“Well-being is realized by small steps, but is truly no small thing.”
—ZENO, QUOTED IN DIOGENES LAERTIUS, LIVES OF THE EMINENT PHILOSOPHERS, 7.1.26
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana tuliyoiona leo.
Ni nafasi bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari JALI VITU VIDOGO VIDOGO…
Mafanikio makubwa kwenye maisha hayatokei kama ajali au bahati.
Badala yake ni matokeo ya vitu vidogo vidogo na hatua ndogo ndogo tunazopiga kila siku.
Vitu ambavyo havina uzito kabisa, vitu ambavyo hakuna anayekuangalia ukifanya, vitu ambavyo ni rahisi kuvipuuza na kuviacha, ndiyo hivyo hivyo vinavyokufikisha kwenye mafanikio makubwa.
Vitu vidogo vidogo kama kuamka mapema, kutandika kitanda chako, kuandika malengo yako, kufanya mazoezi, kujifunza, kuepuka njia za mkato na kuifanya kazi yako, unaweza usione umuhimu wake wakati unavifanya leo.
Lakini endelea kuvifanya kila siku na utashangaa kuona vinajenga maisha ya tofauti kabisa kwako.
Matokeo ya pamoja ya hatuw hizi ndogo ndogo unazorudia kila siku ni makubwa sana, na ndiyo yanaleta mabadiliko makubwa kwenye maisha.
Jali vitu vidogo vidogo, vipe nafasi na kuvifanya kila siku na vitakupa matokeo makubwa sana.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujali na kuweka kipaumbele kwenye mambo madogo madogo yanayojenga maisha yako.
#MafanikioYanaanzaNaHatuaNdogo, #JaliVituVidogoVidogo, #MafanikioSiyoAjali
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha