“When it comes to money, where we feel our clear interest, we have an entire art where the tester uses many means to discover the worth . . . just as we give great attention to judging things that might steer us badly. But when it comes to our own ruling principle, we yawn and doze off, accepting any appearance that flashes by without counting the cost.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 1.20.8; 11

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari GHARAMA YA KUKUBALI VITU FEKI…
Inapokuja kwenye fedha, huwa tuna kila mbinu ya kupima kama fedha ni halali au feki.
Tunapokuwa na wasiwasi kuhusu uhalali wa fedha, tuna vipimo vingi vya kudhibitisha kama fedha hiyo ni halali au la.
Hii yote ni kuhakikisha tunapata thamani halisi ya fedha na siyo kupata kitu feki.

Kadhalika kwenye vitu vingine tunavyonunua kwa fedha zetu, huwa tuna njia mbalimbali za kuangalia kama kitu ni halisi au feki. Labda ni simu umeenda kununua, hutaichukua tu na kuondoka nayo, kwanza utajihakikishia kama kweli ni simu halisi na siyo feki.

Tuna umakini mkubwa sana inapokuja kwenye fedha zetu.
Lakini inapokuja kwenye misingi yetu ya maisha,
Inapokuja kwenye maoni tunayojipa,
Inapokuja kwenye ushauri ambao wengine wanatupa,
Huwa hayujisumbui kupima uhalisia wake, tunapokea tu kama tunavyopata au kupewa.

Na hii ndiyo sababu kuu kwa nini wengi wanakwama kwenye maisha, kwa sababu wanaendesha maisha yao kwa misingi feki.
Wengi wanapewa ushauri na wengine, na kuubeba kama ulivyo, wanapoufanyia kazi na kupata matokeo tofauti na walivyotarajia, wanalaumu waliowapa ushauri huo.
Wengi wamejitengenezea maoni yao kuhusu maisha kwa mazoea waliyonayo na jinsi wengine wanavyofanya.

Rafiki, hakuna eneo unalohitaji umakini katika kuchunguza uhalisia kama kwenye misingi yako ya maisha, ushauri unaopewa na wengine na hata maoni uliyonayo juu yako.
Kushindwa kuchunguza uhalisia kwenye maeneo haya inakugharimu sana maisha yako, unapoteza muda, nguvu na hata fedha kwa mambo yasiyo na maana.

Hakikisha una kipimo sahihi cha kupima uhalisia wa kila kitu kwenye maisha yako. Usipokee chochote bila ya kukiingiza kwenye kipimo chako na kupata uhalisia au ufeki wake.

Ukawe na siki bora sana ya leo, siku ya kupima uhalisia wa kila unachojihusisha nacho kwenye maisha yako na kuepuka gharama ya vitu feki.
#PimaKilaKitu, #AminiLakiniDhibitisha, #HojiUsahihiWaKitu

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha