Mpendwa rafiki yangu,

Iko wazi kwamba hakuna wito ambao utauchagua wewe utakosa kuwa na changamoto. Ukiamua kuingia katika wito fulani kwa kuangalia changamoto na siyo kufuata moyo wako huenda ukashindwa mapema.

Watu wengi wanaoshindwa katika mahusiano ni wale wanaoingia kwa gia moja tu, ndoa ni kama biashara huwa ina changamoto zake. Kama unapata faida basi ujue kuna siku na hasara nayo inakuhusu.

KAVA IJUE NJAA YA WANANDOA

Iko mitazamo mingi sana katika jamii inayowafanya watu waichukulie ndoa kuwa kama siyo sehemu salama.  Ndoa ni salama au siyo salama ni kadiri ya mtazamo au gia uliyoingia nayo. Na kwenye akili huwa inakupa kile unachofikiria, yaani uko hivyo ulivyo kadiri ya kile unachofikiria. Unapofikiria mabaya ya ndoa ndivyo utakavyokutana nayo na unavyofikiria mazuri ndivyo utakavyokuwa.

Kwa asili hakuna kitu kibaya bali mitazamo yetu tuliyokuwa nayo ndiyo yanafanya hicho kitu kuwa kibaya au kizuri.

Baada ya kupata utangulizi huo sasa turudi kwenye kiini cha makala yetu ya leo, ambapo tunakwends kujifunza jinsi ya kuepuka malumbano katika ndoa.

Njia rahisi ya kuepuka malumbano katika ndoa ni kushuka pale mwenzako anapopanda. Ukiona mwenzako ana hisia za hasira basi cha msingi hutakiwi kuwa kama yeye, akiwa na hasira mwache hasira yake imalizike ndiyo mwongee.

SOMA; Kama Unataka Kuboresha Mahusiano Yako Tumia Falsafa Hii Hapa

Mwenza wako akiwa juu wewe shuka chini, kwa namna hiyo utaepuka malumbano sasa kwa mfano, kama mtu akiwa amepanda juu wewe ukijifanya mjinga ukijishusha na kuwa mnyenyekevu atakupatia wapi kwenye ugomvi au malumbano?

Unatakiwa kujifunza kuishi na watu vizuri, mtu uliye naye kwenye ndoa ni mtu ambaye mnatakiwa mchukuliane kwa kila mmoja. Kila mmoja ana changamoto zake na huwezi kumbadilisha mtu awe kama wewe hiyo ni kazi ngumu ambayo ukijaribu lazima itakushinda.

Hatua ya kuchukua leo; epuka malumbano na ugomvi katika ndoa yako. Pale ambako mwenzako yuko juu wewe shuka chini kwa njia hii mtaepusha mambo mengi sana kwani watu huwa wanagombana sana kwa sababu ya ujinga wa kila mtu kutaka kushinda kwenye malumbano.

Kwahiyo, mara nyingi hisia zikiwa juu akili inakuwa chini. Mtu ambaye yuko kwenye hisia hatumii akili bali hisia ndiyo zinamwongoza. Usipambane na mtu ambaye yuko kwenye hisia kwa sababu hatumii akili anaongozwa na hisia na hiyo ni kitu hatari sana.

Makala hii imeandikwa na

Mwl. Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa  http://kessydeo.home.blog vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com //kessydeoblog@gmail.com

Asante sana