza kupata uponyaji wa kweli lakini kama unasamehe ili uonekane na watu bado hasara inakuwa ni kwako kwa sababu bado utaendelea kubaki na maumivu.

Lengo la msamaha ni kuondoa sumu ndani ya mwili sasa unaposamehe kwa uwongo maana yake unaendelea kung’ang’ania ile sumu  ibaki ndani yako.  Hii inakuwa haina tofauti na yule mtu anayekuwa sumu ya panya huku akisubiria adui yake afe. Samehe kwa faida yako mwenyewe na wale siyo ya mtu mwingine.

SOMA; Haya Ndiyo Mahusiano Yaliyopoteza Mwelekeo

Msamaha wa kweli una unyenyekevu lakini wa uwongo hauna unyenyekevu na kitu chochote kikikosa unyenyekevu kimekosa fadhila. Fadhila ni mazoea ya mtu kutenda mema, sasa kama umekosa fadhila utawezaje kusamehe kwa moyo?

Msamaha wa uwongo ni aina ya msamaha uliokosa fadhila, ni msamaha wa masharti. Pale tunapokuwa tumekosewa na wengine tunawapa masharti, kwa mfano, nilikuambie, kosa kama hili siwezi kukusamehe hata Mungu anaona, umerudia tena ehh! na maneno mengine yanayofanana na hayo.

Msamaha wa uwongo unapima makosa katika mizani, hili naweza kukusamehe na hili siwezi kukusamehe. Tunakuwa tunawasamehe watu kwa masharti, kwa vipimo na kuanza kuchambua makosa yalikuwaje.  Tunapoamua kusamehe basi tusamehe msamaha wa kweli ili sisi sote tupate uponyaji wa ndani. Uponyaji wa ndani ndiyo kinga ya kila mtu anayehitaji kuponya majeraha yake ya ndani. Tunapokataa kusamehe tunakuwa tumejinyima haki ya upendo sisi wenyewe.

Hatua ya kuchukua leo; wasamehe wale waliokukosea kwa msamaha wa ukweli. Msamaha wa kweli ni msamaha unaongozwa na nguvu za kimungu. Ni msamaha ambao hauna masharti yoyote, unamsamehe mtu kweli kutoka ndani ya moyo. Unayamaliza hapo hapo bila kuweka tena kinyongo.

Kwahiyo, kuwa mmoja wa watu wanaotumia msamaha wenye fadhila, unaposamehe kutoka moyoni unawafundisha hata wale watu wanaosamehe kiunafiki. Msamaha wa kweli ni mgumu kwa sababu muda mwingine unaweza kuonekana hata mpumbavu mbele ya watu pale unapomsamehe mtu na watu wakasema kosa kama lile ingekuwa mimi nisingemsamehe. Jifunze kusamehe na wewe utasamehewa.

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu kama vile KWANINI MSAMAHA,FUNGA NDOA NA UTAJIRI, ONGEA LUGHA YAKO, MABADILIKO 250 YA USHINDI na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana