“You could enjoy this very moment all the things you are praying to reach by taking the long way around—if you’d stop depriving yourself of them.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 12.1

Ni jambo la kushukuru mimi na wewe rafiki yangu kuiona siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Siyo kwa juhudi wala ujanja wetu tumeioja siku hii, bali kwa bahati tu.
Tukaitumia nafasi hii vizuri ili kuweza kufanya yenye manufaa kwetu na wengine pia.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UNACHOTAFUTA TAYARI UNACHO…
Huwa tunaweka juhudi kubwa sana kutafuta vitu kwenye maisha, wakati vitu hivyo tayari vipo ndani yetu.
Tunahangaika sana kutafuta nje badala ya kuangalia ndani yetu wenyewe na kuanza kutumia vitu hivyo ambavyo tunavyo.

Ukiangalia yale yote tunayofanya, utagundua kuna vitu vitatu ambavyo kila mtu anapigania kuvipata.
Moja ni furaha,
Mbili ni uhuru,
Tatu ni heshima.
Vitu vyote hivyi vitatu tayari vipo ndani yako,
Furaha ni kitu ambacho tayari kipo ndani yako, ni wewe kuanza kuiishi.
Uhuru tayari unao wa kutosha, ni wewe kuamua kuanza kuutumia.
Na heshima, ni kitu kinachoanza na wewe mwenyewe, halafu wengine watakupa pia.

Unaweza kuona ni jinsi gani maisha yako yatakuwa rahisi kwa kuanza na vitu hivyo ambavyo tayari unavyo, badala ya kukimbizana navyo.
Na hii haimaanishi kwamba huna haja ya kufanya chochote kwenye maisha yako, unahitaji kujituma sana, lakini kwa sababu sahihi na siyo kwa sababu unatafuta vitu ambavyo tayari unavyo.

Usijitume kufanya kazi sana kwa sababu unataka furaha, badala yake anza na furaha, na hiyo ikusukume kufanya kazi sana kwa sababu una mchango mkubwa wa kutoa kwa wengine.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuacha kutafuta vitu ambavyo tayari vipo ndani yako.
#UnachotafutaUnacho #FurahaZaoLaNdani #UhuruNiWako

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1