“How beautifully Plato put it. Whenever you want to talk about people, it’s best to take a bird’s-eye view and see everything all at once—of gatherings, armies, farms, weddings and divorces, births and deaths, noisy courtrooms or silent spaces, every foreign people, holidays, memorials, markets—all blended together and arranged in a pairing of opposites.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 7.48

Tusiposhukuru kwa siku hii mpya tuliyoiona leo, siyo tu tunakuwa watu wasio na shukrani, bali pia tunajiweka kwenye nafasi ya kuipoteza siku hii.
Tusiposhukuru tutaichukulia kama siku ya kawaida na tutaishi kawaida, ambapo maana nyingine ya neno kawaida ni HOVYO.
Lakini tunaposhukuru tunaithamini kweli siku hii, tunakwenda kuiishi kwa tofauti kwa sababu tunajua hatutapata siku nyingine kama hii.

Tunakwenda kuiishi siku hii ya leo kwa misingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari MTAZAMO SAHIHI WA KUONDOA HOFU ZINAZOKUKABILI..
Kwenye maisha yetu ya kila siku, vitu mbalimbali na hata watu wanaweza kuwa kikwazo kikubwa kwetu.
Wanaweza kutufanya kujisikia vibaya, kukata tamaa na hata kujawa na hofu kuhusu maisha yetu.
Ukifuatilia habari na mitandao ndiyo kabisa unaweza kuona mwisho wa dunia ni kesho, kila mtu ana lake la kusema kuhusu hali mbaya ya vitu fulani.

Unahitaji kujitambua kwa hali ya juu na nguvu kubwa ya kulinda fikra zako ili zisichafuliwe na mawazo hayo hasi ya watu wengine.
Na moja ya njia hizo ni kuyaangalia mambo kwa mtazamo wa tofauti.
Ukiwa usawa wa ardhi kila kitu ni kikubwa kwako na kinatisha.
Lakini ukiweza kuwa juu zaidi angani, kwa kuwa kwenye ndege, kwenye ghorofa ndefu au juu ya mlima, unapoviangalia vitu kwa chini unaviona ni vidogo sana.
Hata watu ambao wanakutisha ukiwaangalia ukiwa juu sana unawaona kama sisimizi.

Huu ndiyo mtazamo sahihi unaopaswa kuendesha nao maisha yako, kwa kuviangalia vitu kwa mtazamo wa kuwa juu na kuangalia chini. Yale yanayokusumbua sasa yatapotea kabisa. Wale wanaokusumbua utawaona kama sisimizi, na huo ndiyo uhalisia, vitu vingi vinavyokutisha ni vidogo sana, na havina nguvu ambayo unafikiri vinayo.

Mungu ana nguvu kwa sababu anatuona sisi wote kama sisimizi, kuanzia matajiri wakubwa, viongozi wakubwa mpaka watu wa kawaida kabisa. Hakuna anayemtisha.
Amsha nguvu ya uungu iliyopo ndani yako kwa kuona watu au vitu kwa mtazamo wa juu, kwa kuacha kukuza vitu na kuondokana kabisa na kila aina ya hofu.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuyaangalia yale yote yanayokusumbua sasa ukiwa juu angani na utaona ni jinsi gani ni madogo kama sisimizi.
#KuwaNaMtazamoWaAnga, #UsikuzeVituZaidiYaUhalisiaWake, #HakunaChenyeNguvuJuuYako

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha