Siku hizi kila mtu ametingwa, kila mtu yuko bize, kila mtu ana mambo mengi ya kufanya lakini muda alionao ni mchache.
Lakini swali muhimu sana unalopaswa kujiuliza kabla hujafurahia ubize wako ni je umetingwa kwa mambo yenye manufaa au kwa mambo yasiyo na manufaa.
Kwa sababu kwa walio wengi, wametingwa na mambo yasiyokuwa na manufaa kabisa.
Watu wanajipa madeni ya kufanya vitu ambavyo havina mchango wowote kwao kufikia mafanikio na kuwa na maisha bora.
Mfano siku ambayo hujapata nafasi ya kuingia kwenye mitandao, halafu ukapata muda mfupi na ukawa umetingwa kweli kuhakikisha unafuatilia kila kitu ili usipitwe na chochote, unaweza kuwa bize utakavyo, lakini jua hilo halina manufaa yoyote.
Unaweza kuwa na jumbe nyingi za kuwajibu watu waliokutumia, kwenye simu, barua pepe na hata mitandao ya kijamii, lakini hili halina manufaa makubwa kwako.
Unaweza kutingwa kweli kweli kuhakikisha unafanya yale ambayo wengine wanafanya, unakuwa na kile ambacho wengine wanacho, ili usiachwe nyuma, ili usionekane wa ajabu, lakini jua kutingwa huko hakutakuwa na manufaa yoyote kwako.
Kuanzia sasa, kabla hujajiruhusu kuingia kwenye ubize wowote, jipe muda mfupi wa kujiuliza maswali haya; je hili ndiyo jambo muhimu zaidi kwangu kufanya? Je haya ndiyo matumizi bora kabisa ya muda mchache ambao ninao hapa duniani? Je kama leo ingekuwa siku yangu ya mwisho hapa duniani, ningefanya kitu hiki ninachotaka kufanya sasa?
Maswali hayo yanakuwezesha kupiga umuhimu wa chochote unachotaka kufanya na kukupa picha sahihi. Hivyo hata kama utaamua kuendelea kufanya kitu hicho, angalau unakuwa unajua kwamba unapoteza muda au unawekeza muda.
Kumbuka muda wako na nguvu zako ni sawa na fedha zako, unaweza kuziwekeza kwa kufanya mambo yenye manufaa na yatakayokulipa zaidi baadaye au ukavitumia hovyo kwa kufanya mambo yasiyo na manufaa.
Uchaguzi ni wako mwenyewe kwa kuwa maisha ni yako. Ni imani yangu utachagua kilicho bora.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,