Katika zama zilizopita, kitu kikubwa kilichowatofautisha wale waliofanikiwa na walioshindwa kilikuwa ni mawazo bora.
Wale waliofanikiwa sana walionekana kuwa na mawazo bora kuliko wale ambao wameshindwa.
Katika zama hizo, watu wachache walihodhi mawazo bora sana ambayo yaliwawezesha kupiga hatua kubwa kwenye maisha yao.
Lakini zama zimebadilika, kwa sasa tunaishi kwenye zama za maarifa na taarifa, ambapo mawazo ni mengi sana kuliko uwezo wa mtu kuyatekeleza.
Wingi huu wa mawazo umefanya mawazo yasiwe na thamani kubwa sana kwenye mafanikio kama kipindi cha nyuma.
Katika zama hizi, kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa ni hatua ambazo mtu anachukua baada ya kupata wazo.
Wapo ambao wakipata wazo wanasubiri mpaka kila kitu kiwe tayari ndiyo waanze kufanyia kazi wazo walilonalo. Kwa njia hii wamekuwa hawaanzi, kwa sababu hakuna wakati kila kitu kitakuwa tayari kwa wewe kuweza kuanza.
Na wapo ambao wakipata wazo hawasubiri, badala yake wanachukua hatua mara moja, hata kama hawajawa tayari, wanachukua hatua sasa na kuendelea kujifunza. Hawa ndiyo watu wanaofanikiwa sana kwenye zama tunazoishi sasa.
Lakini pia wingi huu wa mawazo ambayo yote yanaonekana bora ni mtego kwenye mafanikio ya wengi. Wengi wamekuwa wanakimbizana na mawazo mapya wanayokuana nayo kiasi kwamba wanashindwa kuweka muda na juhudi za kutosha kwenye wazo moja mpaka wapate matokeo bora. Wengi wanajikuta wakijaribu kila wazo jipya linalowajia na hilo linawafanya wasiweze kupiga hatua kubwa.
Weka thamani kubwa kwenye hatua unazochukua na siyo kwenye wazo pekee. Na pia jiwekee ukomo wa aina gani ya mawazo utakayofanyia kazi, usiwe mtu wa kukimbizana na kila wazo jipya. Chagua mawazo yanayoboresha kile ambacho umechagua kufanya na yatumie hayo kupiga hatua zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,