Katika viumbe hai wote ambao tuko hapa duniani, sisi binadamu ndiyo tumepewa uwezo mkubwa wa kufikiri, kupanga na kufanya maamuzi. Wanyama wengine wote wanaendesha maisha yao kwa msukumo wa kupata wanachotaka au kuepuka hatari.

Simba akiwa na njaa atawinda swala, na hataacha kuwinda mpaka apate chakula. Swala akimwona simba atakimbia kuokoa maisha yake, na hataacha kukimbia mpaka awe salama.

Hutamkuta simba amekaa ana mawazo kwamba kesho atapata wapi swala au kama swala wataendelea kupatikana miaka ijayo. Na pia hutamkuta swala akifikiria ni saa ngapi simba atatokea na kuanza kufikiria ni jinsi gani maisha ni magumu kwa sababu simba wamekuwa wengi.

Simba wanaendelea na maisha yao na swala wanaendelea na maisha yao, hakuna anayehofia kuhusu maisha ya sasa au ya baadaye.

Lakini sisi binadamu, sisi ambao tumepewa uwezo mkubwa wa kufikiri, kupanga na kuamua ndiyo tunateseka sana na uwezo huu tulionao. Kwa sababu tunatumia uwezo huu siyo kutengeneza maisha bora, bali kutengeneza hofu kama mambo hayatakwenda kama ulivyopanga.

Hapa ndipo mtu anahofia kama akipoteza kazi aliyonayo sasa maisha yatakwendaje, hofu hii inamnyima uhuru wa maisha yake na kufanya kazi kwa hofu na siyo kwa uhuru na ubunifu.

Hapa ndipo mtu anahofia kama biashara aliyonayo itashindwa maisha yake yatakwendaje, hivyo anakuwa na hofu ya kujaribu vipya, anaendelea kufanya biashara kwa mazoea hata kama haimpi faida kubwa.

Rafiki, unachopaswa kujua ni kwamba dunia ni kubwa kuliko hofu zako, chochote ambacho unahofia kupoteza, jua dunia inaweza kukupatia kwa wingi kadiri utakavyo. Unachohitaji ni kuwa na mtazamo wa utele, mtazamo wa mambo kuwezekana na usiwe na uhaba.

Dunia ni kubwa kuliko hofu zako, ukipoteza chochote ulichonacho sasa, dunia itakupa vitu vingi kuliko ulivyotegemea. Ni mara ngapi umepoteza kitu ambacho ulifikiri ni muhimu na hutapata tena kama hicho, lakini baadaye ukapata kilicho bora zaidi?

Labda ulifukuzwa kazi uliyoitegemea sana, na hapo ukapata kazi nyingine bora zaidi au ukaweza kuingia kwenye biashara ambayo imekukomboa zaidi. Au ni mahusiano yalivunjika, ukajiambia hutapata mahusiano mengine kama yale, lakini ukaja kupata mahusiano bora zaidi.

Kumbuka hili rafiki, dunia ni kubwa kuliko hofu zako, dunia ina mengi kuliko unavyofikiri wewe. Hivyo jukumu lako ni kuyaishi maisha yako, kwa uhuru na bila ya hofu, dunia haitakosa cha kukupa, wakati ambapo unakitaka.

Kama ambavyo swala na simba wanaendelea na maisha yao, na wewe pia endelea na maisha yako na achana na hofu zozote zinazokujia. Iamini dunia, ina uwezo wa kukidhi mahitaji yako yote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha