“Why then are we offended? Why do we complain? This is what we’re here for.”
—SENECA, ON PROVIDENCE, 5.7b–8

Hongera sana wanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari NDIYO SABABU YA WEWE KUWA HAPA DUNIANI…
Huwa tunatamani sana maisha yetu yangekuwa rahisi,
Hatupendi kukutana na magumu wala changamoto,
Tunataka kupata kila tunachotaka na kila mtu awe na afanye kama tunavyotaka sisi.
Lakini mambo hayaendi hivyo, na hilo linatuvuruga zaidi.

Rafiki, magumu na changamoto ndiyo sababu ya sisi kuwa hapa duniani.
Hivyo ni sehemu ya maisha yetu, ni vitu tunavyopaswa kukabiliana navyo na hatupaswi kuvihofia wala kuvikwepa.
Siyo sisi tumeanza kukutana na magumu na changamoto hizi,
Kizazi chote cha binadamu, tangu enzi na enzi wamekuwa wanapitia magumu na changamoto.

Tena watangulizi wetu walikuwa na mazingira na hali ngumu kuliko sisi.
Hebu fikiria watu walioishi miaka 200 iliyopita,
Wakati ambapo hapakuwa na umeme kabisa, hivyo vitu vingi unavyofurahia kwa uwepo wa umeme havikuwepo.
Hapakuwa na njia nzuri za usafiri, hivyo mtu alipotaka kutoka sehemu moja kwenda nyingine ilikuwa safari ya siku nyingi.
Hapakuwa na mifumo mizuri ya afya hivyo watoto wengi walikuwa utotoni na njia pekee ya kukabiliana na hilo ilikuwa ni mtu kuwa na watoto wengi, ili hata wakifa wachache, wengine wanasalia.

Hebu fikiria vitu vyote vinavyokuzunguka sasa, ambavyo waliotutangulia hawakupata nafasi ya kuwa navyo.
Halafu bado unalalamika mambo ni magumu, changamoto kubwa na huwezi kufanikiwa!
Usijidanganye kwa namna hiyo.

Magumu na changamoto ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku, tuyavuke ili kupiga hatua zaidi kwenye maisha.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuyapokea magumu na changamoto na kuyavuka ili kuwa na maisha bora.
#MagumuNiSehemuYaMaisha, #MaraZoteIpoNjia #HakunaKinachoendaKamaUnavyotaka

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha