Mpendwa rafiki yangu,

Hakuna mtu aliyezaliwa anajua kila kitu na vitu ambavyo tunavyo sasa vyote tumevitafuta hivyo tunao uwezo wa kuviacha kwa sababu hatujazaliwa navyo.

Kumekuwa na tabia za hovyo sana kwa watu wanaoishi mahusiano ya ndoa, watu wanataka kuhalalisha maisha ya ndoa kwa misingi yao wenyewe yaani kufuata misingi ya kidunia. Tukishakuwa tunafuata matakwa yetu sisi kadiri ya matamanio yetu hakika tutakuwa na maisha ya ajabu sana.

Kumekuwa na mitazamo mingi juu ya ndoa wako wanaoona kuwa ndoa ni kitu kizuri na wengine kibaya yote haya ni sawa kadiri ya mtazamo wa mtu binafsi, lakini kiasili ndoa haina ubaya wala uzuri yaani ubaya au uzuri wake unatokana na mitazamo yetu sisi  tunayatoa juu ya ndoa.

Kitu ambacho watu wengi siku hizi wanajaribu kuhalalisha ni kuhalalisha michepuko kuwa ni kitu cha kawaida kadiri ya mitazamo yao. Watu wengi ambao wamekosa kuwa waaminifu katika ndoa zao na kuwa na michepuko hawa wote ni watu ambao wamekubali kuendeshwa na matamanio au hisia za miili yao.

cropped-mimi-ni-mshindi

Huwezi ukabaki salama katika maisha ya ndoa kama wewe ni mtu wa kuendesha na matamanio ya mwili. Kitu pekee ambacho kinawafanya watu wasiwe na uaminifu ni kuendekeza tamaa za mwili. Mwili huwa hauridhiki na huwa unataka uufanyie vile unavyotaka na ukikubali kuwa mtumwa wa mwili lazima utafanya mambo ambayo ni ya ajabu ambayo ni kinyume na taratibu.

SOMA; Hiki Ndiyo Kitu Kidogo Kinachochangia Kuvunja Mahusiano Mengi

Maisha ya kuishi bila uaminifu katika ndoa yanachangaia hata watu kutofanikiwa na kusababisha familia zinakuwa hazina mwelekeo. Watoto wanakuwa hawapati mahitaji yao muhimu huenda baba au mama anaelekeza nguvu nje ya familia yake.

Hakuna kazi kama kazi ya kutumikia mabwana wawili, unapojitoa kwa mmoja lazima kwa mwingine utashindwa. Usikubali kutawanya nguvu zako na kuendeshwa na hisia za mwili badala yake kuwa mwaminifu.

Hatua ya kuchukua leo; usikubali kuendeshwa na hisia za mwili bali tawala akili yako na jiendeshe kwa kutumia akili na siyo matamanio ya mwili na hapo utaweza kushinda mengi katika uaminifu wa ndoa.

Kwahiyo, usiwe mtu wa kuendeshwa na hisia za mwili katika maisha ya ndoa. Ukiwa ni mtu wa kuendeshwa na hisia za mwili utakua siyo mwaminifu katika maisha yako ya ndoa kwani hisia zitakupelekesha na kuvunja uaminifu.

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana