“From the very beginning, make it your practice to say to every harsh impression, ‘you are an impression and not at all what you appear to be.’ Next, examine and test it by the rules you possess, the first and greatest of which is this—whether it belongs to the things in our control or not in our control, and if the latter, be prepared to respond, ‘It is nothing to me.’”
—EPICTETUS, ENCHIRIDION, 1.5
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari PIMA MTAZAMO WAKO…
Mtazamo tulionao ni njia ya mkato kwetu kufanya maamuzi kwenye maisha yetu.
Mtazamo umekuwa unatusaidia kuvuka mlolongo wa maelezo na vigezo mbalimbali katika kufikia maamuzi.
Ndiyo maana tunaweza kumwona mtu mara moja na tukajua kama anafaa kwenda na sisi au la.
Pamoja na uzuri huu wa mtazamo katika kufanya maamuzi, mara nyingi mtazamo tulionao umekuwa unatupotosha.
Kuna maamuzi mabovu tunayoyafanya kupitia mtazamo tulionao.
Hivyo badala ya kuamini mtazamo wako kwa asilimia 100, mara kwa mara pima mtazamo wako.
Pamoja na kuona kwamba kitu kipo kwa namna fulani, kulingana na mtazamo wako, jiulize vipi kama kingekuwa tofauti na unavyochukulia. Kisha jipe ushahidi unaokubaliana na kinyume cha unachoamini wewe.
Kwa kupima hivi, utaona vingi ambavyo hukuwa unaona awali.
Kwa sehemu kubwa, mtazamo tulionao umejengwa na hisia na mazoea yetu wenyewe. Hivyo tusipokuwa tunajipima na kukuza zaidi mtazamo wetu, tutakuwa tunajidanganya sisi wenyewe.
Pima mtazamo wako mara kwa mara na utaweza kufanya maamuzi bora mara zote.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kupima mtazamo ulionao kwenye mambo mbalimbali ili uweze kufanya maamuzi bora.
#PimaMitazamoYako, #DhibitiHisiaZako, #OndokanaNaMazoea
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha