#TANO ZA JUMA #26 2019; Asili Ya Biashara Ni Kukua Na Kufa, Jinsi Ya Kuendesha Biashara Yenye Mafanikio, Siri 101 Za Mafanikio Kwenye Biashara Usizofundishwa Shuleni, Kwa Nini Wenye Uelewa Wa Fedha Siyo Wazuri Kwenye Biashara Na Vitu Viwili Vinavyoitofautisha Biashara.

Rafiki yangu mpendwa,

Tumefika katikati ya mwaka 2019, majuma 26 ya kwanza yameisha, yamebaki majuma 26 ya pili ya kuumaliza mwaka huu.

Huu ni wakati mzuri kwa kila mmoja wetu kufanya tathmini ya jinsi mwaka huu unavyoenda kwake, zile hatua anazochukua na matokeo ambayo ameyapata. Kisha kujilinganisha na malengo ambayo uliweka kwa mwaka huu na kuona kama upo kwenye njia sahihi au umeshatoka kwenye njia hiyo.

Nikukaribishe kwenye TANO ZA JUMA ambapo nakwenda kukushirikisha mambo matano muhimu ya kufanyia kazi ili maisha yako yaweze kuwa bora zaidi.

Juma hili la 26 nakwenda kukushirikisha kutoka vitabu viwili, cha kwanza ni 101 Crucial Lessons They Don’t Teach You in Business School kilichoandikwa na Chris Haroun. Kwenye kitabu hiki tumejifunza siri 101 za mafanikio kwenye biashara na maisha kwa ujumla ambazo hazifundishwi kwenye shule ya biashara.

Kitabu cha pili ni Just Run It!: Running an Exceptional Business is Easier Than You Think kilichoandikwa na Dick Cross. Kupitia kitabu hiki tunajifunza mfumo rahisi wa kuendesha biashara yenye mafanikio makubwa huku ukiwa na uhuru.

just run it

Karibu kwenye tano hizi za juma, ujifunze, uhamasike na uende kuchukua hatua ili uweze kufanikiwa zaidi.

#1 NENO LA JUMA; ASILI YA BIASHARA NI KUKUA NA KUFA.

Biashara ni kiumbe hai. Inatungwa, inazaliwa, inakua, inafikia makamo na kisha kufa. Hivi ndivyo mifumo yote ya maisha inavyokwenda. Kuanzia kwetu sisi binadamu, kabla hujazaliwa mimba inatungwa, anazaliwa mtoto, anakua, anafikia makamo na kisha anakufa.

Katika mfumo huu wa ukuaji wa biashara, utungwaji wa mimba ya biashara ni yale mawazo ya kuanza biashara ambayo mtu anakuwa nayo. Kisha kuanza kwa biashara ni sawa na mtoto anayezaliwa, kukua na kisha kufa. Sasa kama ilivyo kwenye asili, siyo mimba zote zinazotungwa zinazaliwa, nyingine zinaharibika kabla ya kufikia kuzaliwa. Na hata watoto wadogo wanaozaliwa, wengi hawafiki utu uzima, wanakufa kabla. Na wachache wanafika utu uzima na kufa.

Kwenye biashara, biashara nyingi huwa zinashindwa kabla hata ya kuanza, nyingi zinaishia kwenye mawazo pekee. Kwa zile ambazo zinaanza, nyingi huwa zinakufa kwenye uchanga, hazikui kufikia ukomavu. Na zile ambazo zinakua, huwa zinafikia ukomavu na kufa.

Lakini zipo biashara chache sana ambazo zimeweza kuondoka kwenye mfumo huo wa ukuaji na kufa. Biashara hizi zimekuwa zinajua kinachopelekea biashara kufa baada ya kukomaa ni bidhaa au huduma kuzoelekea na kutokuwa na kitu kipya.

Ili kuondokana na hali hiyo ya biashara kufika ukingoni na kufa, wafanyabiashara hao ambao biashara zao hazifi, wamekuwa wanakuja na bidhaa mpya au huduma mpya kila mara ambapo bidhaa au huduma ya zamani imefikia kilele chake cha mauzo. Hawasubiri mpaka mauzo yaanze kupungua na biashara kufa. Badala yake wanakuja na bidhaa au huduma mpya inayowafanya waendelee kuwa sokoni.

Huu ndiyo mfumo unaotumiwa na makampuni makubwa ya teknolojia, chukulia mfano wa kampuni ya Apple ambayo inazalisha simu aina ya Iphone. Kila mwaka huwa wanakuja na toleo jipya la simu zao, ambalo halitofautiani sana na toleo lililopita. Yote hii ni kuhakikisha kwamba wanaendelea kuwa sokoni. Kwa sababu kampuni ikishatoa toleo jipya, na watu wote wakawa nalo, hakuna tena fursa ya ukuaji. Lakini wanapokuja na toleo jipya, wale waliokuwa na toleo la zamani wanatamani kuwa na toleo jipya na hapo mauzo yanaanza upya.

Kwa biashara unayofanya, angalia jinsi unavyoweza kutumia njia hiyo ya kuwa na toleo jipya la bidhaa au huduma kila wakati ili biashara yako isife.

#2 KITABU CHA JUMA; JINSI YA KUENDESHA BIASHARA YENYE MAFANIKIO.

Watu wengi huingia kwenye biashara wakiwa na mpango wa kuendesha biashara hizi na kupata mafanikio yatakayowapa uhuru. Lakini wanachokutana nacho wanapoingia kwenye biashara ni tofauti na mategemeo yao. Wanajikuta biashara inawaendesha wao, na hawana uhuru wala mafanikio waliyotegemea kupata.

Mwandishi na mshauri wa biashara Dick Cross kupitia kitabu chake kinachoitwa Just Run It!: Running an Exceptional Business is Easier Than You Think ametushirikisha mfumo bora wa kuendesha biashara ambao unaiwezesha biashara kujiendesha kwa mafanikio na ambayo itakupa uhuru mkubwa.

Karibu tujifunze njia bora ya kuendesha biashara ambayo itaiwezesha biashara kukua na kukupa wewe uhuru mkubwa.

MOJA; UNAHITAJI FALSAFA TOFAUTI YA KUENDESHA BIASHARA.

Falsafa ambayo wengi wamekuwa nayo kwenye kuendesha biashara ni kuelewa vipande vya biashara wakiamini ndiyo wataweza kuielewa biashara vizuri. Wengi huifikiria biashara kwa vipande vyake, mfano mauzo, masoko, uzalishaji, fedha na kadhalika.

Na hata vyuo vya biashara vimekuwa vinafundisha biashara kwa mfumo huo wa kuangalia kipande kimoja kimoja.

Ili uendeshe biashara yenye mafanikio, unahitaji kuwa na falsafa ya tofauti, falsafa inayoiangalia biashara kwa ujumla na siyo kwa vipande vyake. Unapoweza kuiangalia biashara kwa ujumla kama kitu kimoja, ni rahisi kuona vipande vyake vinashirikianaje na hivyo unapotaka kuikuza, unajua hatua zipi sahihi za kuchukua.

MBILI; VIPANDE VIKUU VINNE VYA BIASHARA YENYE MAFANIKIO.

Baada ya kubadili jinsi unavyoiangalia biashara yako, kutoka kuiangalia kwa vipande na kwenda kuiangalia kwa ujumla wake, biashara yako inakuwa kitu kimoja. Na hapo sasa unaweza kuigawa kwenye vipande vikuu vinne, ambavyo unahitaji kuweka nguvu ili kukuza biashara yako.

Kipande cha kwanza ni wateja.

Wateja ndiyo kipande cha kwanza muhimu sana cha biashara yako. Kama hakuna wateja basi hakuna biashara. Lazima uchague biashara yako inakwenda kuwahudumia watu gani, wanaopatikana wapi na unawafikiaje. Biashara lazima ijenge wateja ambao wanaotegemea kwa kile inachofanya.

Unapoingia kwenye biashara anza na kitu ambacho tayari watu wanajihitaji, hivyo wewe unakuja na suluhisho na kuhakikisha watu wanajua uwepo wako kwenye biashara hiyo. Hivi ndivyo unavyoweza kutengeneza wateja wa biashara yako.

Kipande cha pili ni mahitaji ya wateja.

Ukishachagua aina ya wateja ambao biashara yako inawahudumia, unapaswa kujua yale mahitaji yao ya msingi. Yale mahitaji yanayowasukuma kununua kile ambacho wewe unauza. Ukishayajua mahitaji hayo, jipange kuyatimiza kwa namna ambayo hakuna mfanyabiashara mwingine anayeweza kuyatimiza hivyo.

Kuna vitu viwili muhimu sana unapaswa kujua kuhusu mahitaji ya wateja wako, hofu na tamaa. Wateja wa biashara yako wanafanya maamuzi kwa kutumia hisia hizo mbili, labda wana tamaa ya kupata kitu fulani au wana hofu ya kupoteza kitu fulani. Jua hisia hizo mbili za wateja na zitumie katika mauzo.

Kipande cha tatu ni nafasi yako katika soko.

Biashara yoyote unayofanya, kuna nafasi ambayo upo kwenye soko, unaweza kuwa ndiyo namba moja yaani wateja wanakufikiria wewe kwanza au ukawa haupo kwenye namba za juu, yaani wateja hawakufikirii kabisa. Ili kukuza biashara yako, unapaswa kuwa kwenye nafasi ya juu kwenye soko lako. Unapaswa kuwafanya wateja wako wakufikirie wewe kwanza inapokuja kwenye mahitaji yao.

Matangazo, alama za kibiashara, rangi za kibiashara, kauli mbiu na hata utamaduni wa tofauti wa biashara yako ni vitu vinavyowafanya wateja wakukumbuke na kukufikiria muda mrefu. Tengeneza picha ya tofauti ya biashara yako ambayo inawafanya wateja wakufikirie wewe mara zote.

Kipande cha nne ni ubobezi wa biashara yako.

Je biashara yako imebobea kwenye nini? Biashara yako inajulikana kwa kipi? Je ni kitu gani wateja wanapata kwako ambacho hawawezi kupata kwa wafanyabiashara wengine?

Hayo ni maswali muhimu ya kupima ubobezi wa biashara yako. Biashara iliyobobea kwenye kile inachofanya ndiyo biashara ambayo inapata mafanikio makubwa sana.

Jua ni aina gani ya biashara unayofanya, na kipi cha tofauti unachotoa kwa wateja wako kisha kazana kutoa kitu hicho kwa namna ambayo wateja hawawezi kupata sehemu nyingine na utaweza kufanikiwa sana kwenye biashara unayofanya. Bobea kwenye vitu vichache na hilo litakufanya kinara kuliko kung’ang’ana kufanya vitu vingi.

TATU; VIUNGO VITATU VYA MFUMO BORA WA KUENDESHA BIASHARA.

Bishara zote zenye mafanikio zina mfumo rahisi wa kuziendesha, mfumo ambao kila anayehusika kwenye biashara hiyo anauelewa na kuweza kuutumia.

Mwandishi ametushirikisha mfumo rahisi wenye viungo vitatu ambao kila mtu anaweza kuutumia kuendesha biashara yake na akafanikwa sana.

Kiungo cha kwanza ni MAONO (VISION)

Maono ndiyo sehemu ya kwanza ya mfumo wa biashara yenye mafanikio. Maono ni ile picha kubwa ambayo biashara inafanya kazi kuifikia. Huu ndiyo mwongozo mkuu wa kule biashara inapokwenda. Bila ya maono biashara haiwezi kupiga hatua, itakuwa inaendeshwa kwa mazoea.

Kiungo cha pili ni MIKAKATI (STRATEGY)

Baada ya kuwa na maono, kunapaswa kuwa na mikakati ya kufikia maono hayo. Maono pekee hayatoshi kufanikiwa kwenye biashara, zipo hatua ambazo lazima zichukuliwe ili biashara iweze kufanikiwa. Bila ya mikakati sahihi na inayofanyiwa kazi, maono yanabaki kuwa ndoto.

Kiungo cha tatu ni UTEKELEZAJI (EXECUTION)

Ukishakuwa na maono na kuweka mikakati, kinachofuata ni kutekeleza mikakati hiyo. Utekelezaji wa mikakati ndiyo njia pekee ya kufikia maono makubwa ya kibiashara. Na utekelezaji haupaswi kuwa wa mazoea, badala yake wa ubunifu na utofauti mara zote ili kuweza kupiga hatua zaidi.

Kwenye biashara yako, ona jinsi gani viungo hivi vitatu vinaweza kufanya kazi. Anza na maono makubwa uliyonayo kibiashara, unataka kufika wapi siku 90 zijazo, miezi 6 ijayo, mwaka mmoja ujao, miaka 3 ijayo, miaka 5 ijayo, miaka 10, 20 na hata 50 ijayo. Ukishakuwa na picha hiyo, kaa chini na tengeneza mkakati wa kufanyia kazi ili kufika kwenye picha hiyo. Na ukishakuwa na mkakati, ufanyie utekelezaji huku ukikazana kuwa bora zaidi kila wakati.

NNE; MAAJABU YA MAONO.

Maono makubwa yana maajabu makubwa sana kwenye biashara. Maono ya biashara yaliyotengenezwa vizuri, yanaleta hamasa na msukumo mkubwa kwako mfanyabiashara na hata wale unaowaajiri kuchukua hatua kubwa kufikia maono hayo.

Maono mazuri ya biashara yana viungo vinne muhimu.

Moja ni maadili au miiko au misingi.

Maadili au miiko au msingi ni kile kitu ambacho biashara inasimamia. Hivi ni vitu ambavyo havipaswi kuvunjwa kabisa kwenye biashara. Maadili haya ndiyo yanaifanya biashara kuwa ya kipekee na hata kuwavutia watu kufanya kazi kwenye biashara hiyo.

Maadili ya biashara yanalenga kujibu maswali haya muhimu; ni kitu gani tunaamini kupitia biashara? Ni misingi gani ambayo hatupaswi kuivunja? Ni viwango gani ambavyo tutajipima navyo? Katika wakati wa changamoto ni namna gani mtu anafikia maamuzi sahihi? Ni kitu gani kinamsukuma mtu kufanya kazi kwenye biashara hii?

Kila biashara inapaswa kuwa na miiko au misingi yake ya maadili isiyopungua minne na isiyozidi sita. Misingi hii inapaswa kujulikana na kila aliyepo kwenye biashara hiyo.

Mbili ni kusudi.

Kila biashara inapaswa kuwa na kusudi la biashara hiyo kuwepo. Na kusudi hilo isiwe kupata faida pekee. Kusudi la biashara linapaswa kuwa ule mchango ambao biashara hiyo inatoa kwa wateja wake na jamii kwa ujumla.

Biashara zenye kusudi kubwa zaidi tu ya kupata faida huwa zinapata mafanikio makubwa kuliko zile zinazoangalia faida pekee. Siyo kwamba faida ni kitu kibaya, lakini msukumo unapokuwa ni wa kupata faida pekee, ni rahisi kufanya mambo ambayo siyo sahihi.

Kusudi la biashara ni sehemu ya maono ya biashara hiyo, ambayo inawafanya watu kuona umuhimu wao kwenye biashara hiyo.

Tatu ni malengo.

Maono yanatoa picha ya wapi biashara inaenda, lakini jinsi ya kufika pale biashara inapaswa kuwa na malengo na mipango ambayo inafanyiwa kazi. Hivyo sehemu ya maono ni malengo au misheni ya biashara hiyo. Malengo ndiyo njia ambayo maono yanatoka kwenye picha na kuja kwenye uhalisia.

Nne ni picha inayoshikika.

Kipengele cha nne cha maono ni picha inayoshika. Kumbuka maono ni picha kubwa ya biashara nzima, lakini kuna watu wanaofanya kazi kwenye biashara hiyo, hawa wanahitaji kitu cha kuwahamasisha kuchukua hatua kila siku. Hivyo hapa unahitaji kuwasaidia kutengeneza picha zinazowaonesha hatua watakazokuwa wamepiga pale maono yanapofikiwa. Kwa mtu kuona kwamba yeye binafsi atapiga hatua kama maono ya biashara yatafikiwa, anapata nguvu ya kujituma zaidi.

Tumia viungo hivi vinne kutengeneza maono makubwa ya biashara yako ambayo yataiwezesha kukua na kufanikiwa.

TANO; KUGEUZA MAONO KWENDA UHALISIA – MIKAKATI NA UTEKELEZAJI.

Ili biashara iweze kufanikiwa, inahitaji kuwa na njia ya kuyageuza maono kuwa uhalisia. Maono uliyotengeneza ni picha tu, ili iweze kuwa uhalisia unahitaji kufanyia kazi viungo viwili vya biashara ambavyo ni MIKAKATI NA UTEKELEZAJI.

Kutengeneza mkakati bora.

Wafanyabiashara wengi hufikiri ili kufanikiwa kwenye biashara wanahitaji mkakati wa tofauti na wa kipekee sana. Lakini ukweli ni kwamba mkakati wowote unaoendana na maono ya biashara ukifanyiwa kazi unaleta matokeo mazuri. Hivyo pitia maono yako na jiulize yanawezaje kuwa uhalisia, hapo weka mikakati ambayo inaweza kufanyiwa kazi.

Pia wengi wamekuwa wanaamini mikakati inayotengenezwa na washauri na wataalamu wa biashara ndiyo bora. Lakini ukweli ni kwamba mkakati bora kwa biashara yako ni ule ambao umeutengeneza wewe mwenyewe kwa kushirikiana na wafanyakazi wako. Hivyo weka vikao na wafanyakazi wako, waeleze maono ya biashara hiyo na kisha kwa pamoja tengenezeni mikakati ya kuyafikia. Mikakati inapotengenezwa kwa ushirikiano hivi, inawafanya watu kujituma zaidi.

Katika kutengeneza mkakati wa biashara yako, kuna tathmini tatu ambazo unapaswa kuzifanya;

Moja ni kufanya tathmini ya soko. Hapa unapaswa kujua ukubwa wa soko la biashara yako kwa kujua mahitaji ya wateja na wingi wa wateja hao.

Mbili ni kufanya tathmini sekta ya biashara. Baada ya kufanya tathmini ya kujua ukubwa na uhitaji wa soko, unapaswa kufanya tathmini ya sekta ya biashara. Hapa unaangalia washindani waliopo kwenye soko lako na nguvu yao ya kuwashinda.

Tatu ni kufanya tathmini binafsi.  Hapa unaitathmini biashara yako na kuangalia uwezo wake wa kulifikia soko na kupambana na ushindani uliopo. Hapa utaona rasilimali muhimu zinazohitajika ili kuweza kulifikia soko na kuvuka ushindani.

Zipo njia tatu za kutengeneza mkakato bora wa kufanikiwa kibiashara.

Moja ni kupunguza gharama za kuendesha biashara na hivyo kuweza kubaki na faida kubwa.

Mbili ni kujitofautisha na wafanyabiashara wengine, kutoa kile ambacho mteja hawezi kupata sehemu nyingine.

Tatu ni kuchagua eneo la kubobea na kuweka umakini wako. Kwa kuchagua eneo la kubobea, unajitofautisha na wengine.

Uchukuaji hatua wa kipekee.

Baada ya kuwa na mkakati bora wa biashara yako, kinachofuata ni kutekeleza mkakati huo, yaani kuchukua hatua.

Katika kutekeleza mikakati ya biashara, kuna vitu viwili muhimu vya kufanyia kazi.

Kitu cha kwanza ni kuwa na mpango kazi. Huu ni mpango ambao unaeleza jinsi mkakati unavyotekelezwa, kwa kila hatua inayopaswa kuchukuliwa na jinsi ya kuchukua hatua hiyo. Mkakati unaleza nini kifanywe, mpango kazi unaeleza kitu hicho kinafanywaje.

Kitu cha pili ni kuwa na bajeti ya utekelezaji. Fedha, muda na nguvu ni rasilimali muhimu zenye ukomo kwenye biashara yako. Kama hazitapangiliwa vizuri vitatumika vibaya na mikakati haitaweza kutekelezwa. Tengenea bajeti ya matumizi ya fedha, muda na nguvu kwenye kila mpango kazi unaofanyiwa kazi ili kuweza kupima ufanisi na kuzalisha matokeo mazuri.

SITA; NADHARIA YA KUJIHUISHA.

Kama tulivyojifunza kwenye neno la juma hapo juu, biashara kwa asili huwa zinatungwa, zinazaliwa, zinakua, zinakomaa na kufa. Ili biashara yako iweze kuwa na mafanikio lazima iweze kuvuka mzunguko huo wa kuzaliwa na kufa na badala yake iweze kujihuisha kila wakati.

Njia bora ya kuihuisha  biashara yako ni kupitia vipande vikuu vinne vya biashara yako. Kila wakati angalia ni hatua ipi ya tofauti unaweza kufanya kwenye kila kipande na biashara yako ikawa mpya.

Kwa upande wa wateja, angalia wapi unaweza kupata wateja wapya kwa bidhaa uliyonayo sasa, au kutengeneza bidhaa mpya kwa wateja ulionao sasa.

Kwa upande wa mahitaji, angalia ni mahitaji gani mapya ambayo wateja wako wanayo na unaweza kuyatimiza.

Kwa upande wa nafasi yako kwenye soko, angalia ni kwa namna gani unaweza kujitofautisha zaidi na washindani wako na wateja wakakufikiria wewe tu.

Na kwa upande wa ubobezi, angalia maeneo mapya unayoweza kubobea na ukawahudumia zaidi wateja ulionao au wateja wapya.

Kila wakati biashara yako inapaswa kutengeneza wateja wapya na kuwafanya wateja waliopo waendelee kununua ili isife. Kama biashara haitengenezi wateja wapya, na wale waliopo hawaendelei kununua, biashara hiyo inakufa.

SABA; TENGENEZA UTAMADUNI WA KUJIFUNZA KWA KILA MMOJA.

Ili biashara iweze kukua, lazima wewe mmiliki wa biashara na wafanyakazi waliopo kwenye biashara hiyo wawe wanajifunza. Na sehemu ya kwanza kujifunza ni kutoka kwa kila mmoja. Kila mtu kuna kitu anajua kupitia anachofanya, ambapo akiwashirikisha wengine nao watajifunza pia.

Hivyo tengeneza mazingira na utamaduni wa watu kujifunza kutoka kwa wenzao na kuboresha ufanisi na uzalishaji wao.

NANE; KUHUSU UONGOZI NA USIMAMIZI.

Hivi ni vitu viwili ambavyo vimekuwa vinachanganywa sana kwenye biashara. Ili biashara yako ifanikiwe, inakuhitaji wewe kuwa kiongozi bora lakini pia uweze kuwa msimamizi mzuri.

Tofauti ya uongozi (leadership) na usimamizi (management) ni kwamba watu wanachagua kumfuata kiongozi kutokana na maono makubwa aliyonayo. Lakini usimamizi ni kuhakikisha mikakati iliyowekwa inafanyiwa kazi, na msimamizi haangalii kama watu wanamfuata au la, yeye anachoangalia ni majukumu yametekelezwa.

Ili biashara yako ifanikiwe, inakuhitaji wewe uwe kiongozi mzuri, ambaye una maono makubwa ya biashara hiyo, unaweza kuyaeleza maoni hayo kwa wengine, unaweza kuwahamasisha wengine na kuwapa matumaini na watu hao kuchagua kuambatana na wewe, wakiamini mnakwenda sehemu salama na kila mtu ataweza kupiga hatua.

Lakini pia uongozi pekee haitasaidia kufanikiwa kwenye biashara, unahitaji pia kuwa msimamizi (manager) ambapo unahakikisha mikakati na mipango iliyowekwa imetekelezwa kama ilivyopangwa.

Mambo muhimu ya kuzingatia kwenye kuwaongoza na kuwasimamia watu.

Katika nafasi yako kama kiongozi na msimamizi wa biashara, unahitaji kufanya kazi na watu vizuri ili waweze kupata hamasa ya kutekeleza majukumu yao, lakini pia wayatekeleze vizuri.

Yafuatayo ni mambo ya kuzingatia;

  1. Ondoa ile dhana ya ubosi. Watu wanahamasika zaidi pale wanapoona mnashirikiana kwenye kitu na siyo wako chini ya mtu kwenye kufanya kitu. Hivyo endesha unachofanya kama ushirikiano na wale wanaokusaidia.
  2. Onesha kwa mfano, chochote ambacho unataka watu wafanya, wataelewa na kufanya kama utakifanya wewe mwenyewe.
  3. Tengeneza uadilifu kwako wewe na kwa wengine pia, watu wanapoona wewe ni mwadilifu, wanakuamini na kuwa tayari kufanya kazi na wewe.
  4. Tengeneza hali ya usawa, watu wote wachukuliwe kwa usawa kulingana na kazi zao. Pasiwepo na hali ya upendeleo kwa baadhi ya watu, hilo linawagawa sana watu.
  5. Tengeneza utamaduni wa kuheshimiana, kwa kuanza na wewe kuwaheshimu wasaidizi wako na wao wenyewe kuheshimiana. Watu wanapojua wanaheshimiwa wanajituma zaidi.

TISA; MCHAKATO NA MFUMO WA UDHIBITI.

Baada ya kuwa na mkakati ambao unatekelezwa katika kufikia maono makubwa ya kibiashara ambayo unayo, siyo kwamba kila kitu kitakwenda vizuri. Vikwazo na changamoto ni sehemu ya safari hiyo ya mafanikio ya kibiashara.

Hivyo kuna vitu viwili vya kuzingatia kwenye safari hii.

Kitu cha kwanza ni mchakato unaofanyiwa kazi. Hapa kunakuwa na miongozo ambayo inaeleza majukumu mbalimbali ya biashara yanafanyiwaje kazi. Miongozo hii inamsaidia kila mtu kwenye kutekeleza majukumu yake. Na haya mtu mpya anapoletwa kwenye majukumu hayo, ni rahisi kujua kipi anapaswa kufanya.

Kitu cha pili ni mfumo wa udhibiti. Mfumo wa udhibiti unaeleza mipaka ya kila jukumu ambalo mtu anafanyia kazi. Hii inaeleza nini kinapaswa kufanywa na kipi ambacho hakipaswi kufanywa. Mifumo hii ya udhibiti inapunguza makosa mbalimbali yanayoweza kufanyika pale mtu anapokuwa hana mipaka. Unapaswa kuweka mipaka ya utekelezaji wa kila jukumu ambalo mtu anafanyia kazi na pia kuwa na njia ya kupima ufanisi wa watu kwenye kila jukumu ili kujua wanafanya kwa kiasi na kiwango gani. Katika mifumo hii ya udhibiti pia unapima muda unapotea, na makosa yanayofanyika kwenye biashara na kuja na njia bora za kuokoa kinachopotea na kurekebisha pamoja na kuzuia makosa yanayofanyika.

KUMI; KUHUSU FEDHA.

Fedha ni eneo lenye changamoto kubwa kwa wafanyabiashara wengi. Wengi huwa wanafurahi kuona mauzo yanafanyika, lakini hawajui kama biashara inajiendesha kwa faida au hasara.

Ili uweze kufanikiwa kwenye biashara, lazima uwe na msingi mzuri sana kwenye usimamizi wa fedha za biashara yako. Haitoshi tu kujua mapato na matumizi ya biashara, bali unapaswa kujua gharama za kuendesha biashara yako, jinsi ambavyo mtaji umewekezwa, na hata mwenendo wa biashara yako kwa siku zijazo.

Kuna taarifa tatu muhimu sana za kifedha ambazo kila mfanyabiashara anapaswa kuzijua na kuzifanyia kazi.

Taarifa ya kwanza ni FAIDA NA HASARA (PROFIT AND LOSS)

Hii ni taarifa inayoonesha kama biashara imepata faida au hasara katika kipindi husika. Taarifa hii inaonesha mapato yanayotokana na mauzo na kisha kuondoa gharama za mauzo na gharama za kuendesha biashara. Kama mapato ni makubwa kuliko gharama za mauzo na za kuendesha biashara basi biashara inajiendesha kwa faida. Na kama mapato ni madogo kuliko matumizi, biashara inajiendesha kwa hasara.

Taarifa ya pili ni MALI NA MADENI (BALANCE SHEET)

Hii ni taarifa inayoonesha msimamo wa biashara kwa wakati inachukuliwa. Taarifa hii inaonesha jinsi mtaji wa biashara umetumika, uwekezaji uliofanywa na biashara, fedha iliyopo na madeni ambayo biashara inadai na kudaiwa. Kwa kupata picha hii ya mali na madeni, ni rahisi kuona afya ya biashara. Taarifa hii ya mali na madeni inapima kama biashara itafungwa leo, je italeta faida kwa mmiliki au itakuwa imefilisika.

Taarifa ya tatu ni MZUNGUKO WA FEDHA (CASHFLOW STATEMENT)

Taarifa ya mzunguko wa fedha inakuonesha afya ya biashara yako kifedha kwa wakati husika. Taarifa ya faida na hasara inaweza kuonesha hasara kwa sababu inapima kipindi cha nyuma. Lakini taarifa ya mzunguko wa fedha inapima kuingia na kutoka kwa fedha kwenye biashara kwa wakati husika. Hivyo kila wakati unapaswa kuwa na taarifa ya fedha zinazoingia na kutoka kwenye biashara. Kama zinazoingia ni nyingi kuliko zinazotoka basi mzunguko ni chanya na kama zinazotoka ni nyingi kuliko zinazoingia basi mzunguko ni hasi.

Kwenye #MAKINIKIA ya juma hili nitakwenda kukushirikisha jinsi ya kuandaa na kutumia taarifa hizo tatu kwa ukuaji wa biashara yako.

Hayo ndiyo yale muhimu sana niliyokuandalia kutoka kwenye kitabu JUST RUN IT, ambayo ukiyafanyia kazi utaweza kutengeneza biashara bora, inayoweza kujiendesha yenyewe na kwa mafanikio makubwa sana.

#3 MAKALA YA JUMA; SIRI 101 ZA MAFANIKIO KWENYE BIASHARA USIZOFUNDISHWA SHULENI.

Watu wengi huenda kwenye vyuo kujifunza maarifa sahihi ya kufanikiwa kwenye kazi na biashara. Na wale watu ambao wamesoma na kupata shahada ya uzamivu ya usimamizi wa biashara (MBA), huwa wanaonekana watu wenye uelewa mkubwa sana kwenye kuendesha biashara na hata kazi nyingine wanapokuwa wameajiriwa kwenye makampuni.

Pamoja na mambo mengi mazuri ambayo watu wanajifunza chuoni wakati wanasomea biashara, kuna mambo muhimu 101 ambayo hayafundishwi kwenye vyuo hivi. Mambo hayo 101 ndiyo yanachangia sana kwenye mafanikio ambayo mtu atapata kwenye maisha yake baada ya kumaliza masomo.

Mwandishi Chris Haroun kwenye kitabu chake kinachoitwa 101 Crucial Lessons They Don’t Teach You in Business School ametushirikisha mambo hayo 101 ambayo kila mmoja wetu anapaswa kuyajua ili kuweza kufanikiwa kupitia kazi na biashara tunazofanya.

Kwenye makala ya juma hili nimekushirikisha mambo hayo 101, kama hukupata nafasi ya kuisoma makala hiyo, isome sasa hapa na uondoke na mambo ya kwenda kufanyia kazi kwenye maisha yako. Fungua; Siri 101 Za Mafanikio Kwenye Biashara Ambazo Hazifundishwi Popote Pale.

Endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kila siku upate makala nzuri zenye mafunzo na hamasa ya kufanikiwa zaidi.

#4 TUONGEE PESA; KWA NINI WENYE UELEWA WA FEDHA SIYO WAZURI KWENYE BIASHARA.

Watu ambao wana uelewa mkubwa sana wa fedha, yaani wahasibu, wanahisabati, wachumi na hata washauri wa mambo ya fedha, huwa siyo wafanyabiashara wazuri. Yaani huwa wakiingia kwenye biashara hawafanikiwi ukilinganisha na wasiokuwa na uelewa mkubwa wa fedha.

Huku watu wasiokuwa na uelewa mkubwa wa fedha, ambao hawajui hata kuandika cheki vizuri, wakiingia kwenye biashara wanafanikiwa sana.

Katika maeneo mengi ya maisha, kadiri mtu anavyokuwa na uelewa mkubwa, ndivyo anavyochelewa kufanya maamuzi. Wale wenye uelewa mdogo, wanafanya maamuzi haraka, lakini wenye uelewa mkubwa wanahusisha mambo mengi kwenye maamuzi na hilo linawachelewesha kufikia maamuzi.

Inapokuja kwenye fedha, wasiokuwa na uelewa mkubwa kwenye fedha wanatumia hesabu za aina tano tu kwenye mambo ya kifedha, kujumlisha, kutoa, kugawanya, kuzidisha na asilimia. Ni hesabu hizo tu zinazotosha kuendesha biashara yenye mafanikio.

Wakati wale wenye uelewa mkubwa wa fedha wanakuwa na hesabu nyingi zaidi wanazotumia kwenye maamuzi, mfano, makadirio (projections), uwezekano (probaility), hatari (risk) na nyingine nyingi katika kufanya maamuzi, kitu ambacho kinawachelewesha na hata maamuzi wanayofanya yanakosa uhalisia.

Kama wewe una uelewa mkubwa wa kifedha na unataka kufanikiwa kwenye biashara, kubali kuweka sehemu ya uelewa wako pembeni na uendeshe biashara kwa  vitendo na siyo nadharia.

Unaposoma taarifa za kifedha, angalia zile hatua unazoweza kuchuka ili kukuza biashara yako sasa badala ya kuhangaika na vitu vya kufikirika.

Ukishajua MAGAZIJUTO basi una maarifa ya kifedha ya kukutosha kufanikiwa kwenye biashara yako. Muhimu ni kuzijua namba zako muhimu kwenye biashara kama masoko, mauzo, gharama za kuendesha biashara, faida na mtaji ili uweze kuendesha biashara yenye mafanikio makubwa.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; VITU VIWILI VINAVYOITOFAUTISHA BIASHARA.

“The core values and the purpose of a business are what distinguish it from every other business and mark it, throughout its lifetime, as special. Economies cycle, technology marches on, customer tastes change, and industries come and go, but the DNA of great businesses, regardless of how they evolve over time, stay the same, just as we humans remain the same as we transition from infancy through adolescence to maturity and old age.” – Dick Cross.

Biashara zinazofanikiwa huwa zina upekee ambao haupo kwenye biashara nyingine yoyote ile. Hata kama kwa nje biashara hiyo inaonekana kufanana na nyingine, lakini kwa ndani ipo tofauti kabisa. Na utofauti huo wa ndani ndiyo unaoifanya biashara ifanikiwe sana.

Kuna vitu viwili ambavyo vinatofautisha biashara yoyote ile, vitu hivyo ni misingi au maadili ya biashara na kusudi la biashara. Misingi ni kile ambacho biashara inasimamia, ile miiko ambayo biashara inasimamia katika uendeshaji wake. Na kusudi la biashara ni ile sababu ya biashara kuwepo, kile kitu cha tofauti ambacho biashara hiyo inafanya kwa wateja wake.

Vitu hivi viwili, miiko na kusudi ndiyo DNA ya biashara yoyote ile. Hivi ndiyo vinaifanya biashara iweze kusimama licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali. Kama ambavyo mtu akikatwa mkono hazai mtoto aliyekatika mkono, ndivyo hivyo pia biashara inaweza kuendelea vizuri licha ya changamoto za nje, kwa sababu msingi wa ndani ni imara.

Kwa biashara unayofanya au kutegemea kufanya, anza kujiwekea msingi au miiko ambayo utaisimamia kwenye biashara hiyo. Kisha jua kusudi la biashara hiyo kuwepo, inatatua tatizo au kutimiza mahitaji gani ambayo watu wanayo. Ukiwa na vitu hivi viwili, utakuwa na biashara yenye mafanikio makubwa.

Hizi ndiyo tano za juma la 26, ambazo zimejikita sana kwenye kutengeneza mfumo mzuri wa kuendesha biashara yenye mafanikio. Pia umejifunza siri 101 za mafanikio kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla. Fanyia kazi haya uliyojifunza ili uweze kupiga hatua zaidi.

Kwenye #MAKINIKIA tutakwenda kujifunza jinsi ya kuandaa na kutumia taarifa tatu muhimu za kifedha kwenye biashara yako, yaani taarifa ya faida na hasara (PROFIT AND LOSS), taarifa ya mali na madeni (BALANCE SHEET) na taarifa ya mzunguko wa fedha (CASHFLOW STATEMENT). Hizi ni taarifa tatu ambazo kila mtu aliyepo kwenye biashara anapaswa kuzijua kwa undani na kuzitumia kufanya maamuzi. Tutajifunza hili kwa kina kwenye #MAKINIKIA ya juma hili.

#MAKININIA yanapatikana kwenye channel ya TELEGRAM YA TANO ZA JUMA, ili kupata mafunzo hayo unapaswa kujiunga na channel hiyo. Kwa kuwa kwenye channel hiyo pia unapata uchambuzi wa kina wa vitabu pamoja na vitabu vinavyochambuliwa. Maelezo ya kujiunga na CHANNEL YA TANO ZA JUMA yako hapo chini. Yasome na uchukue hatua sasa.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu