Ni kawaida yetu binadamu kuangalia nyuma na kuona mambo yalikuwa mazuri zaidi siku za nyuma kuliko yalivyo sasa.

Hasa pale mabadiliko yanapokuwa yametokea na kutulazimisha kubadilika bila ya sisi wenyewe kutaka. Huwa tunaona enzi hizo mambo yalikuwa mazuri kuliko sasa.

Lakini ukweli ni kwamba, chochote unachojiambia sasa kuhusu siku za nyuma umekikuza zaidi, umeweka chumvi kuliko uhalisia wake.

Unaweza kuwa unajiambia kama ungesoma kitu fulani ulichoacha kusoma basi maisha yako yangekuwa bora sana sasa kuliko yalivyo sasa.

Au unajiambia ungeoa au kuolewa na mtu uliyekuwa naye kwenye mahusiano siku za nyuma basi maisha yako yangekuwa mazuri mno sasa.

Au kama usingeacha kazi uliyoacha huko nyuma, kwa sasa ungekuwa mbali zaidi.

Yote haya unaweza kuona ni sahihi, lakini unajidanganya.

Kwanza kabisa unapoangalia nyuma huoni kila kitu, bali unaona kile unachotaka kuona, hivyo utaona yale mazuri sana au yale mabaya sana, yale mengine ya kawaida, ambayo ndiyo mengi hutayaona kabisa.

Pili, hakuna kitu kinabaki kama kilivyo, kila kitu kinabadilika, hivyo hata kama ungefanya kile ambacho hukufanya huko nyuma, bado leo hii usingeendelea kupata yale matokeo uliyokuwa unapata kipindi hicho.

Jua kwamba hapo ulipo sasa ndiyo sehemu sahihi kwako kuwa ili kufanikiwa zaidi. Unachopaswa kujua ni jinsi ya kutumia hapo ulipo sasa kwa mafanikio yako zaidi.

Acha kujidanganya na picha nzuri za nyuma, kubali kila hatua ambayo tayari umeshaichukua na angalia unawezaje kufanya maamuzi bora leo ili kesho yako iwe bora zaidi.

Acha kuangalia sana nyuma, hakuna unachoweza kubadili kuhusu nyuma yako, lakini unaweza kuchukua hatua sahihi leo na ukapata matokeo bora sana kesho.

Ukweli ni ule unaoujua na kuuishi leo, yaliyopita unajidanganya na yajayo unajipa matumaini hewa. Angalia pale ulipo sasa na jiulize unawezaje kupiga hatua kubwa zaidi na piga hatua hizo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha