Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu kinachoitwa Poor Charlie’s Almanack; The Wit and Wisdom of Charles T. Munger kilichohaririwa na Peter D. Kaufman ambaye amekusanya pamoja hekima za Charles T. Munger.

Hiki ni kitabu kinachotupa msingi sahihi wa kufanya maamuzi kwenye maisha yetu, ili tuweze kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa.

Poor Charlie's Almanack cover.jpg

Kupitia kitabu hiki, Charlie anatupa akili, hekima na maadili ambayo amekuwa anayatumia kwenye maisha yake na yakampa mafanikio makubwa. Hekima hii ameipata kupitia kujifunza kwa watu mbalimbali na kada mbalimbali za kitaaluma.

Nukuu, mafunzo na hotuba tunazokwenda kujifunza kwenye kitabu hiki, zinatokana na mfumo wa maisha ya Charlie ambao unaendeshwa na misingi ifuatayo;

  1. Kujifunza maisha yote.
  2. Udadisi.
  3. Uzani.
  4. Kuepuka wivu na chuki.
  5. Kuwa mtu unayeweza kutegemewa.
  6. Kujifunza kutokana na makosa ya wengine.
  7. Uvumilivu na ung’ang’anizi.
  8. Kufikiri kwa akili yako.
  9. Kuwa tayari kujaribu imani yako mwenyewe.
  10. Kugeuza kitu ili kukielewa vizuri.
  11. Kutumia mfumo wa akili wa kufanya maamuzi unaohusisha taaluma mbalimbali.

Hii ni baadhi ya misingi ya Munger, lakini ipo mingi zaidi.

Charlie amekuwa akitumia hadithi na vichekesho ili kufikisha ujumbe wake, kitu ambacho kinawafanya watu wamwelewe zaidi.

Lengo kuu la Charlie kwenye maisha ni kuwa huru, hivyo anatumia utajiri kama kitu cha kumpa uhuru na siyo kinyume chake. Amewahi kunukuliwa akisema; “niliamua kuwa tajiri ili niweze kuwa huru kama Lord John Maynard Keynes.”

SOMA; Tano Za Juma Kutoka Kitabu Seeking Wisdom, Jinsi Ya Kufikiri Kwa Usahihi Na Kuepuka Kufanya Maamuzi Mabovu Kwenye Maisha.

Vitu vitatu ambavyo Charlie anasisitiza sana.

Kupitia hotuba zake mbalimbali, kuna vitu ambavyo Charlie amekuwa anasisitiza sana. Vitatu kati ya hivyo ni;

  1. Kuhakikisha unakuwa na uelewa mpana kwa kujifunza maarifa ya msingi kwenye taaluma mbalimbali. Hili litakusaidia sana kwenye kufanya maamuzi. Kama shuleni au chuoni hukufundishwa basi jifunze mwenyewe, fursa za kufanya hivyo ni nyingi.
  2. Kufikiri kinyume, kwa kujua ni kitu gani hutaki kwenye maisha, kisha kujua ukifanya nini utapata usichotaka kisha kuepuka kufanya hicho. Charlie anatuambia jua sehemu ambayo ukienda utakufa kisha usiende sehemu hiyo.
  3. Epuka gharama na hatari kwenye uwekezaji kwa kuchagua kampuni chache zinazofanya vizuri kisha kuwekeza kwenye kampuni hizo na kutulia. Kazi yako inakuwa kusubiri gawio na ongezeko la thamani kwenye uwekezaji wako linakufanya uwe tajiri.

Taaluma Tatu Muhimu Kila Mtu Kujua.

Charlie anatushauri tupate elimu ya msingi kwenye taaluma mbalimbali, na siyo ile tu tuliyosomea. Taaluma hizi zipo nyingi kama tulivyojifunza, lakini kuna tatu muhimu sana ambazo kila mtu anapaswa kuzijua, kwa sababu zitamsaidia sana kufikiri kwa usahihi na kufanya maamuzi.

  1. Saikolojia, hii itakusaidia kujua jinsi watu wanavyofikiri na kufanya maamuzi. Kwa kuwa maisha yako yote utajihusisha na watu, basi unapaswa kujua saikolojia ya watu ikoje. Hapa Charlie anatusisitiza sana kujua mchango wa vitu kama zawadi na adhabu kwenye ufanisi, pia kujua athari za wivu na chuki. Maeneo hayo ndiyo yamekuwa yanaleta matatizo makubwa kwenye mahusiano ya watu.
  2. Uchumi, hasa ule wa chini (microeconomics), kama unafanya biashara ya aina yoyote ile au unafanya uwekezaji, basi elimu ya msingi ya uchumi ni muhimu. Elimu hii itakupa uelewa kuhusu hali ya uchumi, mambo kama mfumuko wa bei (inflation), uhitaji na upatikanaji (demand and supply) na dhana ya ukuaji kwenye biashara na uwekezaji (scalability). Kwa kuwa na elewa kwenye haya na mengine, kutakusaidia sana kufanya maamuzi sahihi ya kibiashara na uwekezaji.
  3. Uhasibu. Charlie anasema hii ndiyo lugha ya biashara. Usipojua misingi ya uhasibu, vitu kama kuandaa na kusoma taarifa za hesabu za fedha kwenye biashara, huwezi kufanya maamuzi sahihi kwenye biashara au uwekezaji. Kuna taarifa kuu tatu za kibiashara ambazo unapaswa kuzielewa na kuweza kuzisoma ili kufanya maamuzi kwenye biashara na uwekezaji, taarifa ya mapato na matumizi (income statement), taarifa ya mzunguko wa fedha (cashflow statement) na mizania (balance sheet). Hivi ni vitu unavyopaswa kuweza kuvisoma na kuvielewa ili kufanya maamuzi sahihi.

Ukiweza kuwa na elimu ya msingi kwenye taaluma hizi tatu, zitakuwa na msaada sana kwako. Ukiweza ongeza sheria, fizikia, baiolojia, hisabati na nyingine.

SOMA; Makosa 28 Ya Kisaikolojia Unayofanya Na Yanayopelekea Wewe Kufanya Maamuzi Mabovu Yanayokugharimu.

Kanuni Ya Utajiri Isiyoshindwa.

Kwa kumalizia, tujikumbushe kanuni ya utajiri ambayo Charlie ametushirikisha, ambayo ukiifuata kwa uaminifu bila ya kuivunja, lazima ufike kwenye utajiri.

Kanuni hii ina vitu vitatu tu vya kufanya, baada ya kuvifanya hivyo kila siku, wewe jipe tu muda na utajiri ni wako.

Moja; matumizi yako yawe madogo kuliko kipato.

Mbili; kwenye kila kipato, weka akiba.

Tatu; akiba unayoiweka, iwekeze kwenye mfumo ambao haukupi gharama kubwa au kutozwa gharama kubwa. (Kwa hapa Tanzania mfumo mzuri ni UTT)

Na kama Charlie anavyotuhakikishia; ukifanya hivi kwa muda mrefu, lazima uwe tajiri, huhitaji akili nyingi kufanya hivyo.

Rafiki, kupata uchambuzi kamili wa kitabu hiki na vingine vingi karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA. Kujiunga na channel hii, fungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.