Huwa tunaamini sana watu kwa kile wanachotuambia, hata kama wanatudanganya. Tunaamini watu wanatuambia ukweli, hasa pale wanapojiamini katika kusema wanachotuambia.

Na wale wenye nia ya kutudanganya, huwa wana mbinu za kutufanya tuamini wanachotuambia. Kama usipokuwa makini, ni rahisi sana kuingia kwenye kudanganywa au kutapeliwa na wengine.

Njia pekee ya kujua ukweli kuhusu kile ambacho mtu anakuambia ni kusikia kile ambacho hakisemwi.

Maana yake ni kutumia lugha ya mwili ambayo inasema mengi kuliko yale yanayosemwa kwa maneno. Mtu anaweza kudanganya kwa mdomo, lakini mikono yake itaeleza ukweli ulivyo, au macho yake yatakuwa yanaonesha wazi kabisa ukweli uko wapi.

Sikia kile ambacho hakisemwi kwa kuweka umakini kwa mtu unayezungumza naye, kwa kusikiliza siyo tu kwa masikio, bali pia kwa macho, kwa kuangalia vitendo ambavyo mtu anafanya wakati anaongea.

Angalia namna mtu huyo anavyojiamini kwenye kile ambacho anazungumzia, kutokujiamini au kujiamini kupita kiasi ni kiashiria kuna kitu kinafichwa.

Kuuliza maswali pia kunakupa nafasi ya kujua ukweli wa kile ambacho mtu anakuuliza. Mfano unapouliza swali ambalo linahitaji jibu rahisi na mtu akakwepa kujibu swali hilo na kutengeneza swali jingine ambalo analijibu, kuna uwezekano mkubwa wa kuwa anadanganya.

Pia kumpa mtu ushahidi unaopingana na kile anachosema, hata kama ni w akutunga na kuangalia jinsi ambavyo anapokea ushahidi huo, kutakuonesha kama mtu huyo anasema ukweli au uongo.

Zipo njia nyingi za kuepuka kudanganywa, lakini ya kwanza ni kuwa makini katika kusikiliza kila kinachosemwa na kisichosemwa, na kuangalia alama za mwili ambazo mtu anatumia.

Hili limekuwa zoezi gumu siku hizi, kwa sababu hakuna tena mtu anayesikiliza kwa umakini, mtu anaongea na anayepaswa kusikiliza yuko bize kwenye simu na mitandao ya kijamii, hivyo haweki umakini kwa yule anayeongea na hapo ni rahisi kudanganywa na kutapeliwa.

Kama hutaki kudanganywa au kutapeliwa, weka umakini mkubwa kwenye kusikiliza na kuangalia alama za mwili za mtu. Ni rahisi kuona uongo au utapeli unapokuwa na umakini mkubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha