“Indeed, no one can thwart the purposes of your mind—for they can’t be touched by fire, steel, tyranny, slander, or anything.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 8.41
Ni siku nyingine mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Tumeipata nafasi bora kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari SIMAMIA KUSUDI LA AKILI YAKO…
Hakuna mtu yeyote mwenye uwezo au nguvu ya kubadili kusudi la akili yako.
Kuna mambo yanaweza kutokea kwenye mwili wako, kama ajali, maradhi na kadhalika.
Yapo mambo yanayoweza kutokea kwenye mali zako, kama kuibiwa, kupoteza, kufilisiwa na kadhalika.
Yapo kambo yanayoweza kutokea kwenye mahusiano yako kama migogoro, kuvunjika na mengine.
Na wapo wengi wanaoweza kukusumbua kwa namna moja au nyingine.
Lakini yote hayo hayana nguvu ya kugusa akili yako.
Wewe pekee ndiye mwenye nguvu ya kugusa akili yako,
Wewe ndiye unayeweza kuwapa wengine ruhusa ya kugusa akili yako.
Uhuru kamili wa maisha yako upo kwenye matumizi sahihi ya akili yako.
Hivyo simamia kusudi la akili yako, bila ya kujali nini kinachoendelea nje.
Simamia kile unachoamini, pigania kile kilicho sahihi kwa sababu hilo ndiyo kusudi la akili yako, hilo ndiyo linakufanya wewe kuwa mtu.
Watu wengi wamepoteza utu wao kwa sababu hawana tena kusudi la akili zao. Hakuna wanachosimamia, chochote kinachotokea nje kinawaathiri mpaka ndani.
Na ndiyo maana wengi wameishia kuwa walevi na wateja wa vilevi, mitandao ya kijamii na starehe nyingine.
Lakini yote hayo ni ya mpito tu,
Suluhisho kamili lipo kwenye kusimamia kusudi la akili yako.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa na uhuru kamili bila ya kujali kinachoendelea nje, kwa kusimamia vizuri kusudi la akili yako.
UhuruKamiliUpoNdani, #UsiyumbishweNaYaNje, #FanyaKilichoSahihi
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1