Asili ni mwalimu mzuri sana wa mafanikio,
Kama utachagua kujifunza kupitia asili, utaweza kupata mafanikio makubwa sana kwenye maisha yako.
Asili huwa inafanya vitu vyake kwa misingi miwili, muda na msimamo.
Angalia sehemu ambapo tone la maji linadondoka kwenye mwamba kwa kujirudia rudia. Tone moja halina nguvu ya kuvunja mwamba, lakini matone hayo yanapoendelea kwa muda mrefu, mwamba unavunjika.
Kadhalika angalia mifumo yote ya maisha kwenye asili, hakuna kitu kinachotokea kwa ghafla, kila kitu kina muda wake wa kutokea. Mfano ukipanda mbegu ya mbuyu, inachukua miaka mpaka mbegu hiyo ichomoze huwezi kulazimisha ichomoze haraka kabla ya muda wake.
Lakini inapokuja kwenye mafanikio yetu, huwa tunataka vitu vitokee haraka, la sivyo tunaacha.
Tunataka kuanza kufanya mazoezi leo halafu kesho tuwe vizuri kiafya, la sivyo tunajiambia mazoezi hayana manufaa.
Tunataka kuanza dayati nzuri leo halafu kesho tuwe kwenye afya bora sana, la sivyo tunasema dayati hiyo haifai.
Tunataka kuingia kwenye biashara leo halafu kesho tuwe tunatengeneza faida kubwa, la sivyo tunajiambia biashara hiyo haifai na kwenda kwenye biashara nyingine.
Rafiki, hakuna mabadiliko yatakayotokea kesho, wala wiki ijayo, wala mwezi ujao na wakati mwingine hata mwaka ujao kwa hatua ambazo umechukua leo. Inachukua muda kidogo kuanza kuona matokeo unayotarajia kuona baada ya kuanza kuchukua hatua za tofauti.
Iige asili, weka vitu viwili upande wako. Jipe muda wa kufanya kitu, ni muda kiasi gani haijalishi, wewe jua kadiri unavyofanya ndivyo unajipa nafasi ya kufanikiwa zaidi.
Pili kuwa na msimamo kwenye ufanyaji, kila siku chukua hatua kwenye kile unachofanyia kazi, unachotaka kupata mabadiliko. Usiwe mtu wa kuanza na kuacha, usiwe mtu wa kujaribu na kuacha na usiwe mtu wa kufanya ukiwa na hamasa na baadaye kuacha. Kuwa mtu wa kufanya kila siku, hata kama ni kwa kiasi kidogo. Unapofanya kila siku, matokeo yanajikusanya na kuwa makubwa.
Mabadiliko unayotaka kwenye maisha yanawezekana, lakini hayatatokea kesho. Jipe muda na kuwa na msimamo na mwisho wa siku utapata chochote unachotaka.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,