Kwenye jambo lolote maishani mwako, nafasi nzuri kwako kwenda ni ile yenye mkusanyiko mdogo wa watu. Hapo ndipo unapoweza kupata nafasi ya kufanya kitu na kikaonekana na pia ukapata manufaa mazuri.

Lakini hivi sivyo asili yetu binadamu ilivyo, tunapenda kwenda sehemu yenye mkusanyiko mkubwa wa watu, tukiamini kwamba wengi hawakosei. Upo mpaka usemi kwamba kifo cha wengi harusi, kwamba ukiwa ndani ya wengi, hata ukikosea basi haiumizi sana kama ukikosea ukiwa mwenyewe.

Lakini kumbuka wewe unataka kufanya makubwa, unataka kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako, hivyo wajibu wako ni kwenda sehemu yenye mkusanyiko mdogo wa watu.

Iwe ni kwenye kazi, biashara na hata mambo mengine ya maisha, sehemu yenye watu wachache ndiyo bora kwako.

Tuchukue mfano wa biashara, ukiingia kwenye biashara ambayo kila mtu anafanya, unajiingiza kwenye ushindani mkali na utapotelea kwenye kelele za kila mtu. Lakini ukienda kwenye biashara ambayo wachache wanaifanya, una nafasi ya kuonekana, una nafasi ya kuwahudumia wateja wako vizuri na wakarudi tena kwako.

Usikimbilie kundi kubwa, bali angalia eneo lenye wachache na jua hapo ndipo penye nafasi ya kujijenga wewe.

Lakini pia unapaswa kuwa makini na eneo ambalo halina mtu kabisa, usifikiri ndiyo umepata fursa ya wewe kulitawala, mara nyingi maeneo ambayo hayana watu kabisa basi hayana thamani. Ni vigumu sana wewe ukawa mtu wa kwanza kuiona thamani hiyo, chunguza kwa umakini na utagundua wapo ambao walishajaribu na ikashindikana kutokana na sababu ambazo zipo nje ya uwezo wa yeyote kuzitatua.

Hivyo kama hutaki kusumbua akili yako sana kwenye kutafuta fursa zilizojificha, epuka eneo lenye watu wengi, na epuka eneo ambalo halina watu kabisa, wewe angalia eneo lenye wachache na ingia hapo ukaweke utofauti wako na utapata nafasi ya kukua zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha