Rafiki yangu mpendwa,

Msiba wa mtu yeyote yule unaumiza sana, kwa sababu kila mtu ana watu wa muhimu kwake, ambao wanamtegemea kwa namna moja au nyingine.

Lakini msiba wa mtu ambaye amepiga hatua kubwa kimaisha, na ambaye ni mfano kwa wengi wanaotaka kupiga hatua, unaumiza watu wengi zaidi.

Hii ndiyo hali ambayo Watanzania na Dunia kwa ujumla, hasa wale wapenda mafanikio waliyonayo kwa sasa, baada ya kifo cha mfanyabiashara mkubwa Dr Reginald Mengi.

mengi

Huu pia ni msiba mkubwa kwa wasaka mafanikio wote, kwa sababu kanuni yetu wasaka mafanikio ni kwamba mtu yeyote aliyefanikiwa kwenye kitu chochote ana kitu kikubwa cha kutufundisha, kama tutakuwa tayari kujifunza. Msiba huu unatunyima nafasi ya kuendelea kujifunza kutoka kwa mfanyabiashara huyu aliyeweza kudumu kwenye biashara kwa zaidi ya miaka 40 na kwa mafanikio makubwa.

Lakini tuna bahati ya kipekee sana ya kuendelea kujifunza kutoka kwa Dr. Reginald Mengi kwa sababu ya kitu kimoja muhimu sana alichofanya wakati wa uhai wake.

Rafiki, maisha yetu hapa duniani ni mafupi sana, miaka 100 ijayo, kila mtu anayesoma hapa sasa hivi atakuwa ameshakufa, na wengine watakuwa wameshasahaulika kabisa.

Pamoja na maisha yetu kuwa mafupi, lakini pia tunasahaulika haraka sana baada ya kufariki kwetu. Kile kizazi ambacho kilitujua moja kwa moja kikishaondoka, kumbukumbu yetu inafutika kabisa hapa duniani.

Na hili halijali una mali au ushawishi kiasi gani, ukishakufa unasahaulika haraka sana. mali na utajiri vinasahaulika haraka sana baada ya mtu kufanikiwa, kwa sababu vinaacha kuwa chini ya mtu mmoja na kugawanywa kwa warithi. Na hata kama mtu una makampuni, bado kampuni siyo wewe, hivyo kama yataendelea kuwepo, yatakuwa na uongozi tofauti na kutengeneza maisha yao yenyewe.

Licha ya Dr Mengi kufariki, amefanya kitu ambacho kitamwezesha kuishi milele, kitu ambacho kitafanya vizazi vingi vijavyo vijue hapa Tanzania amewahi kuwepo mtu ambaye alianzia chini kabisa, kutoka familia duni, akienda shule peku na kuweza kufikia mafanikio makubwa sana kwenye biashara. Na siyo tu kupata mafanikio yake mwenyewe, bali pia kuwasaidia wengi wenye uhitaji.

Kitu alichofanya Dr Mengi ambacho kitamwezesha kuishi milele ni kuandika kitabu kilichoelezea maisha yake. Mwaka 2018, Dr Mengi alitoa kitabu kinachoelezea safari ya maisha yake ya mafanikio, kinachoitwa I CAN, I MUST, I WILL, The spirit of success.

mengi book

Niseme wazi, mimi ni mmoja wa watu ambao nilimjua Dr. Mengi vizuri baada ya kusoma kitabu chake hicho. Unajua jinsi jamii zetu zinavyopenda kutengeneza hadithi mbalimbali hasa kwa waliofanikiwa. Hivyo nilikuwa na hadithi nyingi kuhusu Dr Mengi, lakini niliposoma kitabu chake cha I CAN, nilipata picha tofauti sana, nilimwelewa vizuri Dr. Mengi, magumu aliyopitia kuanzia safari ya maisha duni ya familia, mpaka kupambana kwenda masomoni nchini Uingereza, kisha kurudi Tanzania, nchi ambayo ilikuwa kwenye mfumo wa ujamaa, na kuweza kupambana mpaka kuanzisha biashara. Na tena biashara alizoanzisha zilikuwa za kawaida sana, za kukidhi mahitaji ya kawaida ya watu, kama sabuni, dawa za meno, kalamu na kadhalika.

Kipindi ambacho Dr Mengi anaingia kwenye biashara kilikuwa kigumu sana kuliko kipindi kingine chochote, kwa sababu nchi bado ilikuwa haijaondoka kwenye mfumo wa ujamaa, hivyo Dr Mengi alionekana kama mtu mwenye tamaa na kuwaibia wengine. Lakini kutokukata kwake tamaa na kuendelea kusimamia ndoto zake, kuliweza kubadili kabisa mazingira na mtazamo wa Watanzania kuhusu uchumi huria.

Hii ndiyo zawadi bora kabisa ambayo Dr. Mengi ametuachia Watanzania na dunia kwa ujumla, zawadi ambayo itamfanya aendelee kuishi milele. Kila siku nitaendelea kujifunza kutoka kwake kwa kusoma kitabu chake, kila ninapokwama ninajua wapi pa kurudi na kujifunza kwa Dr. Mengi, kwa sababu kitabu chake ninacho. Na hata vizazi vijavyo, vinaweza kujifunza kutoka kwake, hata kama havitamwona akiwa hai.

Rafiki, lengo kuu la kukuandikia makala hii ni kukukumbusha umuhimu wa kuweka kwenye maandiko yale yote tunayoyajua, kwa sababu maandiko pekee ndiyo yatakayodumu milele hata baada ya sisi kuwa tumekufa.

Sisi Watanzania na Waafrika kwa ujumla tumekuwa wagumu sana kuweka yale tunayoyajua kwenye maandiko ukilinganisha na jamii nyingine. Tuna watu wengi sana ambao wamefanikiwa, ambao wamepambana sana kuanzia chini mpaka kufika kwenye kilele cha mafanikio, lakini hakuna sehemu ya uhakika kujifunza kuhusu wao. Zaidi ya zile hadithi za mtaani, ambazo kila mtu ana toleo lake, huyu atakuambia huyu alianza kuuza maandazi, mwingine atakuambia alianza kushona viatu, mwingine atasema alianza kutembeza kahawa na kadhalika. Watu hao wakifa, wanasahaulika haraka kama ambavyo mali zao zinasambaratika. Lakini kama wangekaa chini na kuandika machache kuhusu maisha yao, wanaacha nafasi nzuri ya wengine kujifunza kupitia wao, hata baada ya kuwa wamefariki.

SOMA; Zawadi Ya Vitabu Nane (08) Vya Mafanikio Vya Kuuanza Mwaka 2019 Na Kuufanya Uwe Mwaka Bora Sana Kwako.

Ni muhimu sana kwetu sisi kama wanamafanikio kuweka kwenye maandiko mchakato mzima wa maisha yetu, kila mtu ana kitu anachojua au ambacho ana uzoefu nacho, ambacho wengine wanaweza kujifunza pia.

Huwa nasema kila mtu ni kitabu kinachotembea, kwa sababu kila mtu ana maisha ya kipekee kabisa, ambayo hayafanani na ya mtu mwingine yeyote. Unapokufa kabla hujatoa kitabu kilichopo ndani yako, unakuwa umeidhulumu dunia, umeinyima isiendelee kujifunza kutoka kwako.

Na wala haihitaji uwe na mafanikio makubwa ndiyo uweze kuandika kitabu, kwa maisha yoyote uliyonayo, andika kitabu, hata kama hakitasomwa na watu wengi, lakini angalau watoto, wajukuu na vitukuu vyako vitakuja kusoma na kujifunza kutoka kwako. Una mengi ambayo yanaweza kuwasaidia wao, badala ya kuanzia sifuri, wanakuwa na mahali pa kuanzia.

Umeingia kwenye biashara na biashara ikafa? Vizuri, hebu weka kwenye maandishi kila ulichofanya kilichopelekea biashara kufa ili wengine wasirudie makosa yako.

Umeajiriwa kwa miaka mingi mpaka kustaafu na hakuna kikubwa ulichofanya, ukapokea mafao na ukapoteza fedha zote? Kuna kitu kikubwa cha kuwafundisha wengine ili wasirudie makosa kama yako.

Umeingia kwenye ndoa na mkaishia kuachana, hapo una kitu cha kuwafundisha wengine kuhusu ndoa na hatua za kuchukua ili kuepuka kuingia kwenye ndoa isiyo sahihi na kuzuia ndoa sahihi isivunjike.

Rafiki, vitu unavyojua, uzoefu ulionao, vipaji ulivyonavyo, uwezo mkubwa wa kipekee uliopo ndani yako pamoja na hatua ulizochukua kwenye maisha yako na matokeo uliyopata, yawe mazuri au mabaya, ni kitabu tosha. Weka mambo hayo kwenye maandishi, kuna watu utawasaidia sana kuliko unavyofikiri. Na hilo pia litakupa nafasi ya kuendelea kuishi hata baada ya kuwa umefariki.

Nikusihi sana rafiki yangu uandike kitabu katika maisha yako, na kwa kuwa hujui lini siku ya kifo chako, nakushauri sana uanze kuandika kitabu sasa. Anza kuandika kidogo kidogo, kuwa na kijitabu chako unachoandika mawazo na hatua zako unazochukua kila siku, na hicho kinaweza kunadilika na kuwa kitabu. Aliyekuwa mwanafalsafa na mtawala wa Roma Marcus Aurelius ameandika kitabu maarufu sana kinachoitwa Meditations, lakini hakukusudia kuandika kitabu. Yeye alikuwa anaandika kwenye kijitabu chake yale anayojifunza kila siku na jinsi ya kuwa bora zaidi, baada ya kufa, watu walikuta maandiko hayo ambayo aliyaweka kwa ajili yake, na kuona yanafaa kwa wengine kujifunza. Ni karibu miaka elfu mbili sasa tangu aondoke hapa duniani, lakini mpaka leo tunajifunza kupitia kitabu chake.

Njia nyingine unayoweza kutumia kuandika kitabu chako kidogo kidogo kila siku ni kuwa na blog ambapo unaweza kuwa unaandika makala kuhusu wewe, kazi zako, uzoefu wako na chochote unachopenda. Baadaye ukaja kugeuza blog hiyo kuwa kitabu.

Mimi kama kocha wako, nakupa nafasi ya kukusaidia kutengeneza mfumo bora kabisa wa kukuwezesha kuandika kitabu cha maisha yako hata kama hujui uanzie wapi. Kama utahitaji msaada kwenye hilo basi tuwasiliane kwa wasap namba 0717396253.

Kumbuka, kila mmoja wetu ni kitabu kinachotembea, njia pekee ya kuishi milele hata baada ya kufariki, ni kuweka kitabu hicho katika maandishi.

Mwisho nikusisitize kama mpaka sasa hujasoma kitabu cha Dr Reginald Mengi, kipate na ukisome sasa, utajifunza mengi na utapata hamasa ya kuchukua hatua ili kufanikiwa zaidi, kwa sababu kama alivyotuambia Mengi, UNAWEZA na UTAFANYA.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge