Kwa watu ambao hawana fedha nyingi, ugumu wa kupata fedha ni sehemu ya maisha yao, mara nyingi wanaishi kwenye hali ya kukosa fedha na hata kuwa wamefilisika. Hilo ni rahisi kueleweka na kila mtu.
Kitu ambacho siyo rahisi kueleweka ni pale mtu ambaye ameweza kujijengea utajiri mkubwa, mtu ambaye ana fedha nyingi na kuonekana wameshajijengea usalama wa kifedha anafilisika ghafla.
Yaani ghafla tu mtu anapoteza fedha zote alizokuwa nazo na maisha yanakuwa magumu sana kifedha. Wengi hutafuta sababu mbalimbali za kuelezea hili, wapo wanaochukulia kwamba mtu huyo alibahatisha kupata fedha hizo na sasa bahati imeondoka upande wake. Wengine watasema alizipata kwa njia za kishirikina na sasa amekosea masharti na zimeondoka.
Sababu hizo, na nyingine zinazofanana na hizo siyo sahihi. Ni sababu rahisi sana kwa swali gumu, kwa sababu kama mtu alishaweza kuwa na fedha nyingi, kuna kitu alikuwa anafanya kwa usahihi, hivyo kufikiri bahati au ushirikina ndiyo umewapa fedha hizo ni kujidanganya na kujipotosha.
Sababu kubwa inayopelekea watu wenye fedha kufilisika ni MIKOPO. Ukiangalia wengi wanaoanguka kutoka kwenye utajiri na kwenda kwenye umasikini, mikopo inakuwa ni sababu kubwa. Kwa kuwa mtu ana fedha, na kwa kuwa anahitaji fedha zaidi ili kupiga hatua zaidi, kuchukua mkopo ni kitu kinachoonekana ni rahisi na bora. Lakini wengi hujikuta wameingia kwenye mikopo mingi, na ambayo hawawezi kuizalisha vizuri na mwishowe inakuwa mzigo kwao.
Kama unataka kuepuka kuanguka kifedha pale unapopiga hatua, kuwa makini sana na mikopo. Kwa sababu kadiri unavyokua kifedha kila mtu atakuambia unapaswa kuchukua mkopo ili ukue zaidi. Taasisi za kifedha zitakuambia unakopesheka, na wewe mwenyewe kwa kufanikiwa eneo moja, unajidanganya unaweza kufanikiwa kila eneo.
Chukua mkopo pale tu unapoweza kujilipa wenyewe, yaani pale unapokuwa na uhakika mkopo huo utatengeneza faida inayotosha kulipa mkopo bila ya wewe kutoa fedha zako mfukoni kulipa mkopo huo. Kama hujafikia ngazi hiyo ya mkopo kuweza kujilipa wenyewe, bado hujastahili kuchukua mkopo.
Pia unapozidi kupata fedha, jifunze sana kufanya maamuzi kwa kufikiri na kuepuka hisia. Kwa sababu hisia zitakutenganisha na fedha zako haraka mno. Yajue makosa 28 ya kisaikolojia ambayo wengi huyafanya kwenye maamuzi na yaepuke ili usifanye makosa. Yasome makosa hayo 28 hapa; Makosa 28 Ya Kisaikolojia Unayofanya Na Yanayopelekea Wewe Kufanya Maamuzi Mabovu Yanayokugharimu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,