“Throw out your conceited opinions, for it is impossible for a person to begin to learn what he thinks he already knows.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 2.17.1
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KAMA UNATAKA KUJIFUNZA, KUWA MNYENYEKEVU…
Kinachowazuia watu wengi kujifunza na kupiga hatua kwenye maisha yao ni kuona kwamba tayari wanajua kila kitu.
Kama tayari unajua kila kitu, hakuna kipya unachoweza kujifunza.
Na kama hutajifunza kitu kipya, siyo tu kwamba hutapiga hatua, bali utakuwa unarudi nyuma.
Kama unataka kujifunza, unataka kuwa bora na kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako, basi kuwa mnyenyekevu.
Tambua kwamba una mengi ambayo huyajui na hivyo kuwa tayari kujifunza.
Elewa kwenye kila hali unayokutana nayo kuna kitu cha kujifunza.
Elewa kwa kila mtu unayekutana naye kuna kitu cha kujifunza.
Jua kwamba hujui mengi na kuwa tayari kujifunza na hilo litakuwezesha kupiga hatua zaidi.
Kila unapokutana na fursa ya kujifunza, weka maoni yako pembeni na jichukulie kama hujui chochote kwenye hali hiyo, kisha kuwa tayari kujifunza.
Kwa sababu ukishajiona unajua, hakuna tena nafasi ya kujifunza.
Kama una kikombe kimejaa maji, lakini wewe unataka maziwa, kuweka maziwa juu ya maji yale haitakusaidia, unapaswa kuondoa kwanza maji kwenye kikombe ndiyo upate nafasi ya kuweka maziwa.
Socrates, mmoja wa watu wenye hekima na busara kuwahi kuwepo hapa duniani, alipoulizwa kwa nini ana hekima na busara sana, alijibu kuna kitu kimoja pekee ninachojua, na kitu hicho ni kwamba hakuna ninachojua.
Hii ni sehemu nzuri sana kwetu kuanzia, kwa mtazamo kwamba hakuna tunachojua, na hivyo kuwa tayari kujifunza zaidi.
Tafuta walimu, washauri, makocha, na hata vitabu vya kujifunza kila siku, na kamwe usijiambie kitu tayari unakijua.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa na unyenyekevu na kuwa tayari kujifunza kwa kila hali na kila unayekutana naye.
#KunaMengiSanaHujui, #KuwaTayariKujifunza, #JifunzeKituKipyaLeo
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha