Ili ufanikiwe unahitaji mipango, lakini mipango siyo inayoleta mafanikio.
Mipango ni sehemu ndogo sana ya mafanikio yako.
Sehemu kubwa ya mafanikio inatokana na hatua ambazo unachukua kwenye mipango uliyojiwekea.
Haijalishi una mipango mingi kiasi gani, kama huchukui hatua huwezi kufanikiwa.
Watu wengi sana wamekuwa wanakwama kwenye mipango. Wanaweka mipango mikubwa na mizuri, lakini inapofikia kwenye kuchukua hatua wanajikuta wanahitaji kuboresha zaidi mipango yao. Hilo linaendelea kwa muda mrefu na unakuta mtu ana mipango mingi lakini hakuna hatua anazochukua.
Kinachowazuia wengi kufanikiwa siyo kukosa mipango, bali kutokuchukua hatua. Mipango kila mtu anayo, lakini kuchukua hatua ni wachache sana wanaofanya hivyo.
Watu wengi husita kuchukua hatua kwa kuona kwamba bado hawajawa tayari kwa mipango waliyonayo, au kuona mipango waliyonayo inahitaji marekebisho na maboresho zaidi.
Hiyo inaweza kuwa sawa, lakini unapaswa kujua kwamba hakuna wakati ambao utakuwa na mpango uliokamilika kwa kila kitu. Hivyo kama unasubiri mpaka mipango yako ikamilike kabisa ndiyo uchukue hatua, hutaweza kuchukua hatua kamwe.
Unahitaji kuchukua hatua hata kabla hujajiona una mipango kamili. Kwa kuchukua hatua utajifunza mambo mengi kuliko kutokuchukua hatua na kusubiri mipango ikamilike.
Popote ulipokwama sasa ni kwa sababu kuna hatua hujachukua. Anza kuchukua hatua sasa na utaweza kuondoka pale ulipokwama na kufanikiwa zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,