Kila mmoja wetu kuna wakati anajikuta njia panda, asijue ni kipi cha kufanya, hatua ipi ya kuchukua katika mengi anayoweza kufanya au kwa kuwa hakuna anachoweza kufanya kabisa.

Nyakati kama hizi ndiyo zinawatofautisha wale wanaofanikiwa na wanaoshindwa.

Wale wanaoshindwa huwa wanakubali kwamba hawajui au hakuna hatua wanayoweza kuchukua, hivyo hawachukui hatua yoyote. Na kama unavyojua, kama huchukui hatua yoyote hakuna chochote kinachobadilika, utaendelea kubaki pale ulipo sasa.

Wale wanaofanikiwa, huwa wanachukua hatua katika hali kama hizi, na hatua gani wanachukua ni yoyote ambayo inafaa kuchukua katika wakati kama huo. Kwenye kila hali ambayo mtu yupo njia panda, labda kwa mengi anayoweza kufanya au kwa kutokuwa na la kufanya kabisa wanaofanikiwa wanajiuliza ni hatua ipi sahihi ya kuchukua katika hali kama hiyo na kisha wanachukua hatua hiyo, hata kama ni ndogo sana.

Hivi ndivyo unapaswa kuyaendesha maisha yako, usikubali kukwama kwenye njia panda ya kutokujua hatua gani uchukue, unapojikuta kwenye hali kama hiyo jiulize swali moja, ni hatua ipi unayoweza kuchukua kwa pale ulipo, kipi sahihi kufanya kwenye wakati kama huo.

Kuchukua hatua ni muhimu kuliko kutokuchukua hatua kabisa, matokeo tofauti yanakuja kwa kuchukua hatua.

Kuchukua hatua zisizo sahihi ni bora kuliko kutokuchukua hatua kabisa. Kwa kuchukua hatua zisizo sahihi utajifunza kwa matokeo utakayopata, wakati kwa kutochukua hatua hutajifunza kabisa.

Kila unapokwama rafiki, jiulize ni hatua gani unaweza kuchukua, na pale unapoanza kuchukua hatua yoyote ile, hali ya kukwama inaondoka kabisa yenyewe.

Kuwa mtu wa kuchukua hatua na utaweza kupiga hatua kubwa sana kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha