Huwa tunaweka sheria mbalimbali ili kutuongoza kwenye maisha yetu, lakini siyo wakati wote sheria zinaweza kuleta matokeo mazuri.

Ndiyo maana hata kwenye tawala za nchi, licha ya sheria kuwa wazi na zinajulikana, bado tunahitaji kuwa na mahakama, ili kuweza kutumia busara na hekima kufikia maamuzi ambayo ni bora kwa kila mtu.

Haki iliyopitiliza ni udhalimu, yaani kama mtu atataka kufuata sheria jinsi ilivyo, bila ya kupindisha hata kidogo, lazima italeta uonevu kwa wengine.

Kuna wakati sheria inapaswa kuwekwa pembeni kidogo na hali kuchukuliwa jinsi ilivyo.

Kuna wakati busara na hekima zinahitajika katika kufanya maamuzi, bila ya kutumia sheria na haki.

Na hapa ndipo sisi binadamu tumepewa uwezo mkubwa kuliko wanyama wengine. Na licha ya kompyuta kuweza kufanya vitu vingi, lakini kwenye hekima na busara, haiwezi kutuzidi.

Tunachopaswa kuelewa ni kwamba, siyo kila wakati tunapaswa kufuata sheria kama zilivyo, na kutaka kufanya kitu kama kinavyopaswa kufanywa. Tunapaswa kutumia fikra zetu kwa usahihi ili kuja na maamuzi bora na ya busara.

Hili linaanzia kwenye taratibu zetu binafsi za maisha na hata kazi au biashara na linakwenda mpaka kwenye tawala za nchi na dunia kwa ujumla. Tunapaswa kujipa nafasi ya kufikiri kila kitu kwa usahihi na kufikia maamuzi ambayo ni sahihi katika hali hiyo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha