“How much better is it to be known for doing well by many than for living extravagantly? How much more worthy than spending on sticks and stones is it to spend on people?”
—MUSONIUS RUFUS, LECTURES, 19.91.26–28
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KITU KINACHOVUTIA KWELI…
Kila mmoja wetu anapenda kufanya vitu vinavyovutia kwa wengine, vitu vinavyomfanya awe mtu wa kuvutia.
Lakini wengi tunafanya hivi kupitiw vitu vya nje.
Tunatumia gharama kubwa kutengeneza mwonekano wa kuvutia, kwa kuvaa mavazi ya ghali, vitu vya thamani na hata kuwa na mahitaji mengi ya anasa.
Ni kweli mambo hayo yanavutia, lakini yanakuacha ukiwa mtupu ndani yako, maana haijalishi ni kitu gani unacho, kama umekuwa nacho kwa ajili ya kuvutia, muda si mrefu kutakuwa na kingine cha kuvutia zaidi ya ulichonacho, hivyo utakazimika kuwa na hicho kipya pia.
Hivi ndivyo watu wanavyoingia kwenye utumwa mkubwa, hata kama wana fedha nyingi, wanajikuta zikiwasukuma kununua vitu vipya kila siku, siyo kwa sababu wana vihitaji, ila kwa sababu wanataka kuwavutia wengine.
Rafiki, kama lengo lako ni kuwavutia wengine, kama lengo ni kuwa mtu wa kuvutia, basi njia ya kweli na sahihi kufanya hivyo ni kupitia matendo yako mema na siyo kupitia vitu vya anasa unavyoweza kumiliki.
Kwa zama tunazoishi sasa, tuna uhaba mkuwa wa watu wenye tabia njema, watu wanaosimamia misingi sahihi na kufanya kilicho sahihi mara zote.
Kwa kuchagua kuwa mtu wa aina hiyo, utawavutia wengi, utakuwa mtu wa kuigwa na kuchukuliwa kama mfano na pia utakuwa huru na maisha yako.
Hutasumbuka kwamba uvae nini au uwe na nini ili watu wakuone, bali tabia zako mwenyewe, yale unayofanya yanakuwezesha kusimama na kuonekana kuliko wengine.
Chagua msingi sahihi wa kuendesha maisha yako, ishi msingi huo kila siku, kuwa na tabia njema na bora na utakuwa mtu wa kuvutia kwa wengi, huku pia ukibaki kuwa huru na maisha yako.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa mtu wa kuvutia kupitia misingi na tabia zako na siyo vitu vya nje.
#KuwaNaMsingiWaMaisha, #JulikanaKwaMatendoNaSiyoVitu, #WavutieWatuKwaUlivyoNaSiyoUlichonacho
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha