#TANO ZA JUMA #14 2019; Kinachozalisha Maamuzi Mabovu, Jinsi Ya Kufikiri Kwa Kina Na Kuepuka Maamuzi Mabovu, Makosa 28 Ya Kisaikolojia Yanayopelekea Kufanya Maamuzi Mabovu, Mpumbavu Hutengana Na Fedha Zake Na Kanuni Kuu Ya Kupata Unachotaka.
Rafiki yangu mpendwa,
Karibu kwenye tano za juma la 14 la mwaka huu 2019, ambapo kwenye tano hizi tunakwenda kujifunza jinsi ya kufikiri kwa kina na usahihi na kuepuka kufanya maamuzi mabovu.
Sehemu kubwa ya maamuzi unayofanya kila siku ya maisha yako hufikiri, unafanya kwa mazoea, kwa tamaa au kwa sababu kila mtu anafanya hivyo. Na hilo ndiyo limekuwa linakuingiza kwenye matatizo mengi unayopitia kwenye maisha yako.
Juma hili la 14 tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kitabu kinachoitwa SEEKING WISDOM; From Darwin to Munger kilichoandikwa na Peter Bevelin. Mwandishi amefanya kazi kubwa ya kukusanya hekima za watu mbalimbali walioweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yao na kwenda kinyume na mazoea. Kuanzia mwanabaiolojia Charles Darwin ambaye alileta mapinduzi makubwa kwenye baiolojia kwa kufikiri tofauti, mpaka kwa mwanafalsafa mwekezaji Charles Munger ambaye pamoja na mshirika wake Warren Buffett wameweza kupata mafanikio makubwa sana kwenye uwekezaji, kuliko wawekezaji wengine wote.
Msingi mkuu wa kitabu hiki ni kufanya maamuzi kwa kufikiri kwa kina na kuondokana na mazoea, hisia au kufuata kile ambacho wengine wanafanya.
Karibu sana tujifunze kwa kina jinsi tunavyoweza kuwa na hekima ya kufanya maamuzi bora kwenye maisha yetu.
#1 NENO LA JUMA; KINACHOZALISHA MAAMUZI MABOVU.
Kila mmoja wetu kuna maamuzi mabovu amewahi kufanya kwenye maisha yake. Ukikaa chini na kuyatafakari maamuzi yote mabovu umewahi kufanya, utaona kuna kitu kimoja kipo nyuma ya maamuzi yote hayo.
Kwanza maamuzi yote mabovu unakuta umeyafanya kwa haraka, yaani kitu kimetokea na wewe kwa haraka ukafanya maamuzi. Pia ukiangalia unagundua wakati unafanya maamuzi hayo ulikuwa na furaha sana au hasira sana. Na kingine ambacho utakiona kwenye maamuzi mengi mabovu uliyofanya ni ulifanya kwa sababu kila mtu ndivyo anavyofanya.
Mambo yote hayo yanayopelekea ufanye maamuzi mabovu yanakuzuia wewe kufanya kitu kimoja muhimu sana, ambacho ni KUFIKIRI KWA KINA. Unapofanya maamuzi kwa haraka, au ukiwa na hisia kali au kwa kuangalia wengine, hujipi nafasi ya wewe kufikiri kwa kina, na hilo ndiyo linalopelekea wewe kufanya maamuzi mabovu.
Hivyo chanzo kikuu cha maamuzi mabovu ni KUTOKUFIKIRI KWA KINA. Na kama unataka kufanya maamuzi mabovu, kama unataka kuwa na busara na hekima, kama unataka kuondokana na hali za hatari kwenye hatua unazochukua kwenye maisha na kama unataka kuyaishi maisha yako, kwa furaha na ukamilifu, lazima UFIKIRI KWA KINA, na ufikiri kwa akili yako mwenyewe.
Ni jawabu rahisi, lakini gumu sana kwenye uhalisia. Watu wengi hawapendi kufikiri kwa akili zao, bali wanapenda kufanya yale yanayofanywa na wengine, ili hata wakishindwa basi wawe na kitu cha kusingizia. Wewe ondoka kwenye kundi hilo na anza kufikiri kwa kina. Utaweza kufanya maamuzi bora sana kwenye maisha yako na utaondokana na changamoto nyingi unazopitia sasa.
#2 KITABU CHA JUMA; JINSI YA KUFIKIRI KWA KINA NA KUEPUKA MAAMUZI MABOVU.
Ni nini tunataka kwenye maisha yetu? Kuwa na afya bora, kuwa na furaha kwetu na familia zetu, kazi zetu na kadhalika. Je ni kitu gani kinaingilia kupata kile tunachotaka kwenye maisha? Hisia za hofu, hasira, huzuni, chuki na hata msongo vimekuwa vikwazo kwetu kuwa na maisha ya furaha.
Mwandishi wa kitabu SEEKING WISDOM; From Darwin to Munger kilichoandikwa, Peter Bevelin ametupa majibu sahihi ya jinsi ya kuvuka vikwazo hivi vinavyotuzuia kuwa na maisha bora. Kupitia kitabu hiki, Peter ametuonesha makosa tunayofanya kwenye kufikiri na jinsi tunavyoweza kufikiri kwa usahihi.
Kitabu hiki kimeandikwa kwenye msingi wa kauli ya mwanafalsafa mwekezaji Charles Munger, ambaye anasema; “All i want to know is where i’m going to die so i will never go there”. Akiwa anamaanisha anachotaka kujua kwenye maisha ni wapi akienda atakufa, hivyo aepuke kwenda eneo hilo.
Kuna makosa ambayo tunayafanya kwenye maisha yetu, ambayo tukiyajua na kuyaacha tutapunguza changamoto kwenye maisha yetu. Kuna njia ambazo zinatupeleka kwenye maisha yasiyo na furaha, ambapo tukizijua na kuziepuka tutakuwa na maisha bora.
Karibu kwenye uchambuzi huu wa kitabu, tujifunze njia inayoelekea kwenye kifo na jinsi ya kuiepuka ili tuwe na maisha bora.
KWA NINI HEKIMA NI MUHIMU.
Ni muhimu sana kujifunza na kupata hekima kwa sababu ndiyo njia pekee unayoweza kuishi maisha bora kwako na kwa wengine. Upumbavu ni mzigo siyo tu kwa mpumbavu mwenyewe, bali hata kwa wale wanaomzunguka na jamii kwa ujumla.
Njia bora ya kujifunza hekima ni kupitia wengine. Itakuchukua muda na maumivu sana kama utataka kujifunza kila kitu kwa kufanya mwenyewe. Badala yake chukua njia ya mkato, kwa kujifunza kupitia wengine. Jifunze kupitia makosa ya wengine, angalia yale wengine wamekosea na wewe usifanye. Pia angalia yale wanayofanya vizuri na wewe uyafanye.
Kwa sababu tunajifunza hekima kupitia wengine, hitaji kubwa kwenye kupata hekima ni kujifunza. Kila kitu unachotaka kujua kimeshaandikwa na wengine, kazi ni kwako kukaa na kusoma, kujifunza na kutumia kwenye maisha yako. Kwa sababu kama utajifunza halafu usitumie, bado hujawa na hekima, unakuwa umepata maarifa pekee. Maarifa yanakuwa hekima pale unapoyatumia kwenye maisha yako.
VITU VITATU VINAVYOATHIRI KUFIKIRI KWETU.
Kama ambavyo tutaendelea kujifunza, makosa mengi tunayofanya kwenye maisha yanaanzia kwenye namna ambavyo tunafikiri. Mara zote ambapo tunakosea tunakuwa hatujafikiri kwa kina na kwa akili zetu. Badala yake tunafanya maamuzi kwa hisia au kwa mazoea.
Vipo vitu vitatu ambavyo vinaathiri kufikiri kwetu.
Kitu cha kwanza ni muundo wa mwili na ubongo, jinsi ubongo wetu ulivyo na ulivyokuzwa, kunaathiri sana kufikiri kwetu. Ubongo wetu binadamu unatofautiana na wanyama wengine kwa kuwa na sehemu kubwa kwenye ubongo wa mbele ambao unatumika kufikiri. Na baina ya binadamu ubongo unatofautiana pia, kwa mfano mtu ambaye amepata ajali inayohusisha kichwa, kama sehemu inayofikiri imehusika, anakuwa na tabia tofauti.
Kitu cha pili ni jeni zetu. Jeni (gene) ndiyo zinatupa utambulisho na utofauti wetu. Ndiyo zinazobeba tabia zetu zote ambazo tunazo. Ndiyo zinafanya uonekane ulivyo, kama ni mfupi au mrefu, mweusi au mweupe na kadhalika. Jeni hizi pia huwa zinadhibiti uzalishwaji wa kemikali mbalimbali mwilini ambazo zinaweza kuathiri kufikiri kwetu. Mfano wapo watu ambao ni rahisi kwao kukasirishwa kuliko wengine. Wapo ambao wanakuwa na hofu kuliko wengine. Tabia hizi nyingi huanzia kwenye jeni.
Kitu cha tatu ni mazingira. Mazingira yetu yanaathiri sana akili zetu na jinsi ambavyo tunafikiri. Mazingira yanaanzia kwenye ukuaji, ulaji, elimu, utamaduni, jamii inayotuzunguka na hata yale tunayopendelea kufanya. Mazingira yetu ndiyo yanayotengeneza uzoefu ambao tunakuwa nao na uzoefu huu unaathiri kufikiri kwetu.
Kwa kuweka vitu hivi pamoja, kuanzia jeni, muundo wa mwili na akili na mazingira yetu, tunapata tabia za watu ambazo zinatofautiana sana. Hakuna watu wawili duniani ambao wana tabia zinazofanana kabisa, hata mapacha wa kufanana, bado mazingira yanawatofautisha, hata kama wamekulia eneo moja.
JINSI MAGEUZI YALIVYOATHIRI KUFIKIRI KWETU.
Mageuzi (evolution) ambayo yametokea kwenye dunia na hata kwetu binadamu, yametutengeneza jinsi tulivyo sasa. Mwanabaiolojia Charles Darwin alitumia sehemu kubwa ya maisha yake kujifunza kuhusu mageuzi kwa viumbe hai. Na katika kuhitimisha yale aliyojifunza, alikuja na hitimisho kwamba kwa kila jamii kuna mashindano ya kuishi, na wale wenye nguvu ndiyo wanaoshinda.
Darwin anasema rasilimali ni chache na hivyo haziwatoshi viumbe wote, hivyo inatokea hali ya kupigania rasilimali chache, wale wenye nguvu wanashinda na hivyo kuendeleza kizazi chao. Darwin anaita hii SURVIVAL OF THE FITTEST, kwamba viumbe wanaoweza kupambana na wanaoweza kuyatawala mazingira ndiyo wanaopona. Wengine wanakufa.
Ukiangalia mageuzi yana malengo makubwa mawili, kupona na kuzaliana. Viumbe wote hapa duniani, wanapambana kwa vitu hivyo viwili, kwanza kupona, yaani usife kwa changamoto mbalimbali unazokumbana nazo. Na ukishajihakikishia kupona basi unazaliana ili kuendeleza kizazi chako.
Huu umekuwa ndiyo msingi wetu mkuu wa kufanya maamuzi. Maamuzi mengi tunayoyafanya, msukumo ni sisi wenyewe kupona na pia kuzaliana. Ndiyo maana ukiangalia tabia za watu mara nyingi utaona kama wana ubinafsi. Ubinafsi ndiyo uliwawezesha watangulizi wetu kupona na sisi kuzaliwa. Kadhalika ufanyaji wa mapenzi ni kipaumbele kikubwa kwa wengi, siyo kwa sababu tunafurahia kufanya mapenzi, kwa sababu pia ni msukumo wa sisi kuzaliana na kuendeleza kizazi chetu.
Ukiweka pamoja muundo wetu wa kibaiolojia, pamoja na mchango wa mageuzi, utaona jinsi ambavyo tumetengenezwa kufanya maamuzi ambayo yanahakikisha vitu viwili vinatokea, moja tunakuwa hai, yaani hatupi na mbili tunazaliana.
Lakini maisha tunayoishi sasa, ni tofauti sana na maisha yalivyokuwa miaka 5000 iliyopita, lakini bado tunafikiri kama watu walioishi miaka hiyo. Tunahitaji kubadili namna tunavyofikiri kama tunataka kuwa na maisha bora na hilo ndiyo tunajifunza kwenye kitabu hiki.
Tumekuwa tunaingia kwenye matatizo mbalimbali kwa sababu ya kufikiri kizamani. Kufikiri kwa ubinafsi, tamaa ya mapenzi, wivu, hofu na kuiga kile ambacho wengine wanafanya. Unahitaji kufanya mabadiliko kwenye mfumo wako wa kufikiri, ufikiri kwa umakini bila ya kuathiriwa na hisia zozote au mtu yeyote.
MAKOSA 28 YA KISAIKOLOJIA YANAYOPELEKEA KUFANYA MAAMUZI MABOVU.
Kwenye makala ya juma hapo chini nimekushirikisha makosa 28 ya kisaikolojia ambayo umekuwa unayafanya na yanakuingiza kwenye maamuzi mabovu. Pia nimekushirikisha hatua za kuchukua kwenye kila kosa ili usiingie kwenye maamuzi mabovu.
FIZIKIA NA HESABU YA KUFANYA MAAMUZI MABOVU.
Kama ambavyo tumeona, yapo makosa ya kisaikolojia ambayo tumekuwa tunayafanya na tunaingia kwenye maamuzi mabovu. Lakini pia tunapofanya maamuzi, huwa hatutegemei fikra zetu pekee, kuna mifumo ya kifizikia na kihesabu ambayo tumekuwa tunaitumia na inapelekea kufanya maamuzi mabovu.
Hapa kuna mambo tisa ya kifizikia na kihesabu ya kutusaidia kuepuka kufanya maamuzi mabovu.
MOJA; KUFIKIRI KIMFUMO.
Badala ya kuangalia kitu kwa upekee wape, tunapaswa kuangalia mfumo mzima unaohusika na kitu husika. Tunapaswa kujua kwamba hakuna kitu kinachojitegemea chenyewe, kila kitu kinategemea vitu vingine. Hivyo hatua yoyote unayochukua, jua italeta matokeo unayotegemea na usiyotegemea.
Unapofanya maamuzi, fikiria mfumo mzima unaohusika na kile unachotaka kufanyia maamuzi na siyo kukiangalia chenyewe. Angalia matokeo ya muda mfupi na ya muda mrefu, pia angalia matokeo unayotegemea na usiyotegemea. Ukifikiria vitu vyote hivyo, utaweza kufanya maamuzi bora.
MBILI; UKUAJI NA UKOMO.
Tunapofanya maamuzi tunapaswa kuangalia kiasi cha kile tunachofanyia maamuzi, jinsi kinavyoweza kukua zaidi na hata ukomo wake. Mfano kuna kitu tunaweza kufanya maamuzi mazuri kikiwa kidogo, lakini kinapofika ukubwa fulani maamuzi hayo hayo yanakuwa mabaya.
Pia unapojaribu kuboresha kitu au mfumo wowote angalia kwanza ukomo na vikwazo vilivyopo. Kwa sababu kufanya maamuzi yoyote bila ya kujua ukomo na vikwazo, na ukaweka nguvu au juhudi zaidi, unapoteza nguvu na juhudi hizo.
TATU; VISABABISHI.
Kila kitu kinachotokea kwenye maisha kina visababishi ambavyo vipo nyuma yake, hakuna kinachotokea kama ajali. Hivyo ili kuweza kutatua tatizo, au kufikia lengo, hatua ya kwanza kuchukua ni kujua visababishi vya matokeo unayoyataka.
Mara nyingi visababishi huwa vinakuwa vingi, ambavyo vina mwingiliano mkubwa.
Jua visababishi vya matokeo unayotaka, na huo ndiyo msingi unaopaswa kuufanyia kazi. Ukiweza kufanyia kazi visababishi, matokeo yatakuwa mazuri.
NNE; NAMBA NA MAANA ZAKE.
Tumia namba katika kuhesabu na kupima kiwango cha kitu unachofanyia kazi. Badala ya kutumia maneno kama wingi, uchache au kukadiria, tumia namba halisi. Unapotumia namba unapata picha halisi ya kile unachofanyia kazi.
TANO; UWEZEKANO NA MATOKEO MBADALA YA KITU KUTOKEA.
Kila kitu kina nafasi ya kutokea, ila utokeaji wa vitu unatofautiana kulingana na uwezekano wake, yaani probability. Kitu ambacho kina uwezekano mdogo wa kutokea, au kinachotokea mara chache ndani ya muda mrefu, haimaanishi kwamba hakiwezi kupotea.
Unapofanya maamuzi yako, tumia uwezekano wa kitu kutokea, lakini usijidanganye kwamba kwa sababu kitu kinatokea mara chache basi hakiwezi kutokea, au kwa kuwa kimetokea siku za karibuni hakitatokea tena.
SITA; WINGI WA MATUKIO.
Pale maamuzi unayofanya yanapohusisha matukio mengi, nafasi za kushindwa au kukutana na ugumu zinakuwa nyingi zaidi. Kwa mfano kama mchakato unapitia vitengo vitano, na kila kitengo kina asilimia 10 ya kushindwa, ukikusanya vitengo vyote vitano, asilimia ya kushindwa inakuwa kubwa zaidi.
Hivyo unapofanya maamuzi, angalia wingi wa matukio yanayohusika ili kufikia matokeo unayopata na kuwa na maandalizi sahihi ili usikwame.
SABA; MGONGANO NA MIUJIZA.
Kuna mambo huwa yanatokea ambayo hatuwezi kuyaelezea, mara nyingi huwa tunakimbilia kusema mambo hayo ni miujiza, lakini kwa uhalisia kunakuwa na mgongano wa mambo ambayo hatukutegemea yatokee.
Unapoweka mipango yako na hatua za kuchukua, jua kwamba chochote usichotegemea kinaweza kutokea, hivyo kuwa na maandalizi sahihi. Pia epuka sana kutabiri mambo yajayo, kwa kuwa huwezi kutabiri kwa usahihi.
NANE; UHAKIKA WA USHAHIDI.
Huwa tunatumia ushahidi mbalimbali katika kufikia maamuzi, lakini tunachopaswa kujua ni kwamba siyo kila ushahidi ni wa uhakika wa asilimia 100. Hata vipimo vingi huwa vina nafasi ya makosa. Mfano mtu anaweza kupimwa ugonjwa fulani kipimo kikasema anao na kumbe hana. Au kipimo kikasema mtu hana ugonjwa wakati anao.
Unapaswa kujua uhakika wa ushahidi unaotumia katika kufanya maamuzi yako, na kadiri unavyokuwa na ushahidi mwingi ndivyo unavyoweza kuwa na uhakika zaidi.
TISA; USHAHIDI UNAOPOTOSHA.
Kutumia historia ya nyuma kama ushahidi wa tukio la sasa ni kitu ambacho kinaweza kukupotosha. Hivyo tunapaswa kuwa makini sana katika ushahidi tunaotumia. Pia kama ushahidi tunaotumia ni wa kitafiti, lakini utafiti huo umehusisha watu wachache, unaweza kutupotosha kwenye maamuzi tunayofikia.
Ni muhimu sana kuwa makini na hili katika kuajiri, uwekezaji na hata biashara, kwa sababu wengi huangalia historia ya nyuma katika kufanya maamuzi, lakini kesho mambo yanaweza kuwa tofauti na matokeo yakawa tofauti kabisa na unavyotarajia.
MWONGOZO WA KUFIKIRI KWA USAHIHI.
Baada ya kuona makosa ya kisaikolojia tunayofanya pamoja na fizikia na hesabu ya kufanya maamuzi mabovu, sasa tunakwenda kujifunza mwongozo wa kufanya maamuzi sahihi. Huu ni mwongozo unaopaswa kuutumia ili kufanya maamuzi yako ili usifanye makosa yanayokugharimu.
Mwongozo huu una mambo 12 muhimu ya kuzingatia.
MOJA; MIFANO YA UHALISIA.
Mifano ya uhalisia inatusaidia kuelewa jinsi dunia inavyofanya kazi. Mifano hii inatuoa majibu ya KWA NINI na KWA VIPI. Unapojikuta kwenye hali ya kufanya maamuzi, tumia mifano ya uhalisia katika kufikia maamuzi. Tumia sheria za fizikia, sheria za hesabu na hata sheria za asili, kuona uhalisia wa jambo. Jiulize kwa nini kitu kipo kama kilivyo na pia jiulize nini kimefanya kiwe vile kilivyo. Kwa kutumia mifano ya uhalisia na kuhoji, utaweza kuona ukweli kama ulivyo.
Mfano mtu anakushirikisha fursa ya uwekezaji ambayo unaona kabisa haiendani na sheria za asili, kwamba fedha inawekwa na inakua, bila ya kazi yoyote kuhusika, huna hata haja ya kujiuliza mara mbili, unajua hapo kuna utapeli unaendelea.
MBILI; MAANA.
Unapaswa kupata maana ya kitu kabla ya kukitumia au kuafikiana nacho. Maneno, maelezo, malengo hayatuelezi chochote kama hatuelewi maana yake. Hata maarifa unayoyapata, hayana manufaa kwako kama huelewi maana yake. Hivyo unapokuwa kwenye hali ya kufanya maamuzi, hakikisha unaelewa maana ya kila unachojihusisha nacho. Usikubali tu kubeba maneno ambayo huelewi maana zake. Pia unapojifunza, hakikisha unaelewa maana ya kile ulichojifunza na jinsi ya kukitumia kwenye maisha yako.
TATU; KURAHISISHA.
Watu wengi huwa wanapenda kufanya mambo yaonekane magumu wakiamini kuwa ndiyo yataonekana ni muhimu. Rahisisha kila unachojihusisha nacho, hata kama kitu ni kigumu kiasi gani, kirahisishe kwanza ndiyo ukifanyie kazi. Unaporahisisha unaona hatua za kuchukua, lakini jambo linapokuwa gumu unakwama usijue hatua gani ya kuchukua.
Kama tatizo au jukumu ni kubwa, ligawe kwanza kwenye vipande vidogo vidogo ambavyo ni rahisi kuelewa na kuanza kuchukua hatua, kwa njia hii utaweza kufikia maamuzi sahihi na kuchukua hatua sahihi. Epuka sana kuyafanya mambo kuwa magumu ukidhani ndiyo sifa. Einsten aliwahi kusema, kama huwezi kukielezea kitu kwa urahisi, basi hujakielewa. Sasa kama hujakielewa kitu, maamuzi yoyote unayofanya yatakuumiza baadaye.
NNE; KANUNI NA MACHUJIO.
Kuna mambo mengi sana ya kuzingatia katika kufikia maamuzi, na unaweza kuwa na muda mchache, hivyo kupitia kila jambo kukawa ni kugumu kwako. Ili kuondokana na changamoto hii, unapaswa kujiwekea kanuni na machujio ambayo yatarahisisha kazi yako ya kufanya maamuzi.
Kwa kujijua wewe mwenyewe, kujua uwezo wako na mipango yako, unapaswa kujiwekea kanuni za mambo gani utafanya na yapi ambayo hutafanya. Hivyo unapokutana na maamuzi ya kufanya, unaangalia kwanza kama kitu hicho kipo kwenye upande wa mambo unayofanya. Kama kipo kwenye upande wa mambo usiyofanya, huna hata haja ya kuanza kufikiria kama inakufaa au la. Mfano kama umeshajiambia hutafanya biashara ya mtandao, mtu anapokuambia kuna fursa nzuri ya biashara ya mtandao, huna hata haja ya kwenda kusikiliza kwamba kutakuwa na kitu cha tofauti, hiyo tayari haipo kwenye orodha ya vitu utakavyojihusisha navyo, hivyo unaachana nayo mapema. Hii inakupunguzia wingi wa maamuzi ya kufanya.
Kwa kujiwekea kanuni za mambo gani utafanya na yapi hutafanya, utazikosa fursa nyingi nzuri, lakini pia itakuepusha kufanya makosa mengi yatakayokugharimu.
Kanuni nyingine unazoweza kujiweka ni kuweka juhudi kwenye kila unachofanya, kushirikiana na watu waaminifu pekee, kuachana na kitu ambacho hukielewi.
TANO; MALENGO.
Unapaswa kuwa na malengo ambayo unayafanyia kazi, na yenye sababu kwa nini unataka kuyafikia. Malengo hayo yanapaswa kuwa wazi, makini, yanayopimika na yenye ukomo wa muda.
Maamuzi yote unayofanya, unapaswa kwanza kuangalia malengo uliyonayo ili usitoke nje ya malengo hayo. Kama huna malengo, kila kitu kitakuwa sahihi kwako kufanya, na hivyo utakosa msimamo na kujihusisha na mambo usiyoyaelewa, kitu kitakachokupelekea kushindwa.
SITA; MBADALA.
Tuna rasilimali ambazo ni haba na uhitaji ni mkubwa. Kuanzia muda wetu, nguvu zetu na hata fedha zetu. Swali ni je tunatumiaje rasilimali hizi ambazo zina ukomo katika mazingira ambayo yanatutaka tuweke rasilimali hizo kwenye kila kitu?
Njia pekee ni kujiwekea vipaumbele, kisha kupima kila unachotaka kufanya katika vipaumbele hivyo. Kama kuna kitu kipya na mbadala ambacho unataka kufanya, anza kukipima kwa vipaumbele vyako. Angalia pia faida na hasara za kufanya kitu kabla hujaamua kuweka rasilimali zako ambazo zina ukomo.
Ukiwa makini katika kupangilia matumizi ya rasilimali zako hizi, utaondoka kwenye msongo wa kukosa muda, kukosa fedha na kukosa nguvu pia, kwa sababu umetawanya sana rasilimali zako.
SABA; MATOKEO.
Kwa kila maamuzi tunayoyafanya, kuna matokeo tunayoyapata. Yapo matokeo ambayo tunayategemea na ambayo hatuyategemei, hivyo tunapaswa kuwa tayari kupokea matokeo yote.
Angalia mfumo mzima na matokeo yote yanayopatikana baada ya kufanya maamuzi au kuchukua hatua, kisha pia madhara yake kwenye matokeo ya mwisho unayotaka kupata.
NANE; KUHESABU.
Lazima uweze kuhesabu matokeo ya kila hatua unayochukua. Na hii ndiyo kazi ya hesabu, kwa sababu zinatuwezesha kupima matokeo yanayopatikana. Lazima tuwe na kigezo tunacholinganisha nacho matokeo tuliyopata. Bila ya kuwa na kigezo huwezi kujua kama unafanya vizuri au unafanya vibaya.
TISA; USHAHIDI.
Katika kufanya maamuzi yako, tumia ushahidi na siyo nadharia pekee. Ushahidi unatokana na uchunguzi, uangalifu, uzoefu, ulinganishi na majaribio.
Katika kufanya maamuzi yako, fuata hatua za kisayansi, ambapo unaanza kwa kuona kitu, kisha kutengeneza nadharia, halafu kuipima nadharia hiyo katika uhalisia. Kuwa tayari kujikosoa wewe mwenyewe na kuwa tayari kubadilika pale nadharia yako inapokuwa siyo sahihi baada ya kufanya majaribio.
KUMI; FIKIRI KINYUME.
Huwa tumezoea kufikiri kwa mbele, yaani tunaanzia pale tulipo sasa, na kuangalia kule tunakokwenda. Ukitaka kufanya maamuzi mazuri, unapaswa kufikiri kinyume, kwa kuangalia kwanza kule ambapo hutaki kwenda, kisha kuona njia zipi uepuke ili usifike huko. Hapa ndipo Charles Munger anapotumia kauli yake ya anachotaka kujua ni wapi akienda atakufa hivyo asiende huko.
Angalia kule ambapo hutaki kufika, kisha jua njia za kukufikisha kule na ziepuke. Kama unataka kufanikiwa kwenye biashara, fikiria ni vitu gani ukifanya utashindwa kwenye biashara, kisha usivifanye. Kama unataka kuwa na mahusiano bora, jiulize ni vitu gani ukifanya vitaharibu na kuvunja mahusiano yako kisha usivifanye.
KUMI NA MOJA; HATARI.
Kuna kelele nyingi sana zinapigwa na wengi kuhusu hatari, wengi wamekuwa wanasema bila kuchukua hatua za hatari huwezi kufanikiwa. Lakini Munger na Buffett wanasema kama unataka kufanikiwa, basi epuka sana hatari. Wanasema kilichowawezesha wao kufanikiwa kwenye uwekezaji siyo kuwekeza fedha zao kwenye maeneo yenye hatari lakini yana faida kubwa. Badala yake wamekuwa wanawekeza maeneo salama yenye faida ndogo.
Katika kufanya maamuzi yako, pima hatari kabla hujaingia. Jiulize mabaya yote yanayoweza kujitokeza na jinsi unavyoweza kukabiliana nayo. Usiingie kwenye kitu chochote kabla hujaona hatari zote na kujiandaa nazo.
KUMI NA MBILI; MTAZAMO.
Pamoja na yote ambayo tumejifunza kuhusu kufanya maamuzi bora, kuna kitu kimoja muhimu sana unachopaswa kukifanyia kazi, kwa sababu ndiyo kinaweza kukukwamisha sana. Kitu hicho ni mtazamo ulionao wewe binafsi. Unapaswa kuwa na mtazamo sahihi kuhusu maisha, mtazamo ambao ni chanya, mtanzamo wa uwezekano na usiwe mtu wa kukata tamaa.
Pia unapaswa kujua kwamba wewe ni wa tofauti na hakuna anayefanana na wewe, hivyo unapaswa kutengeneza mfumo wa maisha unaokufaa wewe na siyo kuiga mifumo ya maisha ya wengine. Unapaswa kujifunza ka wengine, lakini usibebe kama wanavyofanya wao, badala yake boresha ili iendane na maisha yako.
Tafiti za kisayansi zinaonesha kwamba watu wenye mtazamo chanya wanaishi miaka mingi kuliko wenye mtazamo hasi. Pia watu wenye mtazamo chanya wanakuwa na maisha ya furaha, afya njema na mahusiano mazuri kuliko wenye mtazamo hasi. Hivyo mara zote kuwa na mtazamo chanya, utaweza kufikiri kwa usahihi na kufanya maamuzi bora kabisa kwa maisha yako.
Rafiki, huu ndiyo mwongozo wa kufikiri kwa usahihi na kufanya maamuzi sahihi kwenye maisha yako.
#3 MAKALA YA JUMA; MAKOSA 28 YA KISAIKOLOJIA YANAYOPELEKEA KUFANYA MAAMUZI MABOVU.
Rafiki, maamuzi mabovu tunayoyafanya, yana msingi wake mkuu kwenye saikolojia yetu wenyewe. Namna tunavyofikiri na kuchukulia mambo, ina madhara makubwa kwenye maamuzi tunayofikia.
Ni rahisi sana sisi wenyewe kujidanganya, kwa kuona tunachofanya ni sahihi, na hiyo ni kwa sababu saikolojia zetu zinakuwa na upendeleo fulani ambao huwezi kuuona wewe mwenyewe.
Ili kuacha kujidanganya mwenyewe, lazima kwanza ujue saikolojia iliyo nyuma ya maamuzi mabovu unayofanya, ili wakati mwingine unapokuwa unafanya maamuzi hayo, unajikamata kabla hujakosea.
Kwenye makala ya juma nimekushirikisha makosa 28 ya kisaikolojia ambayo umekuwa unayafanya na yanapelekea kufikia maamuzi mabovu. Hii ni makala ambayo kila mtu anayetaka kuwa makini anapaswa kuisoma na kutumia makosa hayo 28 kujiepusha kufanya maamuzi mabovu.
Kama bado hujasoma makala hiyo, unaweza kuisoma sasa hapa; Makosa 28 Ya Kisaikolojia Unayofanya Na Yanayopelekea Wewe Kufanya Maamuzi Mabovu Yanayokugharimu. (https://amkamtanzania.com/2019/04/06/makosa-28-ya-kisaikolojia-unayofanya-na-yanayopelekea-wewe-kufanya-maamuzi-mabovu-yanayokugharimu/)
Karibu uendelee kutembelea AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA kila siku kuna makala nzuri sana zinazokwenda hewani. Weka utaratibu wa kuianza siku yako kwa makala hizo na utaianza siku ukiwa na mtazamo bora wa kukuwezesha kufanya maamuzi bora.
#4 TUONGEE PESA; MPUMBAVU HUTENGANA NA FEDHA ZAKE.
Kuna kauli moja ambayo nimekuwa naitumia pale mtu anaponiomba ushauri unaohusu fedha, hasa kwenye biashara gani mtu afanye au uwekezaji wa kufanya. Kauli hii ni; ‘kila mtu na apende pesa zake’. Ni kauli fupi sana lakini imebeba maana kubwa sana, kama mtu utachukua muda na kuitafakari.
Inapokuja kwenye fedha, huwa tunafikiri kuna watu wana uchungu na fedha zetu kuliko sisi wenyewe. Mtu anaanzisha biashara, yeye yuko mbali, anamweka mtu mwingine wa kuiendesha, lakini hapati muda wa kufuatilia kila kinachoendelea kwenye biashara hiyo, wala hafanyi hesabu za mara kwa mara kwenye biashara, siku biashara inakufa anamlalamikia aliyekuwa anaiendesha. Hii ndiyo maana halisi ya upumbavu.
Mtu anaambiwa kuna biashara au uwekezaji ambao unalipa kweli, unaweka fedha zako na baada ya muda mfupi unapata faida mara mbili, huhitaji kufanya kazi yoyote, wewe unakaa tu na unaanza kuvuna faida ya fedha ulizoweka. Mtu anaamini maelezo hayo, na tamaa inamwingia, anachukua fedha nyingi, wengine hata kukopa, na kuwekeza kwenye kitu hicho, kinachofuatia ni kilio, kwani faida aliyoahidiwa haipati na fedha aliyowekeza imepotea. Hakuna upumbavu zaidi ya huo.
Rafiki, unapokuwa na fedha, kuna watu wanawaza usiku na mchana wanapataje fedha ulizonazo. Wapo wanaowaza kwa njia halali na hivyo wanakushawishi ununue vitu wanavyouza, na wapo wanaowaza kwa njia zisizo halali hivyo wanakuja na njia ya kukutapeli, kwa kuibua tamaa zako au kutumia uzembe wako.
Sasa kinga pekee ya kukuepusha wewe kupoteza fedha zako, ni kutokuwa mpumbavu. Kwa sababu mpumbavu anatengana na fedha zake haraka mno, yaani mpumbavu akipata fedha, hazikai hata muda kidogo, zinatengana naye na kwenda kwa werevu. Vita yako ya kwanza kupigana ni kuhakikisha unaondokana na upumbavu.
Na kwenye upande wa fedha, epuka sana makosa 28 ya kisaikolojia tuliyojifunza hapo juu, maana mengi yanakutenganisha wewe na fedha zako. Na muhimu zaidi, kila wakati jikumbushe kauli niliyokuambia hapo juu ‘kila mtu na apende fedha zake’. Unapowekeza fedha zako mahali, kwanza elewa kwenye kile unachowekeza, na epuka kusukumwa na tamaa. Na pili, fuatilia kwa makini sana fedha zako, usifikiri kuna mtu ana uchungu na fedha zako kuliko wewe mwenyewe.
Usikubali kuwa mpumbavu wa kutenganishwa na fedha zako kirahisi, fikiri kwa kina inapokuja kwenye fedha na fanya maamuzi sahihi utakayoendelea kuyafuatilia kwa karibu.
#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KANUNI KUU YA KUPATA UNACHOTAKA.
The iron rule of nature is: you get what you reward for.
If you want ants to come, you put sugar on the floor.
– Charles Munger
Kanuni ya chuma ya asili ni hii; unapata kile ambacho unakizawadia. Kama unataka kuwapata mchwa, weka sukari na wataifuata.
Rafiki, kuna vitu huwa tunalalamikia, lakini sisi wenyewe ndiyo tunavikaribisha. Mfano una mfanyakazi ambaye anakuibia, haijalishi unamlalamikia kiasi gani, makosa ni yako, wewe ndiye unayempa fursa ya kuiba. Na siyo tu unampa fursa, bali pia unampa zawadi akishakuibia. Kwa mfano kama mtu anaiba halafu hakuna adhabu anayoipata, wala hakamatwi au kusumbuliwa kwa namna yoyote, kwenye akili yake anajifunza kwamba kumbe hapa kuiba siyo tatizo, basi anaendelea kuiba.
Anachotuambia mwanafalsafa mwekezaji Charles Munger ni kwamba, ile tabia ambayo wengine wanaonesha kwetu, sisi ndiyo tumewawezesha kuonesha tabia hiyo. Tumekubaliana nayo na huenda tunawapa zawadi kwa kuonesha tabia hiyo.
Hivyo njia pekee ya kudhibiti tabia za wengine ni kutumia ZAWADI NA ADHABU. Kama kuna kitu unataka watu wafanye, wape zawadi wanapokifanya, wanajifunza kwamba wakitaka zawadi wafanye tena. Na kama kuna kitu hutaki watu wafanye, waadhibu wanapokifanya, kwa adhabu hiyo wanajifunza kuacha kufanya kitu hicho.
Njia hii ya zawadi na adhabu unaweza kuitumia kwenye kila eneo la maisha yako, kuanzia malezi ya watoto, mahusiano mbalimbali na hata kwenye kazi au biashara. Wazawadie watu wanapofanya kile kizuri unachotaka na waadhibu wanapofanya kibaya usichotaka. Usilalamike pale watu wanapokufanyia kitu usichotaka, bali jiulize ni kwa namna gani umekuwa unawazawadia wao kufanya hivyo kisha rekebisha na utapunguza sana watu kufanya yale usiyotaka.
Rafiki, hivi ndivyo unavyoweza kufikiri kwa kina, ukafanya maamuzi sahihi na kuepuka kufanya makosa kwenye maisha yako. Inaanza na wewe kuwa tulivu, kuangalia jambo kwa uhalisia wake, kuzuia hisia na mazoea visikutawale, kufikiri kwa akili yako na kufikia maamuzi ambayo unayasimamia. Fanya hivi kwenye kila jambo na maisha yako yatakuwa bora sana.
Kwenye #MAKINIKIA ya kitabu hiki tulichochambua hapa, nitakwenda kukushirikisha njia saba za uhakika za kuwa na maisha mabovu, utajifunza kupitia hekima za Warren Buffett na Charles Munger na pia utapata mwongozo wa kutumia wakati unafanya maamuzi ili kuepuka kufanya makosa. Ili kupata #MAKINIKIA haya, jiunge na channel ya TANO ZA JUMA kwa maelekezo yaliyopo hapo chini.
#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.
Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.
Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.
Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.
Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.
Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.
Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.
Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)
Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha
Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu