Kufikiri chanya kumekuwa kunatumika vibaya na wengi. Wengi wanaamini kwamba ili ufanikiwe unachohitaji ni kufikiri chanya muda wote, kuwa na mategemeo chanya kwenye maisha hata pale unapopata matokeo ambayo siyo mazuri.
Ni kweli kufikiri chanya na kuwa na mategemeo chanya kwenye maisha kunasaidia kuliko kuwa na fikra hasi na mategemeo hasi. Kwa sababu unapokuwa na mategemeo hasi, hupati hata msukumo wa kuchukua hatua. Utawezaje kupata msukumo wa kufanya kitu ambacho una uhakika kabisa kwamba unakwenda kushindwa?
Lakini unapokuwa na mategemeo chanya, unapokuwa na fikra chanya, ni rahisi kwako kujipa moyo na kupata nguvu ya kujaribu vitu vipya na vikubwa, ambavyo vinawakatisha wengi tamaa.
Lakini kufikiri na kutegemea matokeo chanya muda wote hakupi maandalizi bora kabisa ya kupata unachotaka.
Badala yake unahitaji kuwa na maandalizi ya matokeo hasi. Pamoja na kutegemea kwamba utapata matokeo mazuri, lakini pia pata picha kwamba umepata matokeo mabaya, matokeo ambayo hukutegemea kabisa kuyapata. Na jiulize ni hatua gani utachukua kwenye matokeo kama hayo.
Unapojipa picha ya matokeo mabaya kuliko unavyotegemea, unakuwa unajipa uhalisia wa dunia. Kwa sababu sisi huwa tunapanga mambo yetu, lakini dunia nayo ina mipango yake. Sasa kufikiri kwamba kila wakati utapata unachotaka ni kujidanganya, hakuna mtu yeyote ambaye amewahi kupata kila anachotaka kila mara anapokitaka. Kila mtu kwa namna moja au nyingine amekuwa anapata matokeo tofauti na alivyotegemea.
Hivyo kujipa picha ya tofauti ni kuwa na maandalizi ya kuupokea uhalisia. Chochote kinachotokea hakikushangazi wala kukutisha, hujiambii imekuwaje matokeo yakawa hivi. Badala yake unapokea matokeo hayo huku tayari ukiwa na mpango mbadala wa kuchukua.
Tegemea matokeo chanya, lakini pia jiandae kwa matokeo hasi kwa kuwa na maandalizi ya matokeo ambayo hutegemei. Huo ndiyo uhalisia wa maisha, kama hutaki kupata mshtuko na kukata tamaa, basi kubali kwamba siyo mara zote utapata kila unachotaka.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,