Kila mmoja wetu anasumbuliwa na tabia hii ya kuahirisha mambo. Unapanga kabisa kwamba utafanya vitu gani, lakini wakati wa kufanya unapofika unaahirisha, unajiambia utafanya kesho au wakati mwingine.
Zipo njia nyingi za kuondokana na tabia hii, lakini nyingi zinaishia kukufanya uahirishe zaidi kuliko kuachana na tabia hiyo.
Kinachofanya iwe rahisi kwako kuahirisha ulichopanga kufanya ni kuwa na muda mwingi wa kufanya jambo hilo.
Kwa mfano kama una jambo muhimu unalopaswa kukamilisha ndani ya masaa matano, unaweza kulifanyia kazi kwa masaa matano bila ya kuruhusu usumbufu wowote. Lakini kwa jambo hilo hilo kama unapaswa kulikamilisha ndani ya siku saba, huwezi kufanya kazi kwa dakika 20 bila ya kuruhusu usumbufu.
Kama unavyoona kwenye mfano huo, jambo la kufanya halijabadilika, ila kilichobadilika ni muda tunaoweza kulifanya, na muda umebadili mtazamo wetu kwenye ufanyaji.
Tunapokuwa na muda mwingi wa kufanya jambo inakuwa rahisi kwetu kuahirisha kuliko tukiwa na muda mfupi.
Hivyo basi, kama tunataka kuondokana na tabia hii ya kuahirisha mambo, tujipe muda mfupi wa kukamilisha jambo lolote tunalopanga. Kwa kila unachopanga kufanya, kipe nusu ya muda uliozoea kukifanya. Wape watu ahadi ya kukamilisha kitu mapema kuliko wanavyotegemea.
Na kama unaona kujipa mwenyewe muda haikusukumi sana, chagua mtu wa kukusimamia, ambaye utampa muda uliojiwekea kukamilisha jambo, na kama kwa muda huo utakuwa hujakamilisha kuna gharama kubwa utakayoilipa.
Ubongo wetu una uwezo mkubwa sana wa kufanya makubwa, lakini huwa haupendi kujisumbua, unapenda kudhibiti sana matumizi ya nguvu, na kuzitunza kwa matumizi ya baadaye. Unapojiwekea muda mfupi wa kukamilisha jambo, ubongo unasoma hilo kama tishio na kukuruhusu utumie nguvu iliyohifadhiwa kwa ajili ya kuvuka tishio hilo.
Punguza muda unaojipa kufanya mambo na utaweza kuondokana na tabia ya kuahirisha mambo.
Angalizo, muda unaojipa usiwe mfupi sana kiasi kwamba haiwezekani kabisa kukamilisha jambo hilo. Ukijipa muda mfupi sana utapata msongo mkali ambao utakuzuia kabisa kuchukua hatua.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kwa Elimu ya kutoendelea kuhairisha mambo ya kufanya. Naona mfano mzuri tangu nimejipa jukumu la kusoma kurasa za mafanikio, tangu huu mwaka uanze sijaacha kusoma hata siku moja ila lazima upambane sana kuna wakati unahisi kuchoka au kukosa muda, muhimu nasimamimia pale pale kwamba ni jukumu langu na lazima nilitekeleze. Asante sana kocha.
LikeLike
Vizuri sana Beatus,
Ni kweli inahitaji upambane sana, lakini unapojiambia utafanya na hakuna namna nyingine, unapata nguvu ya kuvuka kikwazo chochote kinachojitokeza.
LikeLike
Kocha nashukuru kwa ujumbe huu, Mara nyingi nimekuwa nikiahirisha mambo ambayo yako ndani ya uwezo wangu kabisa. Baada ya hapo nakuwa kwenye hali ya kuumia kwa nini sikufanya wakati uwezo upo. Naimani ndani ya Kisima hiki nakwenda kubadili mtazamo.
LikeLike
Karibu sana,
Ni kweli wakati unaahirisha unakuwa na sababu ambazo zinaonekana ni sahihi kabisa.
Lakini baadaye unakuja kujutia kuahirisha huko.
Ndani ya KISIMA tunajifunza umuhimu wa kutekeleza kile tulichopanga, bila ya kujali nini kimetokea, na hii itaondoa kabisa tabia ya kuahirisha mambo.
LikeLike