Watu wengi wamedanganywa na kukubali kwamba ushindani ni kitu kizuri kwenye biashara na hata maisha kwa ujumla.

Kwamba kadiri kunavyokuwa na watu wengi wanavyofanya kitu kinachofanana, ndivyo huduma zinakuwa bora na bei zinakuwa nzuri pia.

Hiyo ni kweli, lakini pale ambapo wewe ni mteja au mtumiaji wa huduma ambazo zinatolewa na wale waliopo kwenye ushindani.

Lakini kama wewe ndiye mtoa huduma, ushindani siyo mzuri kwako, bali ushindani ni njia ya kuelekea kushindwa.

Unapoingia kwenye ushindani, iwe ni kwenye biashara au kazi, unaachana na viwango vyako na kuanza kujipima kwa viwango vya wengine. Na ili kuwavutia wengi kwa haraka, njia rahisi ni kufanya vitu rahisi ambavyo vinapokelewa haraka na walio wengi.

Kwenye biashara, kitu rahisi kufanya kwenye ushindani ili kupata watu wengi ni kupunguza bei. Lakini pale washindani wako nao wanapopunguza bei, inakubidi tena upunguze bei, na wao watapunguza bei. Mlolongo unaendelea hivyo, mwisho wa siku hakuna anayetengeneza kipato kizuri katika ushindani huo.

Ni rahisi pia kuona kwamba mteja atanufaika kwa bei za chini zinazotokana na ushindani, lakini hanusuriki hata kidogo. Mteja atadhurika na huduma mbovu ambazo zinatolewa na biashara ambayo inakazana kupunguza bei ili kushinda washindani wake. Hivyo mteja licha ya kupata kwa bei rahisi, huduma anazopata zinakuwa mbovu na hazimridhishi.

Kama kweli unataka mafanikio makubwa kwenye maisha yako, ni lazima uachane kabisa na ushindani. Lazima uache kuangalia wengine wanafanya nini na kufanya kama wao.

Badala ya kushindana, unapaswa kuwa bora zaidi, unapaswa kuwapa wateja wako huduma bora kabisa ambazo hawawezi kuzipata eneo jingine lolote.

Na unafanya hivyo siyo kwa sababu umeona wengine wanafanya, au kwa sababu unataka kuwazidi wengine. Bali unafanya hivyo kwa sababu unajali kuhusu unachofanya na unajali kuhusu wateja wako.

Ushindani ni mbio za kuelekea kushindwa. Ubunifu na ubora ni mbio za kuelekea kwenye kushinda na mafanikio makubwa. Chagua kwa usahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha