Ili moto uwake unahitaji vitu vitatu viwepo.
Moja lazima kuwe na cheche zinazoanzisha moto huo.
Mbili lazima kuwe na nishati inayofanya moto huo uwake.
Tatu lazima kuwe na hewa ya oksijeni ambayo inafanya moto huo uendelee kuwaka.
Ili kuzima moto, au kuzuia usiwake, basi unahitaji kuondoa vitu hivyo vitatu. Uzuri ni kwamba ukiondoa kitu kimoja tu kati ya hivyo vitatu, moto unazima kabisa.
Sasa tukirudi kwenye maisha yetu ya kawaida, kuna moto ambao tumekuwa tunawasha au kuchochea kwenye maisha yetu ya kila siku.
Sehemu kubwa ya moto huo ni kwenye hisia ambazo tunakuwa nazo kwetu wenyewe na hata kwa wengine pia.
Hisia zetu binafsi hasa zile hasi na za kukata tamaa, huwa zinajichochea na kuwa kubwa sana. Kinaweza kutokea kitu kidogo sana, labda umemsalimia mtu hakuitika, hapo hapo ukaanza kujipa mawazo mbalimbali, kwamba mtu huyo anakudharau, hakuna anayekujali, maisha yako hayana maana na kadhalika. Unapata hisia hizo na zinakua zaidi kwa sababu unazichochea.
Hisia zetu kwa wengine mfano chuki, hasira, wivu na kadhalika nazo pia huwa zinakuwa kwa sababu tunazichochea. Mtu anafanya kitu kimoja na ghafla tunaanza kujikumbusha mambo yote mabaya ambayo wamewahi kufanya. Tunasahau kabisa mazuri ambayo amewahi kufanya na tunaona mabaya tu.
Pia kwenye hali ya kutokuelewana na wengine, huwa tunachochea wenyewe. Mfano mtu amekasirika na wewe unakasirika, anakujibu vibaya na wewe unamjibu vibaya, hali hii inajichochea na kuleta madhara makubwa zaidi.
Suluhisho ni kuacha kuchochea, iwe ni kwako mwenyewe au kwa wengine, jikamate pale unapoanza kujenga hisia hasi juu yako mwenyewe au wengine na kisha acha mara moja kuchochea hisia hizo. Achana na kile unachofikiria na fikiria kitu kingine cha tofauti. Au ondoka pale ulipo na nenda sehemu nyingine ambayo mazingira yake hayachochei. Mfano kama upo kwenye hali ya kutokuelewana na mtu, kuondoka pale ulipo na kufanya matembezi kutakupa nafasi ya kuacha kuchochea hali hiyo na hata kufikiri kwa usahihi zaidi.
Ukishagundua umewasha moto, basi hatua ya kwanza ni kuacha kuuchochea moto huo. Utajiepusha na mengi kwa sababu kama tunavyojua, moto ni hatari.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,