Safari ya mafanikio ni safari ngumu sana kwa wengi kwa sababu inahitaji imani zaidi na kujidanganya pia.
Kwa kuwa wengi hawajiamini wao wenyewe, safari hii inakuwa ngumu kwao.
Na pia kwa kuwa wengi hawapo tayari kujidanganya (kwa nia nzuri) basi wanashindwa kabisa kupiga hatua.
Aliyekuwa bondia bora kabisa duniani Mohamad Ali alisema kwamba alianza kujiita bondia bora kabla hata hajawa bora.
Mwigizaji maarufu Jim Carry alijiandikia cheki ya dola milioni 10 kama malipo aliyopokea kwa huduma za uigizaji, akiwa hana hata senti moja, na miaka kumi baadaye akapokea cheki ya kiasi hicho cha fedha kwa huduma zake za uigizaji.
Ipo mifano mingi ya watu waliofanikiwa, ambao walianzia chini kabisa lakini hawakuwa wanajiona wapo chini, ndani yao walijiona wapo juu na wameshafanikiwa, na hilo liliwasukuma kufanikiwa zaidi.
Ndiyo maana nakuambia unahitaji kujidanganya ili ufanikiwe. Unahitaji kukataa uhalisia wako wa sasa, kujiona kama mtu ambaye tayari umeshafanikiwa na unachosubiria ni kukabidhiwa tu mafanikio yako.
Kwa kujiona hivyo kama mtu ambaye tayari umeshafanikiwa, unabadili kabisa maisha yako na unakuwa kwenye nafasi ya kufanikiwa.
Lakini hili linakuwa gumu kwa wengi, kwa sababu huwa wanaanza kuwafikiria wengine kabla ya kujifikiria wao binafsi. Wanafikiria wengine watawachukuliaje pale watakapokuwa wanajiambia wameshafanikiwa wakati kwa nje bado hawaonekani kufanikiwa?
Unafikiria utawaambiaje watu wewe ni tajiri wakati hata fedha ya kula huna?
Rafiki, hilo lisikupe wasiwasi hata kidogo, usisumbuke na wengine wanakuchukuliaje, wewe jiite vile unavyotaka kuwa, jione kama mtu ambaye tayari umeshafika unakotaka kufika, kisha endesha maisha yako kwa misingi ya kuwa na unachotaka kuwa nacho na kwa hakika utafanikiwa.
Kujiamini wewe mwenyewe na kuwa tayari kujidanganya ni vitu vigumu sana kwa wengi kufanya, hakikisha unavifanya kama unataka kufanikiwa kweli.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante kocha, njia ya mafanikio ni safari ndefu na ngumu, nitatumia kila aina ya mafunzo na Elimu yako ili kujiletea Mabadiliko binafsi na pengine wanaonizungaka.
LikeLike
Vizuri Beatus
LikeLike