“Don’t be ashamed of needing help. You have a duty to fulfill just like a soldier on the wall of battle. So what if you are injured and can’t climb up without another soldier’s help?”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 7.7
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ambayo tumeiona leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari USIONE AIBU KUOMBA MSAADA…
Watu wengi huona kuomba msaada kwa wengine ni udhaifu,
Huwa wanaona aibu kuomba msaada pale wanapokuwa wamekwama kwa kutotaka kuonekana ni dhaifu.
Lakini hakuna udhaifu wowote kwenye kuomba msaada.
Hakuna mtu yeyote anayeweza kufanya kila kitu peke yake,
Tunahitaji sana msaada wa wengine.
Tena umefika hapo ulipo sasa kwa sababu ya msaada wa wengine,
Maana ulizaliwa ukiwa huwezi kufanya chochote, huwezi hata kula mwenyewe.
Lakini ukasaidiwa na kuweza kukua.
Hivyo kupiga hatua zaidi ya hapo ulipo sasa, unahitaji msaada wa wengine.
Usione aibu kuomba msaada,
Ni sehemu ya maisha,
Kama mwanajeshi aliyejeruhiwa vitani, haijalishi ni shujaa kiasi gani, anahitaji msaada wa wengine.
Omba huo msaada unaohitaji ili kutoka hapo ulipokwama sasa,
Unaweza kuwa msaada wa mawazo, ushauri, fedha, nguvu na kadhalika.
Na wengi wapo tayari kukusaidia pale utakapo omba msaada wao.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuomba msaada wa wengine pale unapokwama bila ya kuona aibu.
#UnahitajiMsaada #KusaidiwaSiUdhaifu #HuweziKufanyaKilaKituPekeYako
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1