Tuseme labda kuna mahali unataka kuwahi, umeshachelewa na hivyo upo kwenye haraka ya kufika ndani ya muda, unasumbuka sana kuhakikisha unawahi. Unafikiri nani ametengeneza tatizo hilo? Vipi kama ungewahi mapema zaidi je ungekuwa kwenye masumbuko hayo?

Au pata picha una kazi ambayo inabidi uikamilishe kwa haraka, huna muda kabisa na kazi ni kubwa, je huna kumbukumbu kuna kipindi uliona una muda wa kutosha wa kufanya kazi hiyo, ukawa unazembea, mpaka pale muda umeisha ndiyo unaanza kukimbizana na kazi hiyo.

Unaona jinsi ambavyo wewe mwenyewe unajitengenezea kusumbuka?

Labda nikuongezee mfano mwingine, kuna mtu mlikubaliana naye kitu fulani, ukaweka mategemeo yako yote kwa mtu huyo kukamilisha kama alivyoahidi. Lakini mwisho wa siku mtu huyo anabadili mawazo au anashindwa kutekeleza upande wake na hivyo wewe unakwama. Hapo unalalamika na kulaumu jinsi ambavyo watu wengine hawajali. Lakini je unafikiri tatizo hapo ni la nani, yule mwingine au wewe?

Rafiki, kama utapata nafasi ya kuangalia na kutafakari kila kinachokusumbua, basi ukweli utakuja mbele yako kwamba chochote kinachokusumbua umekitengeneza wewe mwenyewe.

Unapokuwa na msongo wa mawazo, jua wewe ndiye umetengeneza msongo huo, hakuna chochote chenye nguvu ya kukupa wewe msongo.

Kama kuna mahali umechelewa, jua ni wewe mwenyewe umetengeneza kuchelewa huko, kama ungejipanga vizuri, ukaondoka mapema basi usingechelewa.

Kama kuna kazi ambayo unapaswa kuimaliza ndani ya muda mfupi, kumbuka ulikuwa na muda wakutosha wa kufanya kazi hiyo, lakini uliona muda ni mwingi na hivyo hukujisukuma sana.

Rafiki, unapoangalia masumbuko yako kwa mtazamo huu, unapata nafasi ya kuyapunguza zaidi baadaye. Inakuwa rahisi kwako kujikumbusha yaliyokusumbua siku za nyuma na kutokurudia tena. Pia inaondoa hali ya kupeleka lawama kwa wengine na kuziweka kwako, na hilo linakuwezesha kuchukua hatua sahihi.

Chochote kinachokusumbua, anza kujiangalia wewe mwenyewe, utaona jinsi ambavyo umekitengeneza mwenyewe na njia ya kutatua itakuwa wazi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha