Kila mmoja wetu amekuwa anakutana na matatizo mbalimbali kwenye maisha yake. Na matatizo mengi huanza kusumbua pale yanapokuwa makubwa.
Lakini ukweli ni kwamba, hakuna tatizo linaloanza likiwa kubwa.
Hakuna mtu anaamka siku moja na kujikuta kwenye deni la mamilioni.
Hakuna tu anaamka siku moja na kujikuta ana uzito uliopitiliza.
Na wala hakuna mtu anayeamka siku moja na mahusiano yake yakawa na matatizo makubwa.
Matatizo yote haya huwa yanaanza kidogo kidogo, kwa kiwango ambacho hakitusumbui, tunaendelea nayo mpaka yanakuwa makubwa ndiyo tunakuja kustuka kwamba tuna matatizo.
Unapoanza kuona fedha hazikutoshi na inabidi ukope kidogo kidogo, huo ndiyo wakati wa kuchukua hatua kabla hujaingia kwenye madeni makubwa.
Unapoanza kuona nguo ulizozoea kuvaa zamani zinaanza kukubana, hapo unapaswa kujua uzito unakwenda upande ambao siyo sahihi.
Unapoanza kuona muda na maelewano na mwenzako siyo kama ilivyokuwa awali, ni wakati wa kuchukua hatua kuboresha mahusiano kabla tatizo halijawa kubwa zaidi.
Kuzuia makubwa yasitokee ni kuchukua hatua kwenye mambo madogo.
Kama waswahili wanavyosema, usipoziba ufa utajenga ukuta. Ni rahisi kupuuza ufa kwenye maeneo mbalimbali kwenye maisha yetu, lakini ukuta unapoanguka, ndiyo tunahangaika kama vile ni dharura.
Kuna dharura chache sana kwenye maisha, nyingi tunazoita dharura ni uzembe wetu wenyewe kwenye maisha, uzembe wa kushindwa kuyaona matatizo yakiwa madogo na kuyashughulikia.
Kuwa mfuatiliaji wa karibu sana wa maisha yako, unapoona kitu kidogo tofauti na kinavyopaswa kuwa, usijidanganye kwamba ni kidogo, badala yake chukua hatua kukitatua. Tatua matatizo yakiwa madogo na hutakuja kuwa na matatizo makubwa kwenye maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,