Inapotokea mtu amefanya kitu ambacho hukutegemea afanya, labda ni wizi, udanganyifu au usaliti, utetezi wao wa kwanza huwa ni kwamba ndiyo mara ya kwanza kwao kufanya na hawatarudia tena kufanya.

Kama tunawaamini sana watu hawa inakuwa rahisi kukubaliana nao, na kuona kweli labda ndiyo mara ya kwanza wamefanya au kujaribu.

Lakini hiyo ni kudanganya, kuna uwezekano mdogo sana wa wewe kumkamata mtu akiwa anafanya kitu kwa mara ya kwanza, yaani hajawahi kufanya kabisa, halafu amefanya na wewe ukamkamata akiwa anafanya.

Ninachokuambia ni kwamba, unapomkamata mtu akiwa anafanya kile ambacho hukutegemea afanye, basi jua hiyo imekuwa tabia yake kwa muda, ulikuwa hujajua tu.

Watu huwa hawafanyi kitu mara moja, badala yake wanarudia kufanya tena na tena, na kadiri wanavyorudia kufanya ndiyo nafasi ya kukutwa wakiwa wanafanya inakuwa kubwa.

Jua hili ili likusaidie kwenye kufanya maamuzi, kwa sababu ukikubaliana na mtu kirahisi kwamba ndiyo mara ya kwanza kufanya, utakuwa umemfundisha awe makini kwenye zaidi kwenye ufanyaji wake.

Unachoweza kufanya ni kukubaliana naye, lakini wewe kujua kwamba siyo mara ya kwanza kwake kufanya, hivyo kama kuna hatua zaidi unapaswa kuchukua basi endelea kuchukua. Usidanganyike kirahisi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha