Kuna jambo moja la kushangaza sana kwenye zama tunazoishi sasa, watu wanatumia muda mwingi kwenye kazi zao, lakini uzalishaji na ufanisi wao ni mdogo mno.
Watu watakuambia wanafanya kazi masaa 16 mpaka 18 kwa siku, wanafanya kazi usiku na mchana, lakini ukiangalia matokeo wanayozalisha, hayana tofauti kubwa na wale wanaofanya kazi kwa muda mchache.
Ni kweli mtu akiweka muda zaidi kwenye kazi anaweza kufanikiwa zaidi. Lakini kinachohitajika kupata mafanikio kwenye kazi siyo muda pekee, bali umakini unahitajika sana.
Kama unafanya kazi huku umezungukwa na usumbufu, hutaweza kuwa na uzalishaji na ufanisi mzuri.
Mfano unafanya kazi inayohitaji umakini, lakini simu yako iko pembeni yako, hivyo simu pamoja na jumbe zinaingia na unazijibu. Unaweza kuona ni kitu kisichokuwa na madhara, lakini kinaathiri sana kazi unayofanya.
Kama unafanya kazi huku unatumia simu, ukifanya kazi hiyo kwa masaa matano, ni sawa na anayefanya kazi hiyo kwa saa moja huku akiwa hana usumbufu wowote ule.
Hivyo basi, kama unataka kuboresha kazi unayofanya, tenga muda ambao utafanya kazi bila ya usumbufu. Muda huo unaokuwa umetenga ni kwa ajili ya kazi tu na simu wala usumbufu mwingine haupo karibu.
Tenga angalau masaa 3 mpaka 5 kwa siku ya kufanya kazi yako kwa umakini mkubwa, na utaweza kuzalisha matokeo makubwa sana.
Na kama kazi unayofanya inakuhitaji muda wote kuwa hewani, basi unahitaji kuitengeneza upya siku yako, kuhakikisha unapata masaa yako mawili mpaka matatu ya kazi kabla ya siku yako ya kikazi haijaanza.
Mfano kama siku yako ya kikazi inaanza saa mbili asubuhi, basi unahitaji kuitengeneza siku yako tofauti. Amka asubuhi na mapema na pata muda wa kufana kazi zako muhimu kabla siku ya kazi haijaanza.
Ukiweka muda na umakini kwenye chochote unachofanya, utaweza kupata matokeo bora sana kwako. Tenga muda ambao utakuwa ni wa kazi tu na hakuna usumbufu mwingine wowote na utaweza kuwa na ufanisi na uzalishaji mkubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,