“We should take wandering outdoor walks, so that the mind might be nourished and refreshed by the open air and deep breathing.”
—SENECA, ON TRANQUILITY OF MIND, 17.8

Ni siku nyingine nzuri, siku mpya na ya kipekee sana kwetu.
Tumepata nafasi hii nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari FANYA MATEMBEZI…
Ipo siri moja kubwa ambayo wale walioweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yao wanaijua.
Wale ambao wameweza kuja na mawazo bora na ya tofauti wamekuwa wanatumia sana siri hii.
Wale ambao wameweza kupata utulivu licha ya kuwa kwenye misukosuko na msongo wameitumia sana siri hii.

Siri yenyewe ni KUFANYA MATEMBEZI.
Kufanya matembezi ni kitu ambacho kwa nje kinaweza kuoneka ni kidogo na cha kawaida.
Lakini kwa ndani ya mwili wako na akili yako ni kitu kikubwa sana, na chenye manufaa nakubwa mno.

Unapofanya matembezi unauweka mwili kwenye mwendo, unachangamsha ubongo wa ubunifu na unaungana na asili.
Vitu hivi vinaufanya mwili kuwa imara, akili kuwanna ubunifu na kuwa na utulivu mkubwa ndani yako.
Hivyo pale unapojikuta umekwama, akili na mwili vimechoka na umepatwa na msongo, ondoka ulipo na fanya matembezi.
Fanya matembezi yasiyo na lengo lolote lile, bali tu kutembea.
Na ukiweza kutembea eneo la asili, kama kwenye pori au bustani, unapata manufaa zaidi.

Leo hakikisha unapata muda wa kufanya matembezi, na fanya huu kuwa utaratibu wako wa kila siku.
Unapokuwa na msongo, fanya matembezi,
Unapokuwa na tatizo kubwa unalohitaji kutatua, fanya matembezi.
Unapokuwa unataka kufanya kitu cha kibunifu, fanya matembezi.
Unapokuwa na mazungumzo kwa njia ya simu, fanya matembezi.
Unapokuwa na mkutano au kuonana na rafiki, fanya matembezi.

Kwa kufanya matembezi, unauweka mwili na akili kwenye hali bora na chochote unachofanya kinakuwa bora zaidi.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kufanya matembezi pale unapokuwa na msongo, umekwama, unataka ubunifu au una mazungumzo na mtu mwingine.
#FanyaMatembezi #OndoaMsongo #IbuaUbunifu

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1