“These are the characteristics of the rational soul: self-awareness, self-examination, and self-determination. It reaps its own harvest. . . . It succeeds in its own purpose . . .”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 11.1–2

Ni siku nyingine mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Ni shukrani pekee tunayopaswa kuitoa kwa kuiona siku hii, kwa sababu hatujaiona kwa nguvu na akili zetu, bali kwa bahati tu.
Hatutakuja kuwa na siku nyingine kama hii, hivyo tuitumie vizuri.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari ALAMA ZA MTU ANAYEFIKIRI KWA KINA…
Wote tunajua ni jinsi gani ilivyo vigumu mtu kufikiri kwa kina zama hizi ambazo kilicho maarufu ndiyo sahihi na kinachofanywa na wengi ndiyo kinaaminika.
Lakini pia tunajua kwamba kitu kufanywa na wengi haihalalishi usahihi wake kama siyo sahihi.
Tunapaswa kufikiri kwa kina kwa kutumia akili zetu kama tunataka kufanya maamuzi mazuri na kupata matokeo bora.

Zipo alama tatu za mtu anayefikiri kwa kina,
Moja, anajitambua yeye mwenyewe, huwezi kufikiri kwa kina kama hujijui wewe mwenyewe.
Mbili, anajitathmini kwenyewe, anajipina kwa kila anachofanya na matokeo yake.
Tatu, anafanya maamuzi yake mwenyewe, hafanyi kile ambacho wengine wanafanya, bali anafanya kilicho sahihi kwake, kulingana na kujitambua kwake na tathmini ambayo amekuwa anafanya.

Je una alama hizo tatu?
Je umekuwa unasimamia misingi hiyo katika kufanya maamuzi yako?
Kama jibu ni ndiyo, upo kwenye njia sahihi na unafanya maamuzi sahihi.
Kama jibu ni hapana, upo kwenye njia ya upotevu na unapaswa kuiacha mara moja.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa mtu unayefikiri kwa kina, kwa kujitambua, kujitathmini na kufanya maamuzi yako mwenyewe.
#Jitambue, #Jitathmini, #Jiamulie

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha