“While it’s true that someone can impede our actions, they can’t impede our intentions and our attitudes, which have the power of being conditional and adaptable. For the mind adapts and converts any obstacle to its action into a means of achieving it. That which is an impediment to action is turned to advance action. The obstacle on the path becomes the way.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 5.20
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ambayo tumeiona leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KIKWAZO NDIYO NJIA…
Kila mipango ambayo tunajiwekea kwenye maisha yetu, kuna vikwazo huwa vinaibuka kutuzuia tusifikie mipango hiyo.
Wengi huchukulia vikwazo hivi kama ndiyo mwisho wa safari yao ya mafajikio.
Lakini hilo siyo sahihi,
Kama unataka kufanikiwa kwenye maisha, hupaswi kuruhusu vikwazo viwe ukomo wa safari yako.
Badala yake vikwazo vinapaswa kuwa ndiyo njia yako ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa.
Kila unapokutana na kikwazo, jua hapo umekutana na njia sahihi ya kuelekea kwenye mafanikio unayotaka.
Umepata hasara kwenye biashara, huo siyo mwisho wa biashara, badala yake ni darasa la kuongeza umakini wako kwenye biashara.
Umekubaliana vitu fulani na watu na baadaye wamekiuka makubaliano hayo, huo siyo mwisho, bali ni darasa la kujua watu gani sahihi wa kukubaliana nao na wapi wa kuepuka.
Umejaribu kitu na kushindwa kabisa, hiyo ni njia nzuri ya kuanza upya, kuanza ukiwa na uzoefu wa kitu gani usifanye.
Kila kikwazo unachokutana nacho kwenye mipango unayojiwekea, jua hiyo ndiyo njia ya wewe kupata kile unachotaka.
Nimekuwa nasema dunia ni kama huwa inatutega hivi, kutupima ni kwa kiasi gani tumejitoa kwa kile tunachotaka.
Hivyo unapopanga kufanya kitu cha tofauti, vinaibuka vikwazo vya kila aina.
Kama kitu unakitaka kweli, utang’ang’ana na dunia itakupa unachotaka. Kama kitu hukitaki kweli utaishia njiani.
Kuanzia leo, kikwazo chochote unachokutana nacho kwenye safari yako ya mafanikio, jiulize kinawezaje kuwa njia ya wewe kufanikiwa zaidi. Kisha kitumie kama njia ya kufanikiwa.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kugeuza kila kikwazo unachokutana nacho kuwa njia ya wewe kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
#VikwazoNiNjia #DuniaHaitakupaChochoteKirahisi #Ng’ang’anaMpakaUpateUnachotaka
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa ,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1