Kuna sehemu ya kila kitu na kila kitu kina sehemu yake.

Huu ni msingi mmoja ambao ukiishi utaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yako.

Kwa sababu kikwazo kwa wengi kupiga hatua ni kukosa msimamo kwenye yale wanayofanya.

Mtu anapanga kufanya kitu fulani, lakini unapofika wakati wa kufanya anaahirisha na kujiambia atafanya baadaye au kesho. Wengi husubiri mpaka wakati wa mwisho kabisa ndipo wafanye kitu.

Hali hii inasababisha ubora wa kile kinachofanywa kuwa mdogo na hata matokeo kutokuwa mazuri.

Lakini kama utaishi kwa msingi wa kila kitu na sehemu yake, ina maana unapopanga kufanya kitu, unafanya kama ulivyopanga, huruhusu kitu chochote kuingilia mipango yako.

Unapojiwekea misingi unasimamia misingi hiyo, hakuna kinachoweza kukuteteresha kwenye misingi hiyo. Kwa kusimamia kile ulichopanga au msingi uliojiwekea, unajipunguzia matatizo mengi kwenye maisha yako.

Angalia matatizo mengi ambayo watu wanayo kwenye maisha, wanajua kabisa njia sahihi za kuepuka matatizo hayo au kuyatatua, lakini wengi hawachukui hatua ambazo wanapaswa kuzichukua.

Unafikiri kuna mtu mwenye uzito ulipitiliza ambaye hajui ni njia zipi sahihi za kuondoka kwenye tatizo la uzito? Au mtu ambaye yupo kwenye madeni na hajui njia sahihi za kuondoka kwenye madeni hayo?

Watu wanajua kila kitu sahihi wanachopaswa kufanya, lakini hawafanyi. Kwa sababu hawajajijengea msingi wa kila kitu na sehemu yake. Wanapanga kufanya kitu lakini wanaruhusu usumbufu uingilie katika kutekeleza mipango yao. Wanajiwekea utaratibu ambao wanapaswa kuufuata lakini wanauvunja utaratibu huo wao wenyewe.

Rafiki yangu, ishi kwa msingi huu mmoja; kuna sehemu ya kila kitu na kila kitu kina sehemu yake. Kwa kufuata msingi huu, utaweza kufanya yale uliyopanga kufanya na kusimamia misingi unayojiwekea.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha