“Whatever anyone does or says, for my part I’m bound to the good. In the same way an emerald or gold or purple might always proclaim: ‘whatever anyone does or says, I must be what I am and show my true colors.’”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 7.15
Kuipata nafasi hii mpya ya leo ni zawadi ya kipekee sana kwetu.
Ni jambo ambalo tunapaswa kushukuru sana, kwa sababu siyo wote waliopata nafasi ambayo sisi tumeipata.
Na kukamilisha shukrani hiyo tuhakikishe tumeitumia siku ya leo vizuri, kwa kutumia muda wetu vizuri na kufanya yale sahihi.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KUWA WEWE, FANYA KAZI YAKO…
Haijalishi wengine wanasema na kufanya nini,
Wewe una jukumu moja kubwa hapa duniani, ambalo ni kuwa wewe na kufanya kazi yako.
Watu watasema mengi kuhusu wewe, mazuri au mabaya, hiyo haijalishi.
Kitu muhimu ni kuwa wewe, kufanya kazi yako, na muhimu zaidi, kuwa mwema na kufanya kilicho sahihi.
Dhahabu inaendelea kubaki dhahabu, iwe watu wanaikubali ni dhahabu au la.
Na wewe endelea kuwa wewe, kwa kufanya kazi yako, kuifanya kwa ubora wa hali ya juu, iwe watu wanakubali au la.
Kama umefanya kazi yako, umefanya kilicho sahihi, dunia itakuwa na wajibu wa kukulipa, hata kama kuna ambao wanakupinga na kukataa, kuna ambao wataona manufaa ya kile unachofanya, na watakuwa tayari kwenda na wewe.
Usipoteze muda na nguvu zako kuangalia wengine wanafanya nini au kisema nini.
Usipoteze muda na nguvu zako kutaka kumridhisha kila mtu, kutaka kila mtu akubaliane na wewe.
Badala yake peleka nguvu zako kwenye kuwa wewe na kufanya kazi yako.
Wale wanainufaika na unachofanya, watafurahia sana uwepo wako na hawatataka uwe kama wanavyotaka wao, bali watakwenda na wewe kama mtu halisi, kama mtu anayefanya kilicho sahihi.
Kuwa wewe, fanya kazi yako, fanya kilicho sahihi mara zote na waache wengine waendelee na maisha waliyochagua. Dunia itakuwa na jukumu la kukulipa kadiri ya unavyofanya.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa wewe na kuifanya kazi yako bila kujali wengine wanasema na kufanya nini.
#KuwaWewe #IfanyeKaziYako #FanyaKilichoSahihi
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1