Huwa nasema ukitaka kuyaelewa maisha, basi ielewe asili.

Kama hujui misingi gani uishi kwenye maisha yako, basi angalia misingi ya asili, angalia asili inajiendeshaje na yaendeshe maisha yako hivyo na utakuwa na maisha bora sana.

Moja ya kanuni muhimu za asili unazopaswa kuzijua na kuziishi ni kanuni kwamba maisha ni mwendo.

Ukiangalia kwenye asili, kila kitu kipo kwenye mwendo, na kitu kikishaacha kuwa kwenye mwendo basi kimekufa.

Dunia yenyewe ipo kwenye mwendo, wa kuzunguka kwenye mhimili wake kila siku na kulizunguka jua kila mwaka. Dunia ikisimama leo hii isiwe tena na mwendo, unakuwa ndiyo mwisho wa maisha hapa duniani.

Vyombo vyote vya maji vipo kwenye mwendo, mito inatiririsha maji kwenda maziwani na baharini, na huko maji yanageuzwa kuwa mvuke kisha mawingu halafu mvua. Maji yakituama mahali ni chanzo cha kila aina ya magonjwa kwa sababu yanakuwa yamekufa.

Kila kiumbe hai kipo kwenye mwendo, kuanzia miti ambayo tunaiona imekaa eneo moja, lakini mizizi yake ina mwendo kila siku. Kadhalika mbegu za mimea hiyo zinajiingia kwenye mwendo ili kuweza kusambaa zaidi.

Inapokuja kwetu sisi binadamu, kipimo cha uhakika cha maisha ni mwendo. Mapigo ya moyo ni kipimo cha kwanza kujua kama mtu yupo hai. Kama hakuna mapigo ya moyo hakuna maisha. Na viungo vyote vipo kwenye mwendo, mapafu, utumbo, damu, mishipa ya fahamu na kila aina ya kiungo.

Sasa inapokuwa kwenye maisha yetu ya kila siku, kama tunataka kufanikiwa, kanuni ni moja, kuwa kwenye mwendo, kuwa na kitu cha kufanya, kuwa na hatua ya kupiga. Usikubali kubaki pale pale ulipo wakati wote.

Iwe ni kwenye kazi au biashara, hakikisha unapiga hatua zaidi kila siku, unakuwa bora zaidi, unajaribu mambo mapya na makubwa zaidi.

Maisha ni mwendo, kila siku kuwa kwenye mwendo na usijikwamishe popote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha