Rafiki yangu mpendwa,

Mwanafalsafa mwekezaji Charles T. Munger ambaye ni mtu wa karibu wa mwekezaji mwenye mafanikio makubwa duniani Warren Buffett, anasema kuna njia mbili za kuendelea kile unachokitaka.

Njia ya kwanza ni kujua wapi unataka kufika na kujua njia ya kukufikisha hapo unapotaka kufika na kisha kuifuata. Hapa utajua kipi sahihi cha kufanya na kukifanya ili kufanikiwa.

Njia ya pili ni kujua wapi hutaki kufika na njia za kukufikisha kule ambako hutaki kufika kisha kuziepuka. Hapa unajua kile ambacho siyo sahihi kufanya na kuepuka kukifanya.

Tukichukua mfano wa biashara, unaweza kuanza biashara ukiwa na picha ya mafanikio ya biashara hiyo, na kuchukua hatua sahihi za kukufikisha kwenye picha hiyo. Lakini pia unaweza kuanza kwa kujiuliza ni vitu gani nikifanya biashara yangu itashindwa na kufa kabisa, kisha unaepuka kufanya vitu hivyo.

Njia hii ya kufikiria usikotaka kufika na kisha kuepuka, Munger anaiita ni kufikiri kinyume, na ina nguvu kubwa sana kwetu kupiga hatua kubwa kwenye maisha yetu.

Katika hotuba yake kwa wahitimu wa chuo kikuu cha Havard mwaka 1986, Charles Munger aliwashirikisha njia saba za uhakika za kuwa na maisha mabovu.

MUNGER

Hapa Munger alitumia mfumo wake wa kufikiri kinyume, wa kufikiria ni wapi hutaki kwenda kisha kuepuka kwenda huko. Hivyo kwa kujua njia hizi za uhakika za kuwa na maisha mabovu, utaweza kuziepuka na kutokuwa na maisha mabovu.

Zifuatazo ni njia saba za uhakika za kuwa na maisha mabovu, unazopaswa kuziepuka sana kwenye maisha yako.

Moja; kutumia kemikali zinazoathiri akili.

Matumizi ya kemikali zinazoathiri akili kama pombe, madawa ya kulevya, sigara, bangi na vilevi vingine ni njia ya uhakika ya kuwa na maisha mabovu. Hakuna manufaa yoyote mtu anayapata kwa matumizi ya kemikali hizi. Kama unataka kuwa na maisha bora, epuka matumizi ya kemikali zinazoathiri akili.

Mbili; wivu.

Wivu ni njia ya uhakika ya kuwa na maisha mabovu, pale unapotumia muda wako mwingi kufuatilia maisha ya wengine na kujilinganisha nao, ni muda ambao unashindwa kuutumia kwa yale muhimu kwako.

Kama unataka kuwa na maisha bora, acha kufuatilia maisha ya wengine, ishi maisha yako na weka malengo yako na yafanyie kazi. Wengine wanafanya nini au wana nini hiyo siyo kazi yako, achana nayo.

Tatu; chuki.

Hakuna kitu kinaharibu maisha kama chuki, kwa sababu unapokuwa na chuki kwa mtu yeyote au kitu chochote, ni kujibebesha mzigo wewe wakati mwenzako yuko huru. Unajiweka kwenye kifungo ambacho anayekufunga hajui hata kama amekufunga.

Usiwe na chuki kwa yeyote au chochote, samehe kila mtu na muhimu zaidi jisamehe wewe mwenyewe. Kuwa huru wakati wote na nguvu zako peleka kwenye kufikia malengo yako na siyo kubeba chuki kwa wengine.

Nne; usiwe mtu wa kutegemewa.

Usiwe mwaminifu kwenye maisha yako, ahidi vitu na usitekeleze, ukipewa kazi usifanye kwa umakini na chelewesha kuikamilisha, kwa kifupi kuwa mzembe utakavyo. Hii ni njia ya uhakika ya wewe kushindwa na kuwa na maisha mabovu. Yaani ukifanyia njia hii moja kazi, utakuwa na maisha mabovu hata kama kitu gani kitafanywa kwako.

Ili kuwa na maisha bora unahitaji kujenga jina lako, kuwa mwaminifu na mtu unayeweza kutegemewa, ambaye neno lako linakuwa sheria na unatekeleza kila unachoahidi.

Tano; jifunze kwa uzoefu wako pekee.

Usikubali kabisa kujifunza kupitia uzoefu wa wengine, kila kitu mpaka ukijaribu wewe mwenyewe kwanza ndiyo ukubaliane nacho. Ukiona wengine wamekosea usijifunze kwao na kufanya tofauti, bali fanya kama walivyofanya wao na ukosee ili ujifunze kwa uzoefu wako. Hii ni njia ambayo siyo tu itafanya maisha yako kuwa mabovu, bali pia yatakuwa magumu sana.

Ili kuwa na maisha bora unapaswa kujifunza kupitia wengine, chukua uzoefu wa wengine na ufanyie kazi. Usirudie makosa ambayo wengine wameshafanya, na kwa chochote unachotaka kufanya, angalia waliofanikiwa kwenye kitu hicho wanafanyaje kisha fanya kama wao.

Sita; ukianguka usiinuke tena.

Pale unapoweka mipango na ikashindwa, pale unapojaribu kitu na ukashindwa, usijisumbue kujaribu tena. Kubali kwamba umeshindwa na huwezi tena na baki hapo chini wala usiinuke tena. Hapo kwa hakika utakuwa na maisha ambayo ni mabovu sana na ya kushindwa kabisa.

Kila mtu anaanguka kwenye maisha, hivyo kuwa na maisha bora ni kuinuka pale unapoanguka, kujifunza na kuanza tena kwa ubora zaidi. Haijalishi umeanguka mara ngapi, unachopaswa kufanya ni kuinuka na kuendelea na safari yako.

Saba; usitake kujua sehemu mbaya na kuiepuka.

Wewe amua kwenda tu kama unavyotaka kwenda, usijisumbue kujua sehemu mbaya au hatari iko wapi na kuiepuka, badala yake nenda kama unavyojisikia mwenyewe. Kwa njia hii utashindwa na kuanguka kwenye kila unalojaribu.

Kuwa na maisha bora unapaswa kufikiri kinyume, na kufuata msingi wa Munger ambao ni kujua sehemu gani ukienda utakufa na hivyo kuepuka kwenda sehemu hiyo. Jua mambo gani ukifanya utakosa kile unachotaka na epuka kuyafanya. Siyo tu utakuwa na maisha bora, bali utaepuka hatari zisizo na maana kwenye maisha yako.

Rafiki, hizi ndizo njia saba za uhakika za kuwa na maisha mabovu, jukumu lako kwenye maisha ni moja, epuka njia hizi ili uwe na maisha bora.

Rafiki, kama ungependa kujifunza na kupata hekima zaidi kutoka kwa Charles Munger na Warren Buffett karibu ujiunge na channel ya TANO ZA JUMA, kwenye channel hiyo nimekushirikisha mengi kutoka kwa wawekezaji hao wawili, ambao wamekuwa pamoja kwa zaidi ya miaka 40 na hawajawahi kupishana kauli. Kwenye kitabu cha SEEKING WISDOM ambacho kimechambuliwa na kuweka kwenye channel hiyo, utajifunza mengi kutoka kwao. Kujiunga na channel ya TANO ZA JUMA, tuma ujumbe kwa app ya telegram messenger kwenda namba 0717396253, ujumbe uwe na maneno TANO ZA JUMA.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge