Rafiki yangu mpendwa,

Kama mzazi au babu/bibi yako aliyeishi na kufariki miaka ya 1980 atafufuliwa leo na kuona yanayoendelea duniani, atashangazwa sana.

Kwamba anaweza kuwasiliana na mtu aliyepo popote duniani kwa urahisi na gharama ndogo, kwamba anaweza kupata taarifa za chochote kinachoendelea duniani hapo hapo na kwamba anaweza kufanya biashara na mtu yeyote kwa mawasiliano rahisi ya mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii ni kitu ambacho kingemshangaza sana.

Kwa sababu miaka aliyoishi yeye, hakuna mtu aliyewahi kudhani kwamba haya yote yangewezekana. Hivyo kama mtu huyo akiletwa duniani sasa, atategemea kuona watu wenye furaha sana kwa sababu mitandao hii imerahisisha mawasiliano na ufanyaji wa kazi na hata biashara.

Lakini kama mtu huyu atapewa muda mchache wa kuwafuatilia wanaotumia mitandao hii ya kijamii, atagundua kwamba alichodhani siyo sahihi. Alichodhani kwamba watu watakuwa na furaha sana kwa kurahisishwa kwa mawasiliano siyo sahihi. Kwani atagundua watu hawana furaha kama wanavyopaswa kuwa nayo na hofu na wasiwasi ni mkubwa zaidi kwa watumiaji wa mitandao hii kuliko ilivyokuwa kwenye maisha yao ambapo hawakuwa na mitandao hii ya kijamii.

Sasa hapa mtu atapatwa na mshangao, kwa kushindwa kuelewa kwa nini watu hawana furaha wakati mawasiliano yamerahisishwa zaidi kwao? Hii ni sawa na kukuta mtu ana njaa wakati amezungukwa na chakula.

social media addiction

Na hapa ndipo tunakwenda kugundua kwamba mitandao ya kijamii, pamoja na manufaa yake mengi, imekuja na hatari moja; inaharibu akili za watu. Mitandao ya kijamii inawafanya watu wengi kukosa furaha, kuwa wapweke, kuwa na hofu, kushindwa kutengeneza mahusiano imara na kushindwa kujitambua wao wenyewe.

Haya ni matatizo makubwa sana ambayo watumiaji wengi wa mitandao hii hawana uelewa nayo, wanakazana kuitumia bila ya kujua madhara yake, na kinachotokea ni maisha yao yanakuwa mabovu lakini hawajui nini kinasababisha maisha yao yawe mabovu.

Mwandishi Cal Newport kwenye kitabu chake kinachoitwa DIGITAL MINIMALISM ameeleza kwa kina changamoto kubwa za mitandao hii ya kijamii, na kuja na falsafa bora ya matumizi ya mitandao hii, ambayo itamsaidia mtumiaji kuondokana na hatari na hasara za mitandao ya kijamii.

Katika kitabu chake, Cal ameeleza kwa kina jinsi ambavyo mitandao ya kijamii inaharibu akili za watumiaji wa mitandao hiyo.

Kitu kikubwa kabisa ambacho mitandao hii inafanya na kinapelekea kuharibu akili ni KUMYIMA MTUMIAJI MUDA WA KUWA PEKE YAKE, dhana ambayo kwenye kitabu Cal ameiita Solitude Deprivation.

UMUHIMU WA KUWA NA MUDA WA PEKE YAKO.

Tangu enzi na enzi, binadamu wamekuwa wakipata maono makubwa na ya tofauti, kupata suluhisho la matatizo makubwa na hata kujitambua wao wenyewe baada ya kupata muda wa kuwa peke yao.

Kuanzia wanafalsafa, wanasayansi, watu wa imani na hata viongozi, waliweza kufanya makubwa waliyofanya baada ya kupata muda wa kuwa peke yao, na mawazo yao, na kuondokana kabisa na usumbufu wa wengine.

Tukianzia kwa watu wa imani, soma historia za viongozi wote wa kiimani, kuanzia Yesu, Mohamad, Budha na wengineo, walibadilika kutoka maisha ya kawaida na kuwa watu wa imani baada ya kupata muda wa kuwa peke yao. Yesu alienda milimani kufunga na kuwa peke yake, kadhalika Muhamad na hata Budha, pamoja na kukulia kwenye maisha ya kifahari, hakupata uamsho mpaka pale alipoenda porini na kupata muda wa kukaa peke yake.

Tukija kwa wanafalsafa na waandishi, waliweza kuja na mawazo yao bora kuhusu maisha baada ya kupata muda wa kukaa peke yao. Wanafalsafa na waandishi wengi waliweza kuja na njia bora za kuishi na suluhisho la matatizo mbalimbali baada ya kujifungia wenyewe kwa kipindi fulani. Mwandishi na mwanafalsafa Hendry David Thoreau ameelea umuhimu wa kuwa na muda wa peke yako katika kitabu chake maarufu kinachoitwa WALDEN. Kupitia kitabu hicho, Thoreau alifanya zoezi la kuondoka kwenye jamii na kwenda kujenga kibanda msituni ambapo aliishi peke yake kwa zaidi ya mwaka. Ni kupitia muda huu wa kuwa peke yake ndiyo aliweza kuja na mawazo bora sana ya jinsi ya kuwa na maisha bora.

Wanasayansi ndiyo wanategemea zaidi muda wa peke yao kuja na ugunduzi na uvumbuzi wa vitu mbalimbali. Tunaelezwa kwamba mwanasayansi Newton aligundua sheria ya mvutano akiwa amekaa peke yake chini ya mti na kuangalia tunda likianguka. Kadhalika mwanasayansi Albert Einstein aliweza kuja na kanuni bora kabisa za kisayansi kwa kuwa na muda wa kukaa peke yake.

Na hata viongozi bora kuwahi kutokea duniani, ambao waliweza kuendesha nchi zao na kuvuka magumu na changamoto mbalimbali, walihakikisha wanakuwa na muda wa kukaa peke yao.

SOMA; Siri Hii Itakusaidia Kuondokana Na Msongo Wa Mawazo Wa Kukosa Muda Katika Ulimwengu Huu Wa Utandawazi.

FAIDA ZA MUDA WA KUWA PEKE YAKO.

Kama ambavyo tumejifunza hapo juu, watu waliofanya mambo makubwa hapa duniani, wote walikuwa na muda wa kuwa peke yao. Hakuna yeyote aliyefanya makubwa ambaye muda wote walikuwa amezungukwa na usumbufu.

Zifuatazo ni faida ambazo kila mtu anaweza kuzipata kwa kutenga muda wa kuwa peke yake na mawazo yake.

  1. Kupata mawazo mapya.

Unapokaa peke yako, hakuna usumbufu au kelele zozote zinazoingia kwenye akili yako, hivyo akili hiyo inaweza kufikiri na kuja na mawazo mapya. Hivi ndivyo watu wamekuwa wakigundua vitu vipya, kwa sababu akili zao zinakuwa hazijatingwa.

  1. Kujitambua wewe mwenyewe.

Huwezi kujitambua wewe mwenyewe bila ya kupata muda wa kuwa peke yako. Unapopata muda wa kuwa peke yako ni rahisi kujihoji na kujitathmini kwa kila unalofanya na matokeo unayopata na kuona madhaifu yako na uimara wako.

  1. Mahusiano bora na wengine.

Huwezi kujua umuhimu wa wengine kwenye maisha yako kama hupati muda wa kuwa peke yako. Ni kupitia muda wa upweke ndiyo unajua umuhimu wa wengine kwenye maisha yako. Pia unapojitambua wewe mwenyewe, mahusiano yako na wengine yanakuwa bora.

  1. Kutatua matatizo magumu.

Matatizo magumu yanahitaji utulivu mkubwa katika kuyatatua, hivyo kuwa na muda wa peke yako ni muhimu sana katika kuyaelewa na kuyatatua matatizo magumu yanayokukabili.

  1. Kudhibiti hisia zako.

Hisia zimekuwa changamoto kwa wengi, matatizo mengi ambayo watu wanakutana nayo kwenye maisha yanaanza na hisia, hasa pale ambapo zinashindwa kudhibitiwa. Unapopata muda wa kuwa peke yako ndipo unaweza kuzikagua hisia zako na kujua kichocheo chake na jinsi ya kuzidhibiti.

JINSI MITANDAO YA KIJAMII INAVYOKUNYIMA MUDA WA KUWA PEKE YAKO.

Mitandao ya kijamii inamnyima mtu muda wa kuwa peka yake kwa sababu ya utahisi wa kuikifikia. Ukichukua mfano, kabla ya ujio wa simu janja, watu hawakuwa na mawasiliano ya muda wote wa siku. Hivyo kama upo kwenye kazi na huna cha kufanya, ulilazimika kukaa peke yako na mawazo yako. Au kama uko na watu wengine, ulilazimika kujihusisha na mazungumzo na watu hao, kwa sababu hukuwa na kitu kingine cha kufanya.

Kwa kifupi, kabla ya ujio wa simu janja na mitandao ya kijamii, maisha yako ya kawaida yalikuwa yanakulazimisha uwe na muda wako peke yako, na hapo ulipata nafasi ya kuyatafakari maisha yako na hata kuja na mawazo mazuri na suluhisho la changamoto mbalimbali.

Lakini baada ya kuja kwa simu janja na mitandao ya kijamii, mambo yamebadilika.

Kwanza urahisi wa kubeba simu hizi umefanya tuweze kuwa nazo kwa masaa 24 ya siku na siku saba za wiki. Hatuwezi hata kwenda kitandani na kuacha simu zetu, ni kama zimegandishwa kwenye mikono yetu. Siku hizi hata mgeni akifika nyumbani, kitu cha kwanza ni kuchaji simu yake, ili isiishe chaji akapitwa na dunia.

Pili kuwa na simu hizi muda wote zinaondoa kabisa ile nafasi ya mtu kuwa peke yako na mawazo yako. Ukiwa kwenye kazi na huna cha kufanya nini kinaendelea? Unajiambia wacha niingie facebook au instagram mara moja, na unakuja kustuka nusu saa baadaye unazidi kushuka tu kuangalia maisha ya wengine yanaendeleaje.

Tatu simu janja na mitandao ya kijamii inatunyima kabisa ile hali ya uchoshi, na hivyo mtu anapochoka kidogo kwenye kitu chochote anachofanya, badala ya kukaa na kufikiri, anakimbilia kwenye mitandao ya kijamii.

Nne mitandao hii inatupa njia rahisi ya kutoroka matatizo au changamoto zetu. Mtu anakabiliwa na changamoto fulani kwenye maisha yake, badala ya kuitatua yeye anakimbilia kwenye kitandao ya kijamii kulalamika kuhusu changamoto hiyo.

Tano mitandao hii inatulaghai kwamba unaweza kuchungulia mara moja na kutoka, lakini hakuna anayeweza kufanya hivyo. Kila unapochungulia unaletewa vitu vya kuvutia zaidi na kujikuta umetumia muda mwingi kuliko ulivyopanga.

Kwa njia hizi, simu janja na mitandao ya kijamii imetunyima kabisa nafasi ya kukaa peke yetu na mawazo yetu. Imekuwa usumbufu mkubwa kwetu ambao umetuganda na hatupati kabisa muda wa upweke ambao ni muhimu kwa ukuaji wetu kama binadamu.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kuondokana Na Matumizi Mabaya Ya Mtandao Wa Intaneti Na Kutumia Vizuri Muda Wako Kujiongezea Kipato.

HASARA KUBWA TUNAYOPATA KWA MATUMIZI YASIYO NA UKOMO YA MITANDAO YA KIJAMII.

Hasara kubwa kabisa ya mitandao ya kijamii ni kumnyima mtu muda wa kuwa peke yake. Na hili ndiyo limezalisha matatizo mengi kwa watu. Tafiti zinaonesha vijana wengi ambao wamekulia kwenye zama hizi za mitandao ya kijamii wana matatizo mengi ya kiakili, hasa wasiwasi na msongo ambao unatokana na matumizi yaliyopitiliza ya mitandao hii. Wasiwasi na msongo huu unatokana na wao kujilinganisha na wengine kupitia picha ambazo zinawekwa kwenye mitandao hii.

Pia vijana hao waliokulia kwenye mitandao hii ya kijamii, ni wabovu kwenye kudhibiti hisia zao, wakikutana na tatizo kidogo badala ya kukaa chini na kufikiria jinsi ya kulitatua, wanakimbilia kuweka mitandaoni. Mfano mahusiano yanakwenda vibaya au yamevunjika, badala ya watu hawa kukaa chini na kuona jinsi ya kuboresha mahusiano yao, wanakimbilia mitandaoni kuwalaumu wenza wao kwa kuvunjika kwa mahusiano yao.

Lakini pia ubora wa mahusiano baina ya mtu na mtu umekuwwa mdogo sana kwenye zama hizi za mitandao ya kijamii. Watu ambao hawajawahi kukutana kwa miaka wanaweza kupata nafasi ya kukutana, lakini baada ya muda mfupi wa kusalimiana, kila mtu anaanza kuangalia simu yake na kumsahau yule aliyenaye pale alipo. Hili linafanya mahusiano kuwa mabovu na watu kushindwa kushirikiana vizuri.

HATUA TATU ZA KUCHUKUA ILI KURUDISHA MUDA WA KUWA PEKE YAKO NA KUONDOKANA NA MADHARA YA MITANDAO YA KIJAMII.

Rafiki, unahitaji muda wa kuwa peke yako na mawazo yako, ni kwa njia hii ndiyo unaweza kuwa mtu bora, kufanya kazi ya tofauti na hata kuboresha mahusiano yako.

Kwa kuwa tumeshaona jinsi ambavyo simu zetu zimetuganda na mitandao hii kuwa sehemu ya maisha yetu, tunahitaji kuchukua hatua za makusudi za kulinda muda wetu wa kuwa peke yetu.

Mwandishi Cal Newport kwenye kitabu chake cha DIGITAL MINIMALISM ametushirikisha hatua tatu za kuchukua ili kulinda muda wa kuwa peke yetu usiharibiwe na simu na mitandao ya kijamii.

HATUA YA KWAZA; TENGA MUDA WA KUKAA MBALI NA SIMU YAKO.

Haijalishi unafanya kazi au biashara ya aina gani, kama inakubidi uwe na simu yako kwa masaa 24 kila siku na siku zote 7 za wiki basi huna maisha. Unaweza kuwa na kila kitu unachofikiri unacho, lakini huna maisha, na hilo ni baya kuliko mengine yote.

Unapaswa kutenga muda wa kukaa mbali na simu yako, ili upate muda wa kukaa peke yako na mawazo yako, kitu ambacho kitakusaidia kufikiri tofauti na kuja na vitu vya tofauti.

Baadhi ya fursa unazoweza kutumia kukaa mbali na simu yako.

  1. Acha simu yako nyumbani unapokwenda kazini au kwenye matembezi.
  2. Tenga masaa ya siku yako ambayo hutatumia simu kabisa, labda asubuhi na mapema, au muda wa kazi, au muda wa jioni unapokuwa na familia.
  3. Usianze siku yako kwa kuangalia simu au mitandao ya kijamii, amka asubuhi na mapema na angalau masaa mawili ya mwanzo baada ya kuamka usiguse kabisa simu yako.
  4. Usilale na simu kitandani, wala isikae eneo la karibu ambapo ikiita utaweza kuifikia.
  5. Tenga muda wa kutembelea mitandao ya kijamii, ile ambayo ni muhimu na isiyo muhimu kwako ondoa kabisa kwenye simu yako.
  6. Siku moja kwa wiki ifanye siku ya kutokuingia kwenye mitandao kabisa, siku ambayo matumizi ya simu na vitu vingine vya kidijitali kuwa madogo.

Kwa kutumia njia hizi na nyingine unazoweza kuja nazo kwa kutafakari hili kwa kina, kila siku utaweza kulinda muda wa kuwa peke yako na kuzia simu na mitandao ya kijamii kutawala maisha yako.

HATUA YA PILI; KUWA NA MATEMBEZI MAREFU.

Hatua ya pili unayoweza kuchukua ya kulinda muda wa kuwa peke yako ni kujiwekea utaratibu wa kuwa na matembezi marefu peke yako. Na itapendeza kama matembezi haya utayafanya kwenye asili, ukiwa peke yako.

Kama unakaa karibu na milima au msitu, unaweza kufanya matembezi yako kwenye maeneo hayo. Pia kama unakaa karibu na ufukwe, unaweza kufanya matembezi yako kwenye ufukwe.

Kwa kufanya matembezi haya peke yako, kwenye eneo la asili, unaipa akili yako nafasi ya kuwa peke yake na mawazo yake na hapo utaweza kufikiri tofauti na kuja na vitu tofauti pia.

Tenga muda wa kufanya matembezi haya kila siku au kila wiki na utaweza kuona manufaa yake kwenye maisha yako.

HATUA YA TATU; JIANDIKIE BARUA.

Hatua nyingine muhimu ya kuchukua ili kuwa na muda wako peke yako ni kujiandikia barua wewe mwenyewe.

Tunaposema kuwa na muda wa peke yako, maana yake unakuwa wewe na mawazo yako tu, husikilizi mtu mwingine na wala husomi chochote, kwa kifupi huingizi kitu chochote kipya kwenye akili yako, bali unatumia kile ambacho tayari kipo.

Zoezi la kuandika ni moja ya mazoezi yanayokuwezesha kutumia kilichopo ndani ya akili yako. Unapokuwa unaandika, unajilazimisha kufikiri hasa na hapo huwezi kuruhusu usumbufu wowote wa nje. Kuandika pia kunaulazimisha kudhibiti mawazo yako badala ya kuyaacha yazurure hovyo.

Utaratibu wa kujiandikia barua ni mzuri kwa sababu unakulazimisha ufikiri kwa kina kuhusu kile unachopitia kwenye maisha yako. Na hapa unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kupata majibu ya changamoto mbalimbali.

Unapokuwa na changamoto au magumu yoyote unayopitia kwenye maisha, tenga muda na jiandikie wewe barua. Andika barua hiyo kama vile unamwandikia mtu mwingine na utashangaa jinsi ambavyo akili yako itakupa hatua sahihi za kuchukua.

Kuwa na kijitabu ambacho kila siku au pale unapokwama unakaa chini na kuandika. Weka utaratibu wa kuandika yale unayopitia kwenye kila siku yako. Jipe zoezi la kufikiria na kuandika njia za kutatua changamoto unayopitia, na kwa namna hii akili yako itafanya kazi zaidi.

Mfano chukua changamoto kubwa inayokusumbua, kisha andika kwenye karatasi njia 20 za kutatua changamoto hiyo. Kama changamoto ni kipato, kwenye kijitabu au karatasi andika NJIA 20 ZA KUONGEZA KIPATO CHANGU, kisha jifungie mahali na fikiria mpaka ujaze majibu 20. Majibu 10 ya mwanzo yatakuwa rahisi, lakini 10 ya mwisho yatakuwa magumu, na hayo ndiyo yatakayokupa suluhisho sahihi kwako kufanyia kazi.

Rafiki yangu mpendwa, mitandao ya kijamii ina manufaa makubwa kwetu, lakini pia ina hasara kubwa mno kama mtu hutakuwa makini na kuitumia kwatahadhari.

Kwenye makala ya TANO ZA JUMA LA 22 nitakwenda kukushirikisha maarifa zaidi ya jinsi ya kutumia mitandao ya kijamii kwa manufaa na kuepuka hasara zake kutoka kwenye kitabu chetu cha juma hili ambacho ni DIGITAL MINIMALISM.

Usikose kabisa tano za juma hili la 22, kwa sababu zinakuja na falsafa mpya ya kuishi kwenye zama hizi za simu janja na mitandao ya kijamii, na kuhakikisha tunaendelea kuwa watu badala ya kuwa maroboti yanayoendeshwa na mitandao hii, kama wengi walivyo sasa.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge

MASAA MAWILI YA ZIADA