“To the youngster talking nonsense Zeno said, ‘The reason why we have two ears and only one mouth is so we might listen more and talk less.’”
—DIOGENES LAERTIUS, LIVES OF EMINENT PHILOSOPHERS, 7.1.23

Shukrani ndiyo kitu pekee tunachoweza kutoa kwa nafasi hii nyingine nzuri tuliyoipata.
Siyo kila aliyepanga kupata nafasi hii ya leo ameweza kuiona.
Kuna ambao wangekuwa tayari kukipa kiasi kikubwa sana dha fedha ili tu waione siku hii, lakini hawajaweza kuiona.
Hivyo kama utachagua kuichukulia siku hii kama siku ya kawaida, kama siku nyingine tu, jua kwa hakika kuna siku hutapata nafasi kama ya leo, na utajutia sana.

Tukaianze siku hii kwa shukrani kuu kwa kuiona siku hii, na kukamilisha shukrani hiyo kwa kuweka vipaumbele vyetu kwa usahihi.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari MDOMO MMOJA, MASIKIO MAWILI…
Ukikutana na mtu ambaye anatumia mikono yake kutembea huku miguu ikiwa mizima kabisa, utakuwa na uhakika kwamba mtu huyo ana tatizo.
Ukikutana na mtu ambaye ameamua kufumba macho yake na kutembea bila ya kuangalia utajua ana tatizo.
Kila kiungo tulichonacho kina matumizi sahihi kwake na kwa kiwango sahihi.
Kutumia kiungo kwa matumizi yasiyo sahihi au kwa kiwango kisicho sahihi ni kiashiria kwamba kuna shida fulani ndani ya mtu.

Hilo ndiyo limekuwa linaonekana kwenye mazungumzo,
Watu wengi wanaongea sana, wanaongea zaidi ya wanavyosikiliza, kitu ambacho ni matumizi mabaya ya viungo vya mwili.
Una masikio mawili na mdomo mmoja, ikimaanisha kwamba unapaswa kusikiliza mara mbili ya unavyoongea.
Ukifuata kanuni hii, kwanza kabisa utajifunza mengi mno, unajifunza kwa kusikiliza na siyo kwa kuongea.
Pili unajiepusha na matatizo mengi, ukitafakari sehemu kubwa ya matatizo ambayo umewahi kukutana nayo kwenye maisha yako, ni mdomo ndiyo uliokuponza.
Kama ungekaa kimya, usingeingia kwenye matatizo mengi uliyoingia.
Kukaa kimya kunakufanya uonekene una hekima kuliko wale wanaoongea hivyo.
Na kadiri unavyoongea sana, ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kusema mambo ya kipumbavu ambayo yataondoa heshima yako kwa wengine na hata kukuingiza kwenye matatizo.

Tumia kwa usahihi viungo vya mwili wako, inapokuja kwenye mdomo na masikio, tumia iwiano uliopo. Sikiliza mara mbili ya unavyoongea na utajifunza na kujiepusha na mengi.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuongea kidogo na kusikiliza zaidi.
#SikilizaZaidiYaKuongea, #KukaaKimyaNiHekimaKuu #SiyoLazimaUweNaMaoniKwenyeKilaJambo

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1