Mpenwa rafiki yangu,

Sehemu kubwa ya maisha yetu sisi binadamu ni mahusiano. Ni lazima tujitahidi kuboresha eneo la mahusiano ili mambo yaende mbele, tukiwa na matatizo kwenye mahusiano tunajikuta tunashindwa kufanya yale muhimu yanayotuletea maana kwenye maisha yetu.

Ukiwa vizuri kwenye mahusiano yako, unajikuta unafanya vizuri maeneo mengi yaliyobakia. Ukiwa na msongo wa mawazo kwenye mahusiano yako basi itakusumbua sana wewe kupata utulivu wa akili na kufanya kazi zako kwa umakini. Unapotoka nyumbani ukiwa vizuri na familia yako hata kazini kwako utaenda kufanya vizuri, ila kama nyumbani hapana amani akili yako pia itataharuki, haitotulia unajikuta sehemu kubwa unafikiria yale matatizo na siyo kazi husika.

KAVA IJUE NJAA YA WANANDOA

Iko falsafa ambayo kila mmoja wetu akiitumia kwenye mahusiano yake atakuwa bora sana.  Ni falsafa ambayo itakufanya usimame na maisha yake na siyo kumtegemea tena mtu akufanyie kitu fulani. Na hili limechambuliwa vizuri kwenye kitabu cha ijue njaa ya wanandoa.  Kama unataka mahusiano yako bora nakusihi sana utumie falsafa hii;

Katika mahusiano yako, ingia na gia hii umekuja kutumika na siyo kutumikiwa. Kila kiongozi ambaye ndiyo wewe mwenyewe, katika mahusiano yako wewe angalia na ishi kwa falsafa hii, usikae chini au unatembea umeweka mikono mifukoni ukifikiria umekuja kutumikiwa. Mahusiano yanakuwa magumu pale watu wanapoanza kuona wao ndiyo wanastahili zaidi kutumikiwa na siyo kutumika.

SOMA;Ushauri Kwa Kijana Yeyote Anayetaka Kuingia Katika Mahusiano Ya Ndoa

Wote kuzaliwa kwetu maana yake tumekuja kutumika, tunapojitoa kutumika utashangaa hata wewe mahusiano yako yanakuwa bora, unajua ni katika kutoa ndiyo tunapokea, kama unataka mwenzi wako akutii, hebu wewe anza kutumika kwa kumuonesha upendo, halafu uone kama hutopata kile unachotaka.

Hatua ya kuchukua leo; anza kuboresha mahusiano yako na familia yako, ndugu, jamaa na marafiki kwa kuanza kutumika kwenye nafasi yako na siyo kusubiri wengine ndiyo wakutumikie. Kila mmoja anatakiwa kuwajibika katika nafasi yake ya mahusiano na kufanya hivyo ndiyo inaleta maana nzima ya falsafa ya umekuja kutumika na siyo kutumikiwa.

Kwahiyo, wako watu wengi wanaona mahusiano yao ni mzigo kwa sababu wameingia kwa gia ya kutumikiwa, hivyo hawajisumbui kutaka kutumika. Ukisubiri kutumikiwa lazima utashindwa maeneno mengi ya maisha yako mwenyewe ili maisha yako yaende. Kama unataka mahusiano yako yawe na upendo, basi tumika kutoa upendo na utashangaa wewe mwenyewe kuona jinsi upendo unavyotawala kwenye mahusiano yako.

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana